Usiniite Mfalme, Niite Daudi (Kisa cha Daudi na Mke wa Uria)-2
Tulipoishia.. Bethsheba Mke wa Uria anampa taarifa kwamba mwezi huu hajaona siku zake...!
Endelea...
“Usihofu mama, mimi ndie Mfalme wa Israel na vyote vilivyomo hakuna mtu yoyote aliyeko juu yangu. Kama niliweza kumuuwa Goliath kwa mkono wangu, sina wa kumuogopa” Daudi alisema huku anamvuta Bethsheba kifuani kwake.
“Sawa Daudi, nakuamini mpenzi” Bethsheba aliyaongea kwa sauti ya chini kama ananong'ona
Mapenzi yalimnogea Daudi kuliko Israel yenyewe. Daudi alikuwa hasikii lolote kwa penzi tamu la mke wa mtu. Alikuwa hakumbuki tena zile amri za Musa. Wala haikuimbuki ile amri inayokataza kuzini wala ile inayokataza kumtamani mke mtu.
Bethsheba pia alikuwa amenogewa na penzi la Mfalme. Ni mwanamke gani asiye utamani Umalikia. Ni nani? Ndivyo ilivyokuwa kwa mke wa Uria.
Usiku baada ya mke wa Uria kuondoka. Daudi alikwenda kulala. Alishtuka kutoka usingizini huku mapigo ya moyo yakienda mbio. Aliamka na kukaa kitandani huku anageuka geuka
kwa hofu kubwa. Ndoto ndio iliyo muogopesha.
Daudi aliota kuwa alikuwa porini anawinda. Ghafla Simba akatokea akaupiga mkuki wake ukadondoka chini, Daudi akakimbia lakini Simba akayavuta mavazi yake. Mavazi ya kifalme yakamvuka. Daudi akabaki uchi.
Daudi hakujua maana ya hii ndoto. Lakini akahisi ina uhusiano na kitendo chake cha kulala na mke wa mtu.
Daudi akaamka, akamuita mpambe wake.
“Hakikisha barua hii inamfikia Yoabu kabla jua halijachomoza” Daudi alimwambia yule mpambe huku anamkabidhi barua
Yoabu ndie alikuwa kamanda wa kile kikosi cha maaskari hodari wa Daudi. Wakati huu alikuwa vitani tena vita ilikuwa imepamba moto.
Saa tatu asubuhi ujumbe ule ulimfikia Yoabu. Yoabu aliusoma. Ulikuwa ujumbe mfupi sana kuliko ujumbe wowote aliowahi kuupokea kutoka kwa Mfalme Daudi.
Ujumbe ulisomeka hivi:
“KABLA JUA HALIJAZAMA, URIA MHITI AWE AMEFIKA KWENYE MAKAZI YANGU”
Yoabu alimwita Uria na kumwambia “Uria unaitwa na Mfalme haraka sana”
Uria aliondoka kurudi Jerusalem huku akiwa na kikundi kingine cha watu kumi wa kumlinda. Yoabu asingeweza kumuacha aende mwenyewe. Asingefika je. Hasira ya Mfalme Daudi angeibabaje.
Itaendelea...