SoC02 Mambo muhimu ya kuyafahamu kabla ya kuomba wazo la biashara mtandaoni

Stories of Change - 2022 Competition

JS Farms

Member
Oct 17, 2011
71
131
Nifanye biashara gani? Nipeni wazo la biashara, nina mtaji wa milioni mbili nifanye biashara gani? Naomba wazo la biashara, biashara gani inayolipa?

Haya ni maswali ambayo watu wengi hasa vijana wamekuwa wakiuliza au kuomba ushauri kupitia mitandao ya kijamii.

Kuomba wazo la biashara mtandaoni si jambo baya, ila kama mhusika ataingia kichwa kichwa anaweza kulia kilio cha mbwa mwizi kwa sababu anaweza kupoteza mtaji na hasa ukizingatia hali zetu Watanzania kwa sababu wengi wetu maisha yetu ni ya kuchumia tumbo, yaani tunafanya kazi ili tupate mlo, fedha haziwekeki na hata ukitaka kuweka kuna tozo kila sehemu benki tozo, kwenye simu tozo, ukiweka kwenye kibubu haziwekeki ili mradi tabu na mahangaiko yasiyoisha kila iitwapo leo.

Biashara ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, Juma anaweza kuwa Mwalimu mzuri lakini hawezi kuwa Polisi mzuri, Seif anaweza kuwa Dereva mzuri lakini hawezi kuwa fundi gari mzuri. Biashara nazo zipo hivyohivyo Joseph anaweza kufanya vizuri kwenye biashara ya viazi lakini asiwe mfanyabiashara mzuri wa nguo. Si kila kazi inawezwa kufanywa na mtu yoyote na si kila biashara inawezwa kufanywa na mtu yoyote. Kwahiyo ukipewa wazo la biashara jiulize mara mbili utaiweza? Unaendana nayo? Kwa sababu unaweza ukapewa wazo la kufanya biashara ya nazi lakini hujui nazi zilizokomaa zinakuwaje, unaenda shamba unalipa nazi zikiwa juu ya mnazi zikishuka chini hazijakomaa, ukipeleka sokoni haziuziki, mtaji unapotea mwishowe unapata msongo wa mawazo.

Kwahiyo ukipewa wazo la biashara usiyoifahamu vizuri na ukiona inalipa, tuliza kichwa, fanya utafiti, jifunze kwa wengine wanaofanya na waliofanikiwa, tembelea sehemu ambako bidhaa au malighafi zinatoka, tembelea sokoni na pia tembelea wateja ujue wanataka bidhaa za aina gani.

Imani ya dini nalo ni jambo la kuzingatia, unapopewa wazo la biashara zingatia pia imani yako ya dini(kwa wale wenye kuamini uwepo wa Mungu)kuna biashara kama za kuuza pombe, biashara haram, madanguro, biashara zinazohusisha kukwepa kodi, ushuru na mengineyo.

Inawezekana ukalazimisha kufanya biashara za aina hizo baada ya kupewa mchanganuo kuwa zinalipa na ukashawishika lakini nafsi yako itakusaliti, kufanikiwa katika biashara za aina hiyo itakuwa ndoto kwa sababu hautakuwa na nguvu ya ndani. Kwahiyo biashara za aina hiyo kwa wale wacha Mungu wanatakiwa waziepuke.

Misimamo binafsi nalo ni jambo la kuzingatiwa, kila binadamu anakuwa na msimamo wake, msimamo ni hali ya kufuata kanuni fulani za maisha.

Inawezekana tangu zamani unaamini kuwa uchomaji wa mkaa unaharibu mazingira lakini ukaambiwa kuwa biashara ya mkaa inalipa lakini msimamo wako ni kuwa uchomaji wa mkaa unasababisha uharibifu wa mazingira. Ukijiingiza kwenye biashara za aina hii zinazopingana na msimamo wako hata kama inalipa unaweza usifanikiwe kwa sababu utakosa ari, yaani hali ya kuwa na moyo wa hima katika kukamilisha jambo, moyo wa kutokubali kushindwa.

Mila na utamaduni wa jamii uliyopo nayo inachangia kwa kiasi kikubwa aina ya biashara unayotakiwa kuifanya. Mfano wanawake wa jamii yako hawavai vijora lakini ukaomba ushauri mtandaoni ukaambiwa ufanye biashara ya vijora inalipa na wewe ukanunua ukapeleka kwa wasiovaa vijora hiyo biashara ni lazima ife.

Mfano mwingine wa kuzingatia mila na utamaduni ni kwenye chakula, kuna watu wanoishi kando ya bahari hawali samaki wa maji baridi lakini mtu anaweza kukuambia sehemu fulani samaki wanalipa na wewe ukabeba samaki wako wa maji baridi ukapeleka huko, watakaonunua ni wachache au wasiwepo kabisa. Kwahiyo kwenye kufanya biashara zingatia mila na utamaduni wa sehemu unakotaka kufanyia biashara.

Tabia, mwenendo na matendo ya mtu nayo inachangia kwa kiasi kikubwa kujua aina gani ya biashara unayoweza kuifanya,mfano kuna biashara zinazohitaji mtu awe mtembezi, kuna biashara zinazohitaji mtu awe na uwezo wa kukaa sehemu moja kwa muda mrefu.Kuna biashara kama za kukopesha ambazo hazihitaji mtu mwenye tabia ya upole na mwepesi kusamehe na pia kuna biashara zinazohitaji mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongea/kushawishi.

Kujua mazingira ya sehemu unayotaka kufanya biashara nalo ni jambo la muhimu.Mfano kipindi cha baridi mikoa yenye baridi biashara ya mablanketi, masweta na majaketi ni biashara inayofanya vizuri au kipindi cha mvua biashara za makoti, miamvuli na mabuti ya matope ni biashara inayofanya vizuri lakini kipindi cha baridi au mvua kikiisha na biashara inapungua kwahiyo kujua mazingira na muda sahihi wa kufanya biashara hasa sehemu ambayo huijui ni jambo la muhimu.

Suala lingine muhimu la kuzingatia ni afya yako, mfano unapoambiwa biashara ya kufuga kuku inalipa lakini ni lazima ujue kuwa kuna baadhi ya watu wakiingia tu kwenye banda la kuku wanapata mafua, kuna watu wakiishi sehemu za baridi wanapata matatizo ya kiafya pia kuna biashara nyingine zinahitaji kusafiri mara kwa mara, kutembea umbali mrefu au kwenye milima kwahiyo suala la kujua afya ni jambo la kuzingatia.

Zingatia pia ili ufanikiwe biashara yoyote inahitaji uzoefu na uvumilivu, mtu anaweza kukuambia kuwa biashara fulani inalipa lakini yeye kaifanya kwa miaka minne au zaidi ya hapo keshapata uzoefu mkubwa kavuka milima na mabonde anajua A mpaka Z kuhusu hiyo biashara na anaiona ni rahisi lakini akikupa wazo hakuambii kama inahitaji uzoefu na uvumilivu.

Kwahiyo jambo la msingi ni kuwa mvumilivu kwa sababu ukiwa mvumilivu unapata uzoefu na uvumilivu unapatikana kwa kujifunza, kupita kwenye milima, tambarare na mabonde hivyo vyote ni lazima uvifahamu.

Zingatia kanuni, miiko ya kufanya biashara, pamoja na kwamba utapewa wazo la biashara na ukawa unatafuta uzoefu lakini pia kumbuka kuzingatia kanuni na miiko ya kufanya biashara.

Jambo la mwisho la kufahamu ni utapeli, kwenye mitandao ya kijamii kuna matapeli wa kila aina, unaweza kupewa wazo la biashara na tapeli akakupa maelezo matamu na kumbuka matapeli wana nguvu kubwa ya kushawishi, kabla ya kutoa fedha zako au kutuma kwa mtu yoyote jiridhishe kwa kina.

MWISHO
Nina imani mmejifunza kitu kwahiyo naomba kura zenu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom