Makapuku Forum

Makapuku Forum

Screenshot_20251127_180043_InstaPro%20.jpg
 
Aliyekuwa Diwani mteule wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Shiwinga, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Lusekelo Mwalukomo amefariki dunia baada ya kunywa maji ya betri. Tukio hilo lilitokea jana Novemba 26, 2025 na amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mbozi Mission.

Akithibitisha kifo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega amesema leo Alhamisi Novemba 27, 2025 kuwa sababu za diwani huyo kunywa maji hayo bado hazijajulikana, ingawa taarifa za awali zinahusishwa na msongo wa mawazo.

“Wataalamu wetu wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi. Alikutwa amekunywa maji ya betri saa nne asubuhi. Madaktari walijitahidi kuokoa uhai wake lakini walishindwa,” amesema Mbega.

Mbega amesema anajiandaa kwenda nyumbani kwa familia ya marehemu kwa ajili ya mazungumzo na kupanga taratibu za mazishi kwa kushirikiana na CCM. Kwa sasa, mazishi yanatarajiwa kufanyika Novemba 28, 2025 nyumbani kwake Shiwinga, baada ya kikao cha familia na chama.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga amesema hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya tukio hilo iliyofikishwa polisi.

“Sijaipokea taarifa hiyo. Kwa taratibu, tukio kama hilo lazima liripotiwe polisi ili fomu ya matibabu itolewe. Tunaendelea kufuatilia, tukipata taarifa kamili tutatoa maelezo,” amesema Senga.
Screenshot_20251127_180529_InstaPro%20.jpg
 
Wanajeshi wa Guinea-Bissau wamemuapisha, Jenerali Horta Nta Na Man kuwa kiongozi mpya wa mpito wa nchi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja leo Alhamisi, Novemba 27, 2025, , siku moja baada ya mapinduzi na kukamatwa Rais Umaro Sissoco Embalo wa nchi hiyo, wakati matokeo ya uchaguzi wa kisiasa yalipokuwa yanakaribia kutangazwa.

Jenerali Horta Nta Na Man ameapa katika hafla iliyofanyika makao makuu ya kijeshi huku askari wenye silaha nzito wakihudhuria na kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Jumapili iliyopita, siku moja baada ya wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa rais kutangaza washindi, kundi la maofisa wa kijeshi liliweka wazi kuwa limechukua "udhibiti kamili" wa nchi.

Waliitwa “Kamanda Mkuu wa Kijeshi kwa Urejeshaji wa Amri” na kupitia televisheni walitangaza kusimamishwa mara moja kwa mchakato wa uchaguzi “hadi itakapotangazwa vinginevyo”.

Rais Embalo aliondolewa madarakani katika kipindi kingine cha machafuko katika nchi inayokumbwa na mapinduzi mara kwa mara. Matokeo ya muda yalitarajiwa kutangazwa kati yake na Fernando Dias, mpinzani wake mpya kisiasa.

Jumapili, mji mkuu Bissau ulikuwa kimya, huku wanajeshi wakiimarisha usalama barabara na wakazi wengi wakiendelea kubaki ndani ya nyumba zao licha ya kuondolewa kwa marufuku ya kuondoka usiku.

Hayo yalijiri wakati biashara na benki zilikuwa zimefungwa
Screenshot_20251127_180650_InstaPro%20.jpg
 
Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ametangaza hali ya dharura ya usalama wa kitaifa kufuatia ongezeko kubwa la mashambulizi ya mauaji na utekaji nyara katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo.

Katika agizo kali lililotolewa jana Jumatano, Novemba 26, 2025, Tinubu ameagiza kuongeza kwa dharura idadi ya vikosi vya usalama na kuchukua hatua thabiti dhidi ya kile alichokiita ‘mawakala wa uovu’ wanaodhoofisha taifa.

Kwa mujibu wa agizo hilo, Jeshi la Polisi la Nigeria limeelekezwa kuongeza maofisa 20,000 zaidi, na kufanya jumla ya idadi inayopangwa kufikia 50,000.

Aidha, Rais ameidhinisha kambi za National Youth Service Corps (NYSC), kutumika kama vituo vya muda vya mafunzo ili kuharakisha kupelekwa kwa askari hao katika maeneo yenye changamoto za kiusalama.

Vilevile, ameagiza maofisa wa polisi waliokuwa wakitumika katika ulinzi wa watu mashuhuri warudishwe kazini na kupatiwa mafunzo ya dharura kabla ya kupelekwa katika maeneo hatarishi.

“Idara ya Huduma za Jimbo imepewa mamlaka ya kupeleka mara moja walinzi wote wa misitu waliohitimu mafunzo, ili kukabiliana na magaidi na majambazi wanaojificha msituni, na kuajiri wengine zaidi kwa ajili ya ulinzi.

Hakutakuwa na mahali pa kujificha tena kwa mawakala wa uovu,” amesema Tinubu.

Ameongeza kuwa operesheni za kuwaokoa wanafunzi waliotekwa kutoka Shule ya Katoliki ya St. Mary katika Jimbo la Niger, pamoja na raia wengine waliotekwa nchini humo, zitaendelea bila kukoma.

Katika hatua nyingine, Rais Tinubu amelihimiza Bunge la Nigeria kuanza mchakato wa kupitia sheria ili kuruhusu majimbo yanayotaka kuanzisha jeshi la polisi la kikanda (state police), kufanya hivyo kisheria hoja ambayo imekuwa ikijadiliwa kwa miaka mingi kutokana na kuzorota kwa usalama wa ndani.

Aidha, ametoa onyo kwa serikali za mitaa dhidi ya kuanzisha shule za bweni katika maeneo yaliyotengwa bila ulinzi madhubuti. Amelihimiza pia makanisa na misikiti katika maeneo hatarishi kuimarisha uratibu wa kiusalama ili kulinda jamii zao.
Screenshot_20251127_180832_InstaPro%20.jpg
 
Mahakama nchini Peru imemhukumu Rais wa zamani wa nchi hiyo, Martin Vizcarra, kifungo cha miaka 14 gerezani baada ya kumpata na hatia ya kupokea hongo miaka kadhaa kabla hajaingia madarakani, hatua inayoongeza idadi ya viongozi wa juu nchini humo waliowahi kufungwa kwa makosa ya ufisadi.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Vizcarra alipokea hongo yenye thamani ya takribani dola 676,000 kutoka kwa kampuni za ujenzi, kama malipo ya kuwapatia zabuni za miradi ya umma alipokuwa Gavana wa Moquegua kati ya mwaka 2011 na 2014.

Vizcarra, ambaye amekuwa akikabiliwa na kesi hiyo tangu Oktoba mwaka jana, alikanusha mashtaka akisisitiza kuwa ni mwathirika wa mateso ya kisiasa.

Vizcarra alishika wadhifa wa kuiongoza Peru mwaka 2018 kufuatia kujiuzulu kwa mtangulizi wake, lakini aliondolewa na Bunge mwaka 2020 wakati uchunguzi wa ufisadi ukipamba moto.

Baada ya hukumu kutolewa, Vizcarra ameandika kwenye mtandao wa X akisema: “Hii si haki, ni kulipiza kisasi. Lakini hawatanimaliza.”

Timu yake ya wanasheria imethibitisha kuwa tayari imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo, ambao pia unamzuia kushikilia nafasi yoyote ya umma kwa kipindi cha miaka tisa.

Wakati huohuo, kaka yake mkubwa, Mario Vizcarra, anapanga kugombea urais katika uchaguzi wa Aprili 2026 kupitia chama cha Peru First, ambacho Martin Vizcarra aliwahi kukihudumia kama mshauri mkuu.

Hukumu hiyo imezidi kuibua mjadala mpana nchini Peru kuhusu mustakabali wa kisiasa na vita dhidi ya ufisadi miongoni mwa viongozi wa juu.
Screenshot_20251127_180935_InstaPro%20.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom