Makapuku Forum

Makapuku Forum

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 34
ILIPOISHIA:
Alipofikisha tatu, nilifumba macho, nikashtukia ghafla tumehama pale tulipokuwa na kwenda upande wa pili, kule barabarani ambako watu wengi walikuwa wamesimama wakishangaa, tukajichanganya na wale watu.
“Hebu angalia wanachokishangaa,” alisema huku akinitaka nitazame pale tulipokuwa tumekaa awali. Macho yalinitoka nikiwa ni kama siamini.
SASA ENDELEA...

Watu wawili, mmoja akionesha kuwa mwanamke na mwingine mwanaume, wakiwa watupu kabisa huku miili yao iking’aa sana, walikuwa wamekaa kwenye msingi wa nyumba, wakiwa wanazungumza. Macho ya kila mmoja yalikuwa yaking’aa sana na nyuso zao zilikuwa na gizagiza fulani ambalo lilifanya iwe vigumu kwa watu kuwatambua sura zao.
“Hivi ndivyo tulivyokuwa tukionekana ndiyo maana unaona hawa watu wote wamekusanyika hapa,” alisema Isri huku akiniegamia.
Nilibaki nimepigwa na butwaa huku nikiwatazama wale watu ambao wala hawakuwa na taarifa kwamba tulikuwa tumeshajichanganya nao. Nilitamani kumuuliza Isri kwamba sasa iweje wale watu wawe wanaendelea kutuona wakati tulishahama na kujichanganya nao? Kabla hata sijamjibu, ni kama alizisoma hisia zangu, akaniambia kile walichokuwa wakiendelea kukiona, ilikuwa ni kiini macho.
Akaniambia kwamba watu wengi hawajui lakini hakuna jambo la hatari kama kusimama usiku na kuanza kutazama vitu usivyovijua au visivyo vya kawaida kwa sababu kama ni watu wenye nia ovu, unapowatazama tu wanajua kwamba unawatazama na wanao uwezo wa kubadilisha kile unachokiona wewe na kukuonesha kitu cha tofauti kabisa.
Akaniambia ndiyo maana baadhi ya watu hupata matatizo makubwa sana baada ya kuona majini usiku, wengine huona watu warefu wenye kwato, wengine huona miti ikibadilika au huona viumbe vya ajabu wakati kiukweli ni kwamba wanakuwa wamewaona wachawi wakiwa kwenye maumbo yao ya kawaida lakini kwa kuwa wachawi nao wanakuwa wameshagundua kwamba wanatazamwa, wanawafanyia kusudi.
“Sijaelewa, kwa hiyo unamaanisha hata mimi na wewe ni wachawi?”
“Sijamaanisha hivyo.”
“Kwani wewe ulijua kwamba wanatutazama?”
“Ndiyo nilijua,” alinijibu Isri na kunifanya nipigwe na mshangao mkubwa. Watu walikuwa wakizidi kuongezeka na wengi walikuwa ni walinzi wa maeneo ya jirani na pale, wengine wakiwa ni Wamasai na wengine wakiwa ni wafanyabiashara wanaodamka alfajiri na mapema kuwahi kuchukua bidhaa zao.
“Sasa mbona wanazidi kuongezeka, itakuwaje? Ina maana hapa hawatusikii wala hawatuoni?” nilimuuliza, akatingisha kichwa kuonesha kukubali, akaniambia ipo namna ya kuwatawanya. Aliposema hivyo tu, mara nilishangaa wale watu ambao watu wote walikuwa wakiwatazama, wakibadilika na kuwa mbwa wawili wakubwa, dume na jike.
Wakaanza kubweka kwa hasira na kuanza kutimua mbio kulifuata lile kundi la watu. Kiukweli kwa jinsi mbwa hao walivyokuwa wakubwa, wenye hasira huku meno yao makali yakiwa yametoka nje, hata mimi mwenyewe nilijikuta nikiogopa mno. Kufumba na kufumbua, kundi lote lilianza kutimua mbio, kila mmoja kivyake.
Na mimi nilitaka kukimbia lakini Isri alinikamata mkono kwa nguvu, wale mbwa wakawa wanazidi kuja kwa kasi, ikabidi nisimame nyuma yake. Watu walizidi kutimua mbio huku wakipiga kelele na ghafla tukasikia breki kali za gari zikifuatiwa na kishindo kikubwa.
