Wizara ya Afya imetoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa Covid-19 nchini katika kipindi cha kuanzia tarehe 05 Mei hadi 03 Juni 2022 ambapo kipindi hicho, jumla ya maambukizi mapya 161 yamethibitika ikilinganishwa na maambukizi 68 kwa kipindi cha tarehe 02 Aprili hadi 4 Mei 2022.
Ongezeko hili ni sawa na asilimia 137, Aidha, katika kipindi cha miezi miwili mfululizo hakuna kifo kilichoripotiwa, halii hii inaashiria kuwa maambukizi yameanza kuongezeka katika jamii.
"Mchanganuo wa idadi ya waliothibitika katika kipindi cha tarehe 05 Mei hadi 03 Juni 2022 inaonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam uliripoti maambukizi 130, Arusha (10), Mwanza (5), Shinyanga (4), Mtwara (3), Dodoma (2), Mara (2), Morogoro (1), Simiyu (1), Katavi (1), Kilimanjaro (1) na Mbeya (1), jumla ya wagonjwa watatu (3) waliothibitika kuwa na Covid-19 walilazwa na wote walikuwa hawajapata chanjo"
"Kwa takwimu hizi, inaonyesha kuwa, chanjo ni kinga dhidi ya madhara ya Covid - 19, Serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo nchini ili kuwezesha wananchi kupata kinga dhidi ya ugonjwa huu"
"Kuanzia tarehe 05 Mei hadi 03 Juni 2022 jumla ya wananchi waliopata dozi kamili ya chanjo ya Covid 19 ni 775,680, Wizara inaendelea kuwasisitiza wananchi kupata na kukamilisha dozi za chanjo ili kuzuia kupata ugonjwa mkali hata kifo pale Mtu anapopata maambukizi" Mganga Mkuu wa Serikali Dr. Aifello Sichwale