Mbinu 20 za kumfanya mtoto aweze kuongea mapema

Oct 5, 2018
33
58
1. Kujiongelesha mwenyewe. Jiongeleshe mtoto akiwa karibu juu ya mambo unayoyafanya. Mfano, naosha vyombo sasa, napika chakula, nafagia nyumba.

2. Simama, mpe mtoto muda wa kujibu. Unapozungumza na mtoto, kaa kimya, mpe nafasi ya kujibu. Akishindwa kujibu msaidie kujibu kisha mtake arudie kujibu.

3. Ongeza neno moja kila siku kwenye maneno ya mtoto. Kazania neno moja siku nzima. Kwa mfano, Chakula. Hakikisha wiki nzima mtoto awe amejifunza maneno angalau 7 mpaka 10.

4. Cheza gemu la kuweka vitu kwenye boksi na mtoto. Mchezo huu ni wa kuchukua vitu unaweka kwenye boksi. Unaweza ukaweka nje ya boksi viatu, shati, simu, kichanuo, kikombe, kijiko na vinginevyo kisha ukaanza: unaweka kijiko unasema kwa sauti naweka kijiko. Kisha zamu ya mtoto kucheza mwambie weka kijiko, weka kikombe, weka kiatu. Hakikisha akishindwa unamsaidia kuweka.

5. Mpe mtoto nafasi ya kuchagua. Unapotaka kumpa mtoto kitu muulize, unataka hiki au hiki? Mpe nafasi ya kuchagua. Ukimpa mtoto nafasi ya kuchagua utamlazimisha kuongea au kuonesha ishara.

6. Ongea kwa sauti mambo anayofanya mtoto. Ukiwa karibu na mtoto, hakikisha unasema mambo anayofanya mtoto. Kwa mfano, umekaa chini, unakula chugwa, unalia na mengineyo.

7. Mwambie mtoto mambo unayotaka aseme. Mwamie mtoto sema kichwa, sema tumbo, sema kikombe kila mara. Hakikisha umeanza na kila kitu kilichopo ndani ya nyumba. Pia, anza na maneno ya msingi kujieleza kama sema naomba, sema asante, sema nimeshiba, sema kukojoa.

8. Mfundishe mtoto kurudia maneno yanayosemwa na wengine. Hii itamsaidia kuiga maneno na jinsi yanavyotamkwa.

9. Muulize maswali mengi mtoto. Muulize mtoto maswali mengi yanayohitaji majibu. Maswali mengi yatamfanya mtoto aanze kutafuta maneno yakutumia. Maswali kama unafanya nini? Unakula nini? Kiatu kiko wapi? Baba yupo wapi? Mtoto akishindwa kujibu, mjibie kisha mwambie arudie ulivyosema.

10. Muoneshe mtoto picha mara kwa mara. Taja kwa majina vitu vinavyoonekana kwenye picha. Kwa mfano, kwenye picha anaonekana ni paka, mwambie mtoto huyu ni paka. Mwambie mtoto arudie kusema paka mara kadhaa.

11. Mwache mtoto aombe/aseme anachotaka. Hata kama unajua mtoto anachotaka muache aseme, usimpe mpaka aseme au auneshe juhudi kujieleza. Kama hawezi kujieleza muulize unataka chugwa? Akisema au kuonesha ishara ya ndiyo mwambie aseme chugwa.

12. Tumia sentensi fupi kuongea na mtoto. Sentensi kama kaa chini, kula chakula, lala, amka, twende dukani. Senstensi za namna hii zitachochea uelewa wa mtoto. Tumia sentensi hizi huku ukionesha vitendo, mara nyingine fanya kitendo akione.

13. Tumia lugha ya ishara unapozungumza na mtoto. Muoneshe ishara mbalimbali kama vile hapana huku ukitikisa kichwa, inuka huku ukionesha ishara ya mikono ya kuinuka, kula huku ukionesha ishara ya mkono kwenda mdomoni.

14. Imba nyimbo nyingi za kitoto kwa mtoto. Nyimbo hujenga sana lugha ya mtoto. Tafuta vitabu vya nyimbo, hakikisha haipiti siku bila kuimba nyimbo na mtoto.

15. Rudia maneno anayoyasema mtoto kwa usahihi. Mtoto akikosea kusema neno usimcheke, lirudie kulisema kwa usahihi na kwa mkazo zaidi.

16. Soma vitabu vya hadithi na mtoto. Hakikisha kila jioni kabla mtoto hajalala unamsomea vitabu vya hadithi. Vitabu vinaoneza maneno kwa mtoto, unapomsomea hakikisha unavitaja kwa majina viitu vyote unavyokutana navyo pindi unavyomsomea.

17. Zima kabisa Televisheni na simu. Usimpe kabisa mtoto simu au kumuwashia televisheni mpaka utakapoona ameanza kuzungumza vizuri. Vifaa vya kielektroniki huingilia maendeleo ya ubongo ya mtoto, huweza kuingilia upande unaohusika na lugha pia.

18. Mtoto acheze na watoto wenzake. Hakikisha mtoto anapata angalau masaa manne kwa siku ya kucheza na watoto wenzake.

19. Mpigie mtoto makofi au mshangilie akiongea neno lolote vizuri. Mtoto atahamasika kuongea maneno mengine vizuri.

20. Usitumie sauti ya ukali unapozungumza na mtoto. Mtoto anapojifunza kuongea anahitaji kuwa katika hali ya uhuru, hali ya kutokuwa na uwoga. Endapo utatumia lugha ya ukali kila mara mtoto anaweza kuwa mkimya, kukwepa kuongea lolote.

 
Ahsante kwa kuniongezea maarifa, lakini mpaka leo sijaiyona hasara ya mtoto kuchelewa kuongea.
 
Ahsante kwa kuniongezea maarifa, lakini mpaka leo sijaiyona hasara ya mtoto kuchelewa kuongea.
nakutana na watoto wenye miaka mpaka saba hawajaweza kuongea. Unadhani wataanza shule muda gani? kuchelewa kuongea kusipopewa suluhisho kunaweza kumfanya mtoto awe nyuma kwenye kila kitu. Pia, watoto wanaochelewa kuongea kwasababu ya autism usipowatafutia suluhu huwa hawawezi kutumia lugha kabisa mpaka utu uzima wao.
 
nakutana na watoto wenye miaka mpaka saba hawajaweza kuongea. Unadhani wataanza shule muda gani? kuchelewa kuongea kusipopewa suluhisho kunaweza kumfanya mtoto awe nyuma kwenye kila kitu. Pia, watoto wanaochelewa kuongea kwasababu ya autism usipowatafutia suluhu huwa hawawezi kutumia lugha kabisa mpaka utu uzima wao.
nimesema sijaona(binafsi) nasikia kwako mtoto miaka 7 hajui kuongea, vipi huyo sio bubu kweli?
 
nimesema sijaona(binafsi) nasikia kwako mtoto miaka 7 hajui kuongea, vipi huyo sio bubu kweli?
Sawa. Binafsi nimekutana nao, ni wengi. Sio mabubu, wanahitaji msaada tu. japo kwa umri huo unakuwa umechelewa sana. Jamii inadanganyana kwamba sio kitu kibaya mtoto kuchelewa. Wazazi wahimizwe kuwasaidia watoto mapema.
 
The early is better.
Uwezo wa kujifunza unaanzia kwenye mawasiliano, na mwenye uwezo wa kuwasiliana ana faida kubwa ya kujikubali, kukubaliwa na kujiamini.
 
Sawa. Binafsi nimekutana nao, ni wengi. Sio mabubu, wanahitaji msaada tu. japo kwa umri huo unakuwa umechelewa sana. Jamii inadanganyana kwamba sio kitu kibaya mtoto kuchelewa. Wazazi wahimizwe kuwasaidia watoto mapema.
Mwanangu anaongea huyo angali bado mdogo sana mpaka namshangaa sijui nimetumia mbinu gani kati ya hizo.
 
Nina ndugu yangu m'moja boya kweli kweli. Eti anamfundisha mtoto wake kuzungumza lugha ya malkia 100% na 24/7.

Anawakataza nyumbani kwake wadada wa kazi kumuwekea mtoto program za tv za kiswahili hata iwaje anataka mtoto awekewe katuni 24/7 na kuongeleshwa kiingereza tu.

Nikatest nae mitambo siku mtoto mwenyewe English yake ya ulimbo.....anaunga unga mafaili. Nikaona jamaa mshamba sana huyu.
 
Back
Top Bottom