Mwanamke mmoja amefariki dunia baada ya mlinzi wa zamani wa hospitali kujifanya daktari na kumfanyia upasuaji, polisi wamesema leo Jumatatu.
Shameema Begum, akiwa na miaka 80, alifariki Jumapili, wiki mbili baada ya Muhammad Waheed Butt kujaribu kumtibu jeraha lililokuwa mgongoni katika hospitali ya serikali iliyopo jijini Lahore, mashariki mwa Pakistan.
"Hatuwezi kujua kila daktari na kila mtu anachofanya wakati wote. Ni hospitali kubwa," alisema ofisa utawala wa hospitali hiyo ya Mayo iliyoko Lahore na ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Alisema haikueleweka ni upasuaji wa aina gani ambao mlinzi huyo alimfanyia mgonjwa ndani ya chumba cha operesheni, ambako wataalamu waliofuzu taaluma ya udaktari walikuwepo.
Hospitali za serikali za Pakistan, ambako wagonjwa hutakiwa kulipa kiasi cha fedha kwa ajili ya matibabu, mara kadhaa zinaweza kukosa ufanisi na kuwa na matatizo.
Familia ya Begum ilimlipa Butt kwa ajili ya upasuaji huo, na alitembelea nyumbani mara mbili zaidi kufunga jeraha la mwanamke huyo.
Lakini wakati damu ilipovuja kwa wingi na maumivu kuzidi, familia yake ilimrudisha hospitalini, ambako waligundua kilichotokea.
Mwili wake unahifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi kujua kama kifo chake kilisababishwa na matatizo yaliyotokana na upasuaji huo.
"Mlinzi ameshtakiwa na yuko mahabusu polisi," alisema msemaji wa polisi wa Lahore, Ali Safdar alipoongea na AFP.
"Butt alijifanya daktari na zamani alitembelea nyumbani kwa wagonjwa wengine."