Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mtendaji wa PAP, Harbinder Seth, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wamepitia barua iliyoandikwa na mshtakiwa huyo na kufikia makubaliano kwa kile alichokiomba.
Seth aliandika barua hiyo Juni 10, kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akiomba kukiri mashtaka yake na kupunguziwa adhabu.
Barua hiyo ilijadiliwa kwa siku mbili na upande wa mashtaka na ule wa utetezi na kisha kutolewa mrejesho.
Wakili wa Serikali Mkuu, Marterus Marandu akisaidiana na Ladslaus Komanya jana alitoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili Marandu alitoa maelezo hayo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kuwasilisha mrejesho wa kile walichozungumza kati yao na Seth kwa ajili ya kuimaliza kesi hiyo.
“Kesi imekuja kwa ajili ya kutoa mrejesho wa barua iliyoandikwa na mshtakiwa huyu (Seth), niseme barua tumeshazipitia kwa pamoja na tumefikia mahali pa kukubaliana kuhusu kile ambacho mshtakiwa alikuwa anakiomba na baada ya hapo, tumekubaliana kuendelea na shauri hili,” alidai wakili Marandu.