Ripoti ya pili ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 imebaini mambo nane.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege, Redemptus Bugomola amesema ripoti ya kwanza walikwenda na kushuhudia eneo la tukio na kuona ndege ilivyoumia, “na hii ya pili, tumekwenda mbele zaidi kwa kuangalia vinasa sauti.”
Mambo hayo nane ni;
1. Ndege ilikuwa imeandikishwa kihalali.
2. Marubani wa ndege hiyo hawakuwa na tatizo la kiafya.
3. Hali ya hewa katika uwanja wa ndege wa Bukoba haikuwa nzuri.
4. Hali mbaya ya hewa iliathiri marubani kutekeleza jukumu lao.
5. Marubani hawakutilia maanani ishara za tahadhari zilizotolewa.
6. Ndege iligonga kwanza bawa lake la kushoto wakati ikianguka.
7. Pia, ilianguka kwa kasi na kugonga sehemu ya mbele kwenye kina cha maji ya ziwa.
8. Vifaa vyote vya kuongezea ndege vilikuwa vinafanyakazi kwa kuzingatia matakwa ya rubani.
Ripoti ya awali ya ajali hiyo ilitoka Novemba 23, 2022 ilichambua mambo mbalimbali ya kitaalamu yaliyotokea wakati wa ajali hiyo.