Makapuku Forum

Makapuku Forum

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 36
ILIPOISHIA:
“Naam baba,” niliitikia huku nikijaribu kumtoa Rahma maana alikuwa amenishika kimahaba, baba akaja mbiombio na kunishika mkono, akamwambia Rahma kuna kazi hatujamaliza kwa hiyo anisubiri, alinishika mkono na kuanza kunivuta kuelekea nje lakini tulipofika kwenye kingo za mlango tu, jambo la ajabu lilitokea.
SASA ENDELEA...

Kishindo kikubwa kilisikika, nikamuona baba akianza kuyumbayumba kama amelewa, na mimi nikaanza kusikia kizunguzungu kikali huku damu zikianza kututoka wote, mdomoni na puani. Muda huo tulikuwa tumeshavuka kizingiti cha mlango.
Sijui nilipata wapi ujasiri kwani ni muda huo ndipo nilipogundua kwamba kuna kosa nilikuwa nimelifanya, Isri aliniambia kwamba nisitoke nje mpaka giza litakapoingia, jambo ambalo nililikiuka kwa hiyo ili kurekebisha makosa, nilimvuta baba kwa nguvu, wote tukaangukia upande wa ndani wa mlango.
Kilisikika kishindo kingine kisha baba akawa ni kama amezinduka kutoka kwenye usingizi mzito.
“Nini kimetokea?” baba aliniuliza huku na yeye akiwa ni kama amepigwa na butwaa, akainua shingo na kutazama huku na kule, nikamuona akishtuka zaidi baada ya kuona damu zinamtoka mdomoni na puani pale chini.
“Hata mimi sijui,” nilimjibu huku nikisimama, na yeye akasimama kisha akawa anajifuta damu huku akitazama vizuri pale mlangoni. Aliangalia kwa sekunde kadhaa kisha akanigeukia na kunitolea macho ya ukali.
“Umeweka nini hapa?” aliniuliza kwa ukali.
“Hakuna kitu.”
“Una uhakika?” aliniuliza huku akinisogelea mwilini. Miongoni mwa sifa za baba, huwa hapendi kabisa mtu muongo, ni bora akikuuliza unyamaze kuliko kutoa majibu ya uongo. Ili kuepusha shari, nilinyamaza na kujiinamia.
“Si naongea na wewe?”
“Wakati naingia nilipakaza damu hapo kwenye mlango,” nilisema, akaonesha kushtuka mno, hakusema kitu zaidi ya kunishika mkono, akawa ananivutia ndani huku akiendelea kujifuta damu.
Tulienda mpaka kwenye kile chumba changu, tukaingia huku baba akiwa makini kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayetutazama. Wakati naingia, nilitupia macho kwenye mlango wa chumba cha Rahma, nikamuona akiwa anatuchungulia. Nilimuonesha ishara kwamba anisubiri, akatingisha kichwa kuniitikia.
“Mimi ni nani kwako?”
“Ni baba yangu.”
“Haya nataka unieleze kila kitu, umetokaje mahabusu na nini kimetokea mpaka ukapaka damu kwenye mlango,” alisema baba kwa sauti ya chini, lakini akionesha kutokuwa na hasira na mimi.
Kabla sijamjibu, niliingiza mkono mfukoni na kutoa ile dawa ya ajabu ambayo kwa kiasi kikubwa ilinisaidia sana.
“Hiyo ni mimi nilikuwekea muda ule wakati polisi wanakuchukua, naamini imekusaidia sana,” alisema baba huku akiichukua ile dawa mikononi mwangu na kuiweka kwenye mfuko wa shati. Ni hapo ndipo nilipoanza kupata picha juu ya nini kilichotokea.
“Sasa baba, unataka nikueleze nini wakati kumbe unajua kila kitu na wewe ndiye uliyenielekeza jinsi ya kutoka mahabusu?”
“Unachokisema ni sawa lakini najua kuna mambo mengi yametokea ukiachilia mbali wewe kutoka mahabusu na ndiyo maana nimekutoboa mkono wako na kukinga damu yako, mimi ni baba yako na hakuna mtu mwenye uchungu na wewe kuliko sisi wazazi wako, ni lazima ujifunze kuniamini na kuwa muwazi kwangu,” alisema.
Kiukweli sikuwahi kumsikia baba akizungumza kwa busara na mimi kiasi hicho, yaani ni kama alikuwa akizungumza na mkubwa mwenzake na hata ule ukali wake wa siku zote, hakuuonesha kabisa.
Nilishusha pumzi na kukaa vizuri, sikuona sababu ya kuendelea kumficha, nilianza kumueleza kila kitu kilichotokea, kuanzia nilipofikishwa kituoni, wale wachawi waliokuja usiku kule mahabusu na jinsi yule mwingine alivyobadilika sura na kufanana na mimi.
Nilipofikia kipengele hicho, baba alinikatisha, akaniambia kwamba dawa aliyokuwa amenipa, ina nguvu kubwa ya kufanya chochote ninachokitaka. Akaniambia kwamba yule mchawi aliyebadilika sura, alishindwa kutoka mpaka asubuhi na askari walipoingia kwa ajili ya kufanya ukaguzi.
“Nasikia wameshtuka sana kumuona, wakadhani ni wewe lakini tofauti ikawa ni kwamba sura mmefanana lakini yeye ni mzee na amekutwa hana nguo hata moja, mtaani kote ndiyo gumzo na hata vyombo vya habari vimeanza kuripoti tukio hilo la ajabu,” alisema baba.
Kauli yake ilinifanya niwe na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kimeendelea, akaniambia nisiwe na wasiwasi atanieleza lakini pia akaniambia kwamba anataka kumtumia yule mchawi kama funzo kwa watu wengine wenye tabia ya kufanya uchawi wa kijinga.
Aliposema uchawi wa kijinga, sikumuelewa anamaanisha nini, nikataka kumuuliza tena lakini aliniambia niendelee kumueleza kilichotokea. Nilimueleza kila kitu na jinsi nilivyokutana na yule msichana usiku ule.
“Lakini si nilishakukataza kuwa karibu na Isri?” alisema huku akinitazama usoni, nilishtuka kumsikia baba akimtaja jina. Kwa ilivyoonesha, kumbe baba alikuwa akimfahamu vizuri msichana huyo na hata aliponikataza kuwa naye karibu, alikuwa na maana yake.
“Huyo si ndiye aliyekusababishia matatizo mpaka ukakamatwa kwa tuhuma za mauaji? Ina maana wewe hukushtuka mtu amekufia mchana gesti halafu usiku unakutana naye tena? Akili zako zinafanya kazi sawasawa kweli?” baba alinibadilikia, nikawa nataka kujitetea lakini alinikatisha na kuniambia anaelewa kila kitu kilichotokea kati yetu.
“Hebu hiyo mikono yako,” alisema, nikasita kidogo lakini baadaye nilimpa, akaishika na kuanza kuitazama upande wa mbele kisha akanitazama usoni.
“Na wewe umeshakuwa kama yeye,” alisema huku akiniachia, akaniambia nifumbue mdomo wangu. Nilifanya hivyo, akawa anayatazama meno yangu kwa makini. Bado nilikuwa na maswali mengi kuliko majibu na ilionesha kwamba baba anamfahamu vizuri sana Isri.
Kitendo cha kutazama mikono yangu kisha wakati huohuo akaanza kukagua meno yangu, kilitosha kunifanya nielewe kwamba kumbe anajua jinsi msichana huyo alivyonigeuza na kuwa kiumbe wa ajabu.
“Umewapa ushindi maadui zangu kwa sababu ya mambo yako ya kipumbavu,” alisema baba huku akiinuka, bado damu zilikuwa zikimtoka puani ingawa safari hii haikuwa kwa wingi kama ilivyokuwa mwanzo.
Alipotaka kutoka, nilimuita, akageuka na kunitazama, nikamwambia Isri ameniambia nisitoke nje mpaka giza litakapoingia, akanijibu kwa kifupi kwamba anajua kisha akaondoka zake.
Harakaharaka niliinuka na kukimbilia bafuni kwani nilikuwa najisikia aibu kukutana na Rahma nikiwa na harufu mbaya kiasi kile, nikajifungia na kufungulia maji kwa wingi, nilivua nguo zangu kisha nikaanza kujimwagia maji huku nikijikagua kama hakukuwa na kitu chochote kisicho cha kawaida mwilini mwangu.
Mara nilisikia mlango wa bafu ukigongwa, nikahisi ni Rahma amenifuata, harakaharaka nikaufungua, nikakutana uso kwa uso na baba.
“Ogea hii,” alisema huku akinipa ile dawa ambayo aliwahi kunipa niogee, ambayo ukiogea mwili unatoa uchafu mweusi kama mkaa. Nilimshukuru na kufunga mlango, nikaendelea kuoga. Maji machafu, meusi tii yalianza kunitoka, safari hii nikawa sina wasiwasi maana nilikuwa naelewa kinachotokea.
Nilioga mpaka uchafu wote ukaniisha mwilini, nikachukua nguo zangu na kuzikung’uta sana kisha nikavaa na kutoka. Rahma alikuwa amesimama kwenye mlango wa chumba chake, akionesha kunisubiri kwa shauku kubwa.
Hakuwa amevaa chochote zaidi ya kujifunga upande wa khanga nyepesi, akawa ananitazama usoni kwa macho yake mazuri, ambayo yalikuwa ni kama yana usingizi kwa jinsi yalivyolegea.
Nilitazama huku na kule, nilipoona hakuna mtu anayetutazama, nilimsogelea, akanikumbatia kwa mahaba kisha akanivutia ndani. Hatukukumbuka hata kufunga mlango, kwa makusudi aliuachia ule upande wa khanga, ukadondoka chini, nikawa kama fisi aliyeona mfupa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 37
ILIPOISHIA:
Nilitazama huku na kule, nilipoona hakuna mtu anayetutazama, nilimsogelea, akanikumbatia kwa mahaba kisha akanivutia ndani. Hatukukumbuka hata kufunga mlango, kwa makusudi aliuachia ule upande wa khanga, ukadondoka chini, nikawa kama fisi aliyeona mfupa.
SASA ENDELEA...

Harakaharaka nilichojoa magwanda yangu huku nikiwa na pupa isiyo na mfano, muda mfupi baadaye tulikuwa saresare maua, nikamnyanyua Rahma juujuu na kumbwaga kwenye uwanja wa fundi seremala. Mwenyewe alionesha kufurahia sana, akanibana kwenye kifua chake kilichojaa vizuri, tukagusanisha ndimi zetu.
Hata hivyo, tofauti na mara zote ninapokuwa kwenye mazingira kama hayo, ambapo ‘Togo’ wangu huwa mkali kama nyoka koboko, nilishangaa akiwa kimya kabisa, kama hajui ni nini kilichokuwa kinataka kutokea.
Kama nilivyoeleza tangu mwanzo, sikuwa najua chochote kwenye ulimwengu wa kikubwa na Rahma ndiye aliyekuwa wa kwanza kuniingiza kwenye ulimwengu huo, akifuatiwa na Isri, tena ndani ya siku chache tu. Kwa hiyo, sikuwa mzoefu na hicho kilichotokea, kilikuwa kitu kigeni kabisa kwangu.
Nimewahi kusikia kwamba, kwa mwanaume, hakuna aibu kubwa kama kuwa na mwanamke faragha halafu ukashindwa kazi, nikajikuta nikiwa na wasiwasi mkubwa kweli ndani ya moyo wangu. Sikujua Rahma atanichukuliaje, sikujua atanidharau kwa kiasi gani, nikajikuta kijasho chembamba kikinitoka huku akili ikiwa imehama kabisa.
“Togo, vipi?” aliniuliza Rahma baada ya kubaini mabadiliko niliyokuwa nayo. Swali lake lilinifanya nizidi kujisikia aibu, nilikosa cha kujibu na kiukweli sikuwa na majibu. Alipeleka mkono bondeni yaliko makazi ya ‘Togo’ na kujaribu kumpa hamasa kwa kutumia mikono yake laini lakini ilikuwa sawa na kazi bure.
“Mshukuru sana Mungu wako, ulikuwa unaenda kumuua mtoto wa watu, mshenzi sana wewe,” nilisikia sauti ya baba ikiniongelea sikioni kwa ukali, ikafuatiwa na msonyo mrefu, nikakurupuka kwa hofu kubwa, nikawa namtazama Rahma nikiwa nimekodoa macho, kijasho chembamba kikinitoka.
Nilikumbuka tukio lililonitokea na Isri, nilipokutana naye kwa mara ya kwanza faragha, ambapo tukiwa mchezoni, ghafla ‘alikata roho’ ingawa baadaye nilikutana naye tena akiwa mzima na ndiyo yakatokea yale yaliyotokea usiku uliopita. Alichokisema baba kilinifanya nihisi kwamba huenda kuna kitu kibaya mwilini mwangu ambacho ndiyo chanzo cha yote na nikifanya masihara, kweli Rahma atakufa na kusababisha msiba mzito kwa familia yake.
Nilikumbuka pia kauli ya Isri kwamba mimi ndiye mwanaume pekee niliyeweza kuushinda mtihani wa kifo baada ya kukutana naye kimwili.
“Togo, una nini mpenzi wangu,” alisema Rahma huku akisimama, naye akionesha kushangazwa na kilichotokea. Alinisogelea na kutaka kunikumbatia lakini nilijitoa harakaharaka, nikavaa nguo zangu huku nikiendelea kuhema kwa nguvu, nikamuona Rahma akikaa pembeni ya kitanda na kujiinamia, machozi yakaanza kumtoka.
Niliondoka haraka na kuelekea bafuni, nikajifungia mlango kwa ndani na kujiinamia, nikiwa hata sielewi nini cha kufanya. Ilibidi nijimwagie tena maji, mwili wangu ukapata nguvu, nikatoka na kwenda chumbani kwangu, nikawa nimejilaza huku nikiendelea kutafakari kilichotokea.
Kwa mbali ile kiu kali ya kukutana kimwili na mwanamke ilinianza upya, nikawa najiuliza, inawezekanaje muda mfupi tu uliopita nimeshindwa kabisa kufanya chochote na Rahma na kumuacha akiwa na huzuni kubwa kwenye moyo wake, halafu dakika chache baadaye niwe na hamu kali isiyoelezeka.
Nilipokumbuka ile kauli ya baba, niliona kabisa kinachoenda kutokea ni janga kubwa kwa Rahma kwa sababu muda si mrefu, mimi ningeenda chumbani kwake au yeye angekuja kwangu, tungeanza kubembelezana na mwisho tungeishia kuangukia dhambini, na matokeo yake dhambi ingekomaa na kuzaa mauti kwa Rahma, jambo ambalo lingenifanya niishi na hatia ya kukatisha maisha ya mtu asiye na hatia milele.
Nilichokifanya, harakaharaka niliamka pale kitandani, nikavaa viatu vyangu na kutaka kutoka lakini nilikumbuka kwamba giza halikuwa limeingia kwa hiyo kutoka nje kungemaanisha kwamba ningepata madhara makubwa kama Isri alivyonipa masharti.
Niliamua kwenda kukaa sebuleni, ndugu zangu pamoja na wadogo zake Rahma wakawa wananishangaa. Kwa muda mfupi tu tuliokaa hapo nyumbani, tayari nilishaonesha tabia za ajabu sana. Kila mtu akawa ananitazama kwa macho ya chinichini, haikuwa kawaida yangu kukaa sebuleni.
Nilijikaza kiume, nikakazia macho kwenye runinga, nikawa sina habari na mtu, ukimya ukatanda pale sebuleni. Baba na baba yake Rahma walikuwa wamekaa kwenye sehemu ya kulia chakula, wakiwa wanacheza bao huku mama na mama yake Rahma wenyewe wakiwa jikoni.
Muda mfupi baadaye, Rahma alikuja na kuchungulia pale sebuleni, alipochungulia tu, macho yangu na yake yakagongana, akanionesha ishara ya kuniita kwa mkono kisha nikamsikia akitembea kuelekea chumbani kwake.
“Mungu wangu, sasa itakuwaje?” niliwaza, nikaamua kujikausha kama sijamuona Rahma, nikawa naendelea kukazia macho kwenye runinga imngawa kiukweli wala akili zangu hazikuwa pale na sikuwa najua hata kunaoneshwa nini.
Muda mfupi baadaye, Rahma alikuja tena lakini safari hii, alikuja na kukaa kwenye kochi nililokuwa nimekaa mimi, uso akiwa ameukunja. Nilijua kwamba amekasirika lakini sikuwa na namna zaidi ya kujiepusha naye, nilikuwa nampenda Rahma na sikuwa tayari kuona anapatwa na jambo lolote baya.
Alikuwa amejifunga khanga nyepesi na ndani hakuwa na kitu kabisa, nikazidi kujikuta kwenye wakati mgumu, tukawa tunatazama runinga bila mtu yeyote kumsemesha mwenzake. Hata wale ndugu zetu nadhani nao waligundua kwamba hatupo sawa kwa sababu si kawaida ya mimi na Rahma kukaa sehemu moja bila kusemeshana, tena mara nyingi tulikuwa tukicheka na kufurahi.
Dakika kadhaa baadaye, Rahma alibadili mkao aliokuwa amekaa, akanisogelea halafu akawa ni kama ameniegamia kimtindo, haikuwa rahisi kwa watu wengine kuelewa kilichokuwa kinaendelea lakini kiukweli nilijikuta nikipata msisimko mkubwa sana.
Mwisho niliamua kukata shauri maana na mimi nilikuwa nateseka, nikaamua liwalo na liwe, nikamgeukia Rahma na kumtazama usoni, naye akanigeukia, tukawa tunatazamana machoni, nikampa ishara kwamba atangulie ndani, akaniitikia huku akinitazama kwa macho yenye hisia kali za mapenzi.
Aliinuka na kutembea kwa madoido, nikawa namsindikiza kwa macho, nikawaona watu wote pale sebuleni wakitazamana. Nilishusha pumzi ndefu na kukaa vizuri kwenye kiti, nikawa navutia kasi ili na mimi niinuke na kumfuata Rahma kule ndani, tukatii kiu zetu.
“Togoo,” nilisikia sauti ya baba akiniita, nikaitika na kusimama, ilibidi nijiweke vizuri maana ilikuwa aibu kwa wote waliokuwa pale sebuleni, nikaelekea kule walikokuwa wamekaa baba na baba yake Rahma.
“Wewe sasa hivi una mambo ya kikubwa, hutakiwi kuwa unachanganyikana na wenzako, inabidi uanze kukaa na sisi baba zako, vuta kiti kaa hapa,” alisema baba, akawa ametibua shoo nzima, nilitaka kutoa visingizio lakini hakutaka kusikia chochote kutoka kwangu, ikabidi nikae na kujiinamia, wote wakawa wananitazama.
Je, nini kitafuatia?
 
  • Thanks
Reactions: Lee
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 38
ILIPOISHIA:
“Wewe sasa hivi una mambo ya kikubwa, hutakiwi kuwa unachanganyikana na wenzako, inabidi uanze kukaa na sisi baba zako, vuta kiti kaa hapa,” alisema baba, akawa ametibua shoo nzima, nilitaka kutoa visingizio lakini hakutaka kusikia chochote kutoka kwangu, ikabidi nikae na kujiinamia, wote wakawa wananitazama.
SASA ENDELEA...

“Una matatizo gani?” baba aliniuliza baada ya kuniona nikiwa nimekaa huku uso wangu nikiwa nimeukunja.
“Unajua hata sisi wote unaotuona hapa, kuna kipindi tulikuwa kama wewe, sote tulikuwa vijana hapa na tulipitia yote unayoyapitia, kwa hiyo usitake kujifanya mjanja, umenisikia?” baba alisema kwa msisitizo.
“Na nyie mlipitia mauzauza kama yangu? Kwa nini kila siku huniambii ukweli mimi ni nani?” kwa mara ya kwanza nilimpandishia baba sauti mbele ya baba yake Rahma, nikaona wameacha kucheza karata, wakawa wanatazamana kisha wote wakanigeukia.
“Sisi ni baba zako, hutakiwi kuzungumza kwa namna hiyo, umesikia mwanangu,” alisema baba yake Rahma huku akinipigapiga begani. Tofauti kati ya baba na baba yake Rahma, yeye alikuwa na busara na mpole lakini baba yeye alizoea kufokafoka tu.
“Hapana mimi nimechoka, kila siku nikimuuliza baba aniambie ukweli hataki, mauzauza yanazidi kunitokea kila siku, mambo ya ajabu yananikumba mimi tu, mbona ndugu zangu hakuna anayepata shida kama mimi,” nilisema kwa uchungu huku machozi yakianza kunilengalenga.
Baada ya kusema ya moyoni, niliegamia meza na kujilaza huku machozi yakinitoka, kiukweli nilikuwa na dukuduku kubwa sana moyoni. Hakuna kitu ambacho kilikuwa kikinikasirisha kama kitendo cha baba kuwa ‘ananikontroo’ kama roboti bila kunieleza ukweli uliokuwa nyuma ya maisha yangu.
“Najua kwamba mimi ni mwanaye, tena anayenipenda kuliko watoto wengine wote lakini kwa nini nipo tofauti? Kwa nini haniambii ukweli?” nilisema kwa kulalama, machozi yakiwa yanaendelea kunitoka.
“Kama anaweza kufikiria haya maana yake ni kwamba ameshapevuka kiakili, nafikiri ni muda muafaka wa yeye kuujua ukweli.”
“Hapana, bado hajakua huyu, ana mambo ya kitoto sana, mimi ndiyo namjua,” baba alisema, kauli ambayo ilinifanya niinuke pale mezani na kumkodolea baba macho. Yaani kumbe alikuwa anashindwa kunieleza ukweli kwa kipindi chote hicho kwa sababu tu alikuwa anahisi kwamba mimi bado nina akili za kitoto?
Kauli ile ilinifanya nijiulize maswali mengi yaliyokosa majibu. Kwa nini baba alikuwa ananiona mimi kama bado mtoto wakati tayari nilishapevuka na kuwa mwanaume kamili? Hata Rahma aliniambia kwamba mimi ni kidume cha mbegu, achilia mbali Isri aliyekuwa akinisifia sana. Na kama ni hivyo, mbona pale aliponiita alisema nimeshakua mkubwa kwa hiyo natakiwa kukaa nao?
“Kwa nini unaniona bado mdogo?”
“Kwa sababu huwezi kuelewa kitu kwa kuelezwa mara moja. Kila unachokatazwa kufanya wewe unafanya,” alisema baba na kurudia kauli yake kwamba hawezi kuniamini kwa asilimia mia moja mpaka nitakapomuonesha ukomavu wangu wa akili.
Kiukweli kwa kipengele hicho baba alikuwa amenishinda kwa pointi na udhaifu wangu mkubwa nilikuwa nimeuonesha kwenye suala zima la mapenzi. Nakumbuka tulianza kutofautiana na baba baada ya kukutana na Isri kwenye basi, akawa ananikataza kuwa naye karibu lakini nikampuuza.
Pia hata tulipofika kwa akina Rahma, mara kadhaa alishagundua kwamba tulikuwa na ukaribu usiofaa na akanikataza kwa msisitizo kwamba nisijaribu kukutana kimwili na Rahma, tena mpaka wakatumia kigezo kwamba sisi tulikuwa ndugu lakini bado tuliangukia dhambini, tena siyo mara moja.
Kubwa zaidi, hata hapo tulipokuwa tukizungumza, licha ya baba kunikataza kwamba endapo nitakutana kimwili tena na Rahma basi atakufa, kama wasingeniita na kunizuia, pengine muda huo ningekuwa ‘nikilitafunilia mbali tunda la mti uliokatazwa’ na Rahma.
Kama kigezo hicho pekee ndicho kilikuwa kinaonesha kwamba mtu amekuwa mkubwa, basi ni kweli nilikuwa nimefeli mtihani uliokuwa mbele yangu, nikawa mdogo kama ‘piriton’.
“Eti ni kweli anachokisema baba yako?” aliniuliza baba yake Rahma, nikakosa cha kujibu.
“Unajua kwa jinsi sisi baba zako tulivyo, na pengine wewe ukija kupata nafasi hiyo, hakuna kitu ambacho kinaheshimika kwenye jamii yetu kama utii. Ukiambiwa jambo ni lazima ufanye vilevile ulivyoambiwa na si vinginevyo, kosa dogo tu linaweza kusababisha matatizo makubwa mno ndiyo maana baba yako anakuwa mkali,” alisema baba yake Rahma.
Kauli hiyo ilinifanya nijiulize maswali mengine mengi zaidi. Aliposema ‘jamii yetu’, baba yake Rahma alikuwa akimaanisha nini? Nilianza kupata picha kwamba huenda naye alikuwa anafahamu kila kitu kinachoendelea na kama alikuwa jamii moja na baba, basi moja kwa moja na yeye alikuwa akishughulika na mambo kama yale ya baba.
Tangu tumefika, baba yake Rahma hakuwahi kutoka kwamba labda anaenda kazini au kwenye biashara zake, muda wote alikuwa nyumbani tu lakini alikuwa na maisha ya hali ya juu sana. Nikiwa bado naendelea kujiuliza maswali mengi, baba yake Rahma alinisogelea.
“Baba yako anasema hakuamini kwa sababu bado una akili za kitoto lakini mimi nikikutazama nakiona kitu kikubwa sana ndani yako, tucheze dili?” aliniuliza kwa sauti ya chini huku akinikonyeza kwa jicho moja. Sikujua ni dili gani ila kwa sababu nilikuwa nataka kujua ukweli wa maisha yangu, nilitingisha kichwa kuonesha kumkubalia.
“Inatakiwa mimi na wewe tukazungumze lakini hatuwezi kuzungumzia humu ndani, inabidi tutoke nje! Lakini hapohapo, baba yako ameniambia kwamba kuna ‘madhambi’ mengine umeyafanya kiasi kwamba wewe na yeye hamuwezi kutoka mpaka giza liingie, ni kweli au si kweli?”
“Ni kweli.”
“Sasa mtihani wa kwanza, unatakiwa ukazivunje hizo nguvu zako za giza ulizozitega pale mlangoni.”
“Mimi sina nguvu zozote za giza wala sijatega chochote...” nilimkatisha lakini alinitazama usoni na kunikumbusha kwamba utii ni jambo muhimu sana, nikaufyata mkia.
“Unauona ule mlango, inatakiwa utembee kinyumenyume mpaka pale, ukiukaribia, unaugeukia lakini unatakiwa kufumba macho, kisha unakojoa mkojo wa kutosha kulowanisha eneo lote la mlango,” alisema baba yake Rahma, macho yakanitoka kama mjusi aliyebanwa na mlango.
“Hakuna kitu kinachoweza kuvunja na kumaliza kabisa nguvu za giza kama mkojo, haya fanya kama nilivyokwambia,” alisema baba yake Rahma. Ama kweli huo ulikuwa mtego mkali sana kwangu, yaani nikakojoe mlangoni, tena mahali ambapo watu wote waliokuwa sebuleni wangeweza kuniona?
Sikujua ndugu zangu watakichukuliaje kitendo hicho, wala sikujua Rahma na wadogo zake nao watanichukuliaje ila kwa sababu nilikuwa na shauku ya kuujua ukweli, nilipiga moyo konde.
Wakati nikijiandaa kwenda, nilimsikia Rahma akiimba huku akitoka koridoni na kwenda kule sebuleni, nadhani alishachoka kusubiri na kuamua kunifuata, mtihani ukazidi kuwa mgumu. Ningemjibu nini Rahma endapo angeniuliza kwa nini nakojoa mlangoni wakati choo kipo, tena siyo kwamba nimelewa au naumwa, nina akili zangu timamu kabisa!
Baba na baba yake Rahma walikuwa wametulia wananitazama huku nikimuona baba uso wake ukionesha ishara kama anayesema ‘hawezi huyu, akili zake bado za kitoto’. Niliamua kujilipua, nikasema liwalo na liwe, nilisogea usawa wa mlango, nikageuka na kuupa mgongo, nikaanza kutembea kinyumenyume kuuelekea kisha nikafumba macho, nilipoukaribia, niligeuka, macho nikiwa nimeyafumba.
Nilifungua zipu kisha nikaanza kufanya kama vile nilivyoelekezwa. Nikiwa naendelea na kitendo kile cha aibu na cha aina yake, nilisikia watu wote waliokuwa sebuleni wakishtuka, nadhani waliniona nilichokuwa nakifanya, sikuwajali, nikaendelea kuumwaga, mara kilisikika kishindo kikubwa ambacho kilinifanya nishindwe kuendelea kufumba macho, nikayafumbua.
“Mungu wangu!” nilisema kwa sauti ya juu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 39
ILIPOISHIA:
Nilifungua zipu kisha nikaanza kufanya kama vile nilivyoelekezwa. Nikiwa naendelea na kitendo kile cha aibu na cha aina yake, nilisikia watu wote waliokuwa sebuleni wakishtuka, nadhani waliniona nilichokuwa nakifanya, sikuwajali, nikaendelea kuumwaga, mara kilisikika kishindo kikubwa ambacho kilinifanya nishindwe kuendelea kufumba macho, nikayafumbua.
“Mungu wangu!” nilisema kwa sauti ya juu.
SASA ENDELEA...

Kile kilichokuwa kikinitoka, hakikuwa haja ndogo kama mwenyewe nilivyokuwa nadhani, ilikuwa ni damu, tena nzito kabisa yenye wekundu uliokolea kisawasawa, na kile kishindo kilichosikika, kilikuwa ni cha dude kubwa lililoanguka kutoka angani.
Sijui niliiteje dude hilo kwa sababu kwanza lilikuwa na miiba kama nungunungu, lakini pia lilikuwa na mabawa yenye kucha kama popo, ukubwa wake ulikuwa kama ng’ombe mdogo.
Usoni lilikuwa na pembe zilizojikunja na sehemu ya macho, kulikuwa kumezibwa kabisa, kwa kifupi halikuwa na macho. Ile damu iliendelea kunitoka, hata pale nilipotaka kuikata haja ndogo, iliendelea kunitoka kwa wingi utafikiri inavutwa na bomba.
Lile dude la ajabu, lilijiburuta chini na kusogea mpaka pale nilipokuwa natolea haja ndogo, kwenye vizingiti vya milango, likafumbua mdomo kidogo na kutoa ulimi mrefu uliokuwa umegawanyika katikati kama wa nyoka, likaanza kulamba kile nilichokuwa nakitoa.
Naomba nieleze vizuri kilichotokea na ambacho huwa kinatokea pale mtu anapokumbwa na nguvu za uchawi. Yaani tukio unaliona, na ile hatari iliyopo mbele yako unaiona kabisa lakini mwili unakufa ganzi, unakuwa huwezi kufanya chochote zaidi ya kile ambacho unakuwa umeshaanza kukifanya na akili zako zinakosa maamuzi, kwa kifupi unakuwa siyo wewe.
Hicho ndicho kilichotokea, sikuwa na uwezo wa kuikatisha ile haja ndogo ya damu, sikuwa na uwezo wa kwenda mbele, wala sikuwa na uwezo wa kurudi nyuma, nilitamani kupiga kelele za kuomba msaada lakini pia sikuweza kufanya hivyo, nikabaki nimeduwaa tu.
Lile dude lililamba ile damu yote pale mlangoni, likaona haitoshi, likafumbua mdomo wake ambao ulikuwa na meno mengi na kukinga ile iliyokuwa ikiendelea kunitoka kupitia haja ndogo, nikasikia kitu kama ganzi ikinipata kwenye maeneo yangu nyeti kisha ile damu ikakata.
Lile dude ambalo ama kwa hakika lilikuwa linatisha, likajilamba na kugeuka, likajikung’uta kwa nguvu kwenye mabawa yake yenye kucha kubwa na kali, likawa kama linataka kuruka kwani lilipigapiga mbawa zake, kufumba na kufumbua, likayeyuka na kupotea.
Lilipopotea tu, nilihisi kichwa kikiwa kizito, nikaanza kuona giza machoni mwangu, nikawa nasikia sauti za ajabuajabu masikioni, nikadondoka chini kama mzigo. Sikuelewa tena kilichoendelea.
***
Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nimelala chini kwenye majani, mwili wangu ukiwa unahisi baridi kali kuliko kawaida. Kilichonizindua zilikuwa ni kelele za ngoma na manyanga na sauti za ajabuajabu za watu wakiimba nyimbo kwa lugha ambayo sikuwa naielewa.
Nilifumbua macho, huku mapigo yangu ya moyo yakiwa yananienda mbio kuliko kawaida, macho yangu yalitazama juu moja kwa moja. Nikawa naziona nyotanyota kwa mbali kuashiria kwamba ni usiku sana, lakini pia upande wangu wa kushoto, kulikuwa kumewashwa moto mkubwa ambao ulipafanya pale nilipolala, pawe na mwanga.
Niligeuza shingo kutazama pale ni wapi, nilishtuka kugundua kwamba kumbe nilikuwa katikati ya duara, watu wengi waliokuwa hawana kitu mwilini zaidi ya kujiziba kidogo na nguo nyeusi au nyekundu kwenye maeneo nyeti walikuwa wamenizunguka. Wengine ambao ni wanawake, walikuwa wamejiziba pia vifuani mwao.
Walikuwa wakiimba na kucheza kwa kuzunguka duara ambalo ndani yake nilikuwa nimelazwa mimi na pia kulikuwa na moto mkubwa jirani kidogo na pale nilipokuwa nimelala. Walikuwa wakiimba na kucheza, huku kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa.
Nilishtuka mno, nikawa sielewi pale ni wapi na nimefikaje, nilijaribu kuwatazama watu hao kwenye nyuso zao kama kuna yeyote ninayeweza kumtambua lakini macho yangu hayakuwa na nguvu za kutosha kuona. Nilitaka kusimama lakini nilishtuka zaidi kugundua kwamba kumbe nilikuwa nimefungwa mikono na miguu kwa kamba za miti.
Zile purukushani zangu, ziliwafanya wale watu waache kila walichokuwa wanakifanya, wote wakawa wananitazama. Niligeuka huku na kule, wote walikuwa wamenikazia macho. Kilichozidi kunitisha, macho yao yalikuwa yakiwaka kama wanyama wakali wa porini.
Nikamsikia mmoja kati yao akizungumza kwa lugha ambayo sikuwa naielewa, watu wote wakainua mikono juu kisha taratibu wakaishusha chini, wakati wakishusha mikono, nao walishuka mpaka wakapiga magoti, wakapeleka vichwa vyao mpaka chini kisha wakainuka na kusimama kama mwanzo.
Yule mwanaume ambaye sikuwa najua yupo upande gani, aliyarudia tena maneno yale, wakafanya hivyo tena mpaka chini, wakarudia mara tatu kisha wote wakakaa chini na kukunja miguu.
Kizee kimoja kilichokuwa kimepinda mgongo, kiliibuka kutoka kusikojulikana, kikiwa kinatembelea mkongojo. Kikawa kinajikongoja kuja pale nilipokuwa nimefungwa, kadiri kilivyokuwa kinanikaribia ndivyo mapigo ya moyo wangu yalivyokuwa yakizidi kuongezeka.
Sikujua kinataka kunifanya nini, kilisogea mpaka pale nilipokuwa nimefungwa, nikakiona kikitoa kisu kikali, kikaniinamia huku kikiyumbayumba, nikajua nimekwisha. Nimewahi kusikia kwamba wachawi wana mchezo wa kuchinja watu na kuwala nyama, nikajua na mimi ndiyo siku yangu ya kuliwa imewadia.
Tofauti na nilivyotegemea, wala hakunidhuru mwilini, badala yake alikitumia kile kisu kukata kamba nilizofungwa mikononi na miguuni. Kilichonishangaza zaidi, kumbe alikuwa akinijua mpaka jina langu kamili.
“Togolai!”
“Naam, shikamoo babu,” niliitikia kwa kutetemeka. Hakujibu salamu yangu, badala yake alinionesha sehemu ya kukaa, akaniambia kwa ishara nikunje miguu kama watu wengine wote walivyokuwa wamekaa. Nilitii agizo hilo haraka.
Kumbe pembeni ya pale nilipokuwa nimelazwa, kulikuwa na vifaa mbalimbali, nikamuona akichukua kibuyu kimoja, akakitingisha kisha akanipa na kunionesha kwa ishara kwamba ninywe kilichomo ndani.
Huku nikitetemeka, nilikishika kibuyu hicho, nikawa nakipeleka mdomoni huku nikimtazama kwa kina mzee huyo, pamoja na watu wengine waliokuwa wamenizunguka kwa mbali.
“Nwa, ulogoleza shoni, nwa!” aliongea kwa kilugha ambacho sikuwa nakielewa lakini kwa jinsi matamshi yake yalivyokuwa, nilihisi ananiambia, ‘kunywa, unaogopa nini, kunywa’.
Nilipokisogeza kibuyu hicho karibu na pua, nilikumbana na harufu kali kwelikweli, ikabidi nizibe pua, nikanywa huku nikiwa nimefumba macho. Kabla sijameza, nilisikia vitu vikinitembea mdomoni, nilipotazama vizuri kile kibuyu, pale kwenye mdomo wa kunywea, sikuyaamini macho yangu, nikataka kutema lakini tayari nilishachelewa, vitu vyote vilikimbilia tumboni vyenyewe.
Je, nini kitafuatia?
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 40
ILIPOISHIA:
Nilipokisogeza kibuyu hicho karibu na pua, nilikumbana na harufu kali kwelikweli, ikabidi nizibe pua, nikanywa huku nikiwa nimefumba macho. Kabla sijameza, nilisikia vitu vikinitembea mdomoni, nilipotazama vizuri kile kibuyu, pale kwenye mdomo wa kunywea, sikuyaamini macho yangu, nikataka kutema lakini tayari nilishachelewa, vitu vyote vilikimbilia tumboni vyenyewe.
SASA ENDELEA...

Pale kwenye sehemu ya kunywea, ndipo paliponipa picha kwamba nilichokunywa kilikuwa ni kitu gani. Minyoo mingi ya rangi mbalimbali, ilikuwa imechanganywa na maji machungu yenye harufu mbaