Abiria 40 wamenusurika baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda wilayani Malinyi mkoani Morogoro kuteketea kwa moto katika eneo la Maseyu mkoani hapa.
Tukio hilo limetokea leo asubuhi, Desemba 9, 2025, katika kona kali ya Maseyu, Kata ya Gwata ambapo basi hilo aina ya Tata
lilianza kuwaka moto na kuungua lote huku abiria wakifanikiwa kutoka wakiwa salama.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 9.2025 mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Halfan Omary, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, na lilikuwa limepakia abiria 40 ambao wote wameokolewa bila majeraha.
“Hili gari limeteketea kabisa, lakini tunashukuru hakuna abiria aliyejeruhiwa. Hata hivyo, mizigo na mali nyingine za abiria zilizokuwamo ndani zimeungua,” amesema Kamanda Mkama.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya mfumo wa umeme wa gari, ingawa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini undani wa tatizo hilo.
View attachment 3513806View attachment 3513807