Karudi Baba Mmoja
Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali,
kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili,
watoto wake wakaja, ili kumtaka hali,
wakataka na kauli, iwafae maishani.
Akatamka mgonjwa, ninaumwa kwelikweli,
hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali,
roho naona yachinjwa, kifo kina nikabili,
kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,
baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
akili zetu nyembamba, hazijajua methali,
kama tunataka mali, tutapataje shambani?
Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,
fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,
kama mnataka mali mtayapata shambani.
Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,
mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,
kama mnataka mali, tutayapata shambani.
Shamba wakapalilia, bila kupata ajali,
mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,
wote wakashangilia, usemi wakakubali,
"KAMA MNATAKA MALI MTAYAPATA SHAMBANI".