“Tayari!” alisema Isri lakini sikumtilia maanani, akili zangu zote zikawa kwa wale mbwa. Cha ajabu, japokuwa sisi tulikuwa tumesimama, walitupita kwa kasi kubwa na kuendelea kuwatimua wale watu.
“Tayari huko,” alisema Isri kwa mara nyingine, ikabidi nimuulize tayari nini? Akaniambia twende tukajionee wenyewe. Yeye alitangulia, mimi nikawa namfuata, tukanyoosha na ile barabara ya lami mpaka mahali palipokuwa na njia panda, akanionesha kwa kidole nitazame mwenyewe.
Gari dogo aina ya Toyota Carina lilikuwa limeacha njia na kugonga kingo za daraja na kuingia mtaroni, huku barabarani kukiwa na mtu amelala huku damu nyingi zikimtoka akionekana amegongwa na gari lile.
“Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko, akaniambia mtu huyo alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa pale wakitushangaa na wakati akiwakimbia wale mbwa ndipo akaingia barabarani bila kutazama, hali iliyosababisha agongwe na gari hilo kisha na lenyewe likapoteza mwelekeo na kugonga kingo za barabara.
Yaani kwa jinsi Isri alivyokuwa akizungumza kirahisirahisi, ungeweza kudhani anasimulia stori au anazungumza masihara, alikuwa anarahisisha sana mambo hali ambayo ilinifanya nigeuke na kumtazama usoni.
Nilishtuka sana nilipomtazama usoni, macho yake yalikuwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu sana na kung’aa huku kwenye kingo za mdomo wake kukiwa kama na michuruziko ya damu, meno makali kama ya wale mbwa yakiwa yametokea kila upande.
Mshtuko nilioupata ulikuwa hauelezeki, nikahisi na mimi nipo kwenye mtego mbaya wa kifo, sikusubiri chochote, nilikurupuka na kuanza kutimua mbio kwa kasi kubwa nikiwa hata sielewi naelekea wapi.
“Togo! Togo rudi nakwambia, ohooo!” alisema kwa sauti kali ya kutisha lakini wala sikuvijali vitisho vyake. Jambo ambalo najisifia, ni uwezo mkubwa wa kutimua mbio. Unajua maisha ya kule kijijini tuliyokulia, ilikuwa ni lazima tu ujifunze kukimbia kwa kasi kubwa, kwani kinyume na hapo usingeweza kuambulia chochote mnapoenda kuwinda wanyama wa porini.
Nilikimbia kisawasawa, dakika chache baadaye nikawa nimeshafika mbali kabisa, nikatokezea kwenye barabara kubwa ya lami ambayo japokuwa ilikuwa ni usiku, yenyewe ilikuwa na magari mengi yakiendelea kupita, hasa makubwa ya mizigo.
Kiukweli nilikuwa mgeni kabisa na jiji lakini niliona ni bora nipotee kuliko kuendelea kukaa karibu na Isri. Japokuwa alikuwa amenieleza mambo mengi kuhusu yeye, yale mambo aliyoyafanya dakika za mwisho, ikiwemo kuwabadilisha wale watu kuwa mbwa, jinsi alivyokuwa akichekelea ile ajali iliyosababisha maafa makubwa na jinsi alivyobadilika na kuwa kama mnyama mkali wa porini, yalinifanya nimuogope mno.
Nikawa naendelea kukimbia pembezoni mwa barabara nikiwa hata sijui naelekea wapi. Kwa mbali kulianza kupambazuka, nikaanza kuona watu wachache wakifanya mazoezi ya kukimbia pembeni ya barabara.
Niliamini hao ndiyo wanaoweza kunisaidia uelekeo wa kufika nyumbani kabla hakujapambazuka kabisa.
Cha ajabu, kila nilipokuwa nikimkaribia mtu yeyote anayefanya mazoezi, alikuwa akitimua mbio za ajabu kunikwepa, mwingine almanusra agongwe na gari kwani alikuwa akija kwa mbele, na mimi nikawa nakimbia taratibu huku nikionesha dalili za kutaka kusimama ili nimuulize lakini ghafla aliponiona, alipiga kelele na kuvuka barabara kwa kasi kubwa mpaka upande wa pili bila hata kutazama, lori kubwa likapiga honi kali na dereva akakata kona kali kumkwepa.
Ilibidi nisimame na kujitazama mwilini kwa nini watu wananikimbia. Jambo la kwanza ambalo lilinishtua, kumbe kwa muda wote huo nilikuwa nikikimbia kwa kutumia mikono na miguu, hata sijui kwa nini muda wote huo sikujishtukia, harakaharaka nikainuka na kusimama kwa kutumia miguu.
Nilipojitazama mwilini, nilishtuka mno kugundua kwamba kumbe nilikuwa na manyoya mengi kama mnyama wa porini, nilipojitazama mikono, nilizidi kupagawa baada ya kugundua kuwa kumbe mikono yangu ilikuwa imebadilika na kuwa kama ya mbwa.
Mara nilishtukia jiwe kubwa likirushwa na kunikosakosa, kabla sijatulia nikashtukia jiwe lingine likinikosakosa, nikaona naweza kuuawa bure, nikaanza kutimua mbio lakini nilipojaribu kukimbia kwa miguu nilijikuta nikishindwa, ikabidi nijaribu kutumia na mikono, nikaweza na kasi ilikuwa kubwa zaidi. Nilikimbia sana huku nikilia nikiwa sielewi nini itakuwa hatma yangu.
Ni hapo nilipogundua kwamba kumbe Isri alikuwa amenigeuza umbo langu na kuwa kama mbwa mkubwa, nilimlaani sana moyoni mwangu na kujikuta nikiyakumbuka maneno ya baba ambaye mara kwa mara alikuwa akinionya kuhusu msichana huyo.
Nikiwa naendelea kukimbia, nilishtukia mtu mmoja akija kwa kasi kubwa nyuma yangu, nikazidi kuongeza kasi lakini kabla sijafika mbali nilishtukia kamba nene ilipita shingoni mwangu na kunifunga kitanzi, nikadondoka chini kama mzigo.
Nikiwa bado hata sijui nini cha kufanya, nilishtukia nikifungwa mikono na miguu, nikajaribu kukurupuka lakini sikuweza kufanya chochote, ikabidi nitulie na kuanza kumtazama ni nani aliyenifanyia kitendo hicho na alikuwa na lengo gani kwangu maana niliona kifo changu kikiwa kimewadia. Na hata kama ningeuawa, kila mtu angeamini aliyekufa ni mbwa mkubwa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 35
ILIPOISHIA:
NIKIWA bado hata sijui nini cha kufanya, nilishtukia nikifungwa mikono na miguu, nikajaribu kukurupuka lakini sikuweza kufanya chochote, ikabidi nitulie na kuanza kumtazama ni nani aliyenifanyia kitendo hicho na alikuwa na lengo gani kwangu maana niliona kifo changu kikiwa kimewadia. Na hata kama ningeuawa, kila mtu angeamini aliyekufa ni mbwa mkubwa.
SASA ENDELEA...

“MIMI sipendi mtu mkaidi, siku nyingine nitakuacha uwe mbwa koko, unafikiri unaweza kunikimbia mimi?” alikuwa ni Isri, akiwa anahema huku jasho likimvuja kwa wingi. Nilitaka nimuombe msamaha lakini sauti haikutoka, nikawa naendelea kutokwa na machozi kwa wingi.
Aliniinamia pale chini, akanionyesha ishara nifumbue mdomo, nikafanya hivyo, akaingiza mkono mfukoni na kutoa kichupa kilichokuwa na maji, akayamimina yote mdomoni mwangu. Yalikuwa machungu sana lakini nilivumilia, akanionyesha ishara kwamba niyameze.
Nilifanya hivyo, nikahisi kama mwili wangu wote unawaka moto kwa maumivu lakini kufumba na kufumbua, nilijikuta nikibadilika na kurudi kwenye hali yangu ya kawaida. Alinifungua ile kamba ya shingoni kisha mikononi na miguuni, akaniambia nisimame lakini nilishindwa kufanya hivyo kwani sikuwa na nguo hata moja mwilini, akafungua kimfuko alichobeba mgongoni na kunirushia nguo zangu.
Yaani kama kuna mtu anabisha uchawi haupo kwenye hii dunia, basi anajidanganya sana, kuna uchawi na wachawi na wengine wana uwezo mkubwa kuliko unavyoweza kufikiri. Sijui hata hizo nguo nilizivua saa ngapi na yeye alizipata wapi, sikutaka kuhoji, harakaharaka nilizivaa huku nikitazama huku na kule kama hakuna mtu yeyote anayetuona.
Bado mwili wangu ulikuwa na harufu ya mbwa-mbwa na mikono ilikuwa imechubuka nadhani ni kwa sababu ya kukimbia kama mbwa.
“Kwa nini unanifanyia hivi Isri? Kosa langu ni nini?”
“Sasa kwani mimi nimekufanyaje? Badala unishukuru unaanza kunilaumu tena.”
“Nikushukuru! Nikushukuru kwa lipi,” nilisema kwa hasira huku nikimsogelea Isri mwilini, mwili wangu ukitetemeka kwa jazba.
“Unataka kufanya nini Togo!”
“Nataka unieleze, kwa nini umenifanyia hivi? Unanijua au unanisikia?” niliwaka kwa jazba. Miongoni mwa vitu ambavyo nilikuwa najivunia na hata wenzangu kule kijijini walikuwa wakiniogopa, ni ubavu niliokuwa nao. Hakukuwahi kutokea ugomvi wowote wa kupigana halafu nikashindwa ingawa ilikuwa si rahisi kunikuta nikipigana mpaka mtu anichokoze sana.
“Mimi ni nani kwako?” Isri aliniuliza swali ambalo kidogo lilizifanya jazba zangu zitulie. Aliniuliza swali hilo kwa mara nyingine, halafu akaniuliza kama naamini yeye anaweza kunifanyia jambo baya kwa makusudi kwa jinsi alivyokuwa ananipenda mpaka kufikia hatua ya kunipa mwili wake wa thamani. Akaniuliza kama nimesahau mapenzi makubwa aliyonionyesha tangu siku ya kwanza ananiona, nikajikuta nikishusha pumzi ndefu na kujiinamia, mwili ukianza kupunguza kutetemeka.
“Twende huku,” alisema huku akinishika mkono, nilitaka kujichomoa lakini moyo ukasita, nikawa mpole kama kondoo anayepelekwa machinjioni, nikamfuata mpaka chini ya mwembe mkubwa uliokuwa jirani na pale tulipokuwa. Akaniambia nimpe mkono wangu wa kushoto, akaugeuza na kuutazama kwa muda kwenye upande wa nyuma wenye kucha.
“Unauona huu mshipa wa damu,” aliniambia huku akinionyeshea mshipa mkubwa wa damu uliokuwa unaonekana. Akaniambia kwamba nikifika nyumbani, kabla sijaingia ndani, natakiwa kuchukua kitu chenye ncha kali, iwe sindano au wembe na kujitoboa kwenye huo mshipa ili damu itoke.
“Damu ikiwa inatoka, hakikisha unaipakaza kwenye kingo mbili za mlango kisha ndiyo uingie ndani na usitoke mpaka giza liingie,” aliniambia huku akinipa pole kwa yote yaliyotokea, sikumjibu kitu kwani bado sikuwa najua nini itakuwa hatma yangu.
Baada ya hapo, aliniambia nifumbe macho, nikatii alichokisema, akaniambia nisifumbue mpaka atakaponiambia. Ghafla nikaanza kuhisi kama kimbunga kikali kinavuma pale chini ya mwembe tulipokuwa, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka niliposikia sauti za watu ninaowafahamu wakilitaja jina langu, akiwemo Isri mwenyewe.
Ikawa ni kama nimetoka kwenye usingizi mzito ambao hata sielewi ulitokea wapi, nilipofumbua macho, nilishtuka mno kujikuta nipo nje ya nyumba ya akina Rahma huku mama na ndugu zangu wakiwa wamenizunguka lakin Isri hakuwepo. Yaani kuna mambo mengine yanatokea hata ukiulizwa yametokeaje, huwezi kuelezea.
“Vipi? Mbona umelala nje?” mama aliniuliza huku akiniinua. Sikutaka kuwa na maelezo marefu maana kila mtu angeniona mwendawazimu kama ningesimulia kila kitu kilichotokea. Kwa bahati nzuri, baba alitoka na kuja hadi pale nilipokuwa, nikiwa bado nimekaa chini kwenye maua.
Akanitazama usoni kwa makini kisha akawaambia ndugu zangu pamoja na mama wakaendelee na usafi kwa sababu ndiyo kwanza walikuwa wametoka kuamka na walikuwa wakifanya usafi wa mazingira na nyumba.
Waliondoka kwa shingo upande, mara kwa mara wakawa wanageuka na kunitazama, wakiwa na maswali mengi yasiyo na majibu. Walichokuwa wanakijua wao ni kwamba nilikuwa nimekamatwa na polisi na kwa jinsi taratibu za kisheria zilivyo, isingekuwa rahisi mimi kutoka bila kuja kuwekewa dhamana na hakukuwa na mtu mwingine wa kufanya hivyo zaidi ya baba na baba yake Rahma.
“Hebu simama,” alisema baba huku akinipa mkono, na mimi nikampa mkono wa kushoto. Wakati akinivuta kuniinua, nilimuona akiukazia macho mshipa wangu wa mkononi, uleule ambao Isri aliniambia nikifika nyumbani, kabla sijaingia ndani niutoboe kisha damu nizipake kwenye kingo za mlango.
“Umefanya nini? Hebu tuone?” alisema baba huku akizidi kuuvutia ule mkono wangu kwake, akautazama ule mshipa kwa sekunde kadhaa kisha nikamuona akiingiza mkono wake mmoja mfukoni, akatoa pochi yake na kuipekuakwa mkono mmoja, huku ule mwingine akiwa bado amenishikilia.
Nikamuona akitoa sindano ya kushonea nguo iliyokuwa na uzi mweusi, nikiwa bado najiuliza anataka kufanya nini, nilishtukia akinitoboa, nikaruka kwa maumivu, damu nyingi ikawa inaruka kwa kasi. Harakaharaka, akiwa bado amenishikilia, nilimuona baba akitoa kichupa kidogo mfukoni, cha ajabu eti akawa anakinga damu ambayo licha ya kutobolewa sehemu ndogo, ilikuwa ikiendelea kuruka kwa nguvu.
Sikuelewa kulikuwa na uhusiano gani kati ya ule mshipa wangu, damu iliyokuwa inanitoka na kile alichokisema Isri. Kile kichupa kidogo kilikaribia kujaa lakini cha ajabu, damu yenyewe ilikuwa nyeusi tii. Ilipopungua kutoka, baba aliniachia, akakifunga kile kikopo na bila kunisemesha kitu aliingia ndani haraka na kuniacha palepale nje.
Ndugu zangu waliokuwa wakiendelea kunitazama kwa macho ya kuibia, walibaki kunishangaa tu. Kwa kuwa baba hakuniambia chochote, na tayari Isri alikuwa amenipa maelezo fulani, nilijifuta ile damu iliyokuwa ikiendelea kunivuja, safari hii ikiwa imepungua, harakaharaka nikasogea mlangoni na kuipaka kwenye kingo za mlango, nikawa nageuka huku na kule kuhakikisha hakuna anayeona ninachokifanya.
Nilipofanya kitendo hicho tu, nilisikia kama masikio yamezibuka hivi, nikawa nasikia sauti za ajabuajabu kama miluzi hivi ambayo awali sikuwa naisikia, nikajikuta nikilazimika kuziba masikio kwa mikono, nikaingia ndani.
Cha ajabu, nilipoingia ndani tu, ile miluzi ilikoma kusikika, nikarudi kwenye hali yangu ya kawaida ingawa bado damu ilikuwa ikinitoka kidogo.
“Togoooo!” Rahma ambaye ndiyo kwanza alikuwa akitoka chumbani kwake baada ya kuamka, alisema huku akinikimbilia pale koridoni nilipokuwepo, akaja na kunikumbatia kwa nguvu huku akipiga kelele, akasema eti haamini kama ameniona.
“Mbona unatoka damu?”
“Nimeumia,” nilimjibu kwa mkato, akanipa pole sana na kunishika mkono, akawa ananipeleka kule chumbani kwake. Mwili wangu ulikuwa mchafu na nilikuwa nanuka lakini mwenyewe hakujali. Furaha aliyokuwa nayo, iliweza kabisa kuumaliza uchovu wa asubuhi aliokuwa nao, uso wake ukachangamka mno, akawa anatembea kwa madaha huku akijinyonganyonga.
Kabla ya kupatwa na yale matatizo siku iliyopita, hatukuwa tumeonana na Rahma kwa sababu asubuhi aliwahi sana kuamka na kuondoka na mama yake kufuatilia mambo ya chuo, hatukupata muda wa kuwa pamoja.
“Togoo!” nilisikia baba akiniita kwa sauti ya juu akiwa amesimama kwenye mlango wa chumba anacholala na mama.
“Naam baba,” niliitikia huku nikijaribu kumtoa Rahma maana alikuwa amenishika kimahaba, baba akaja mbiombio na kunishika mkono, akamwambia Rahma kuna kazi hatujamaliza kwa hiyo anisubiri, alinishika mkono na kuanza kunivuta kuelekea nje lakini tulipofika kwenye kingo za mlango tu, jambo la ajabu lilitokea.
Je, nini kitafuatia?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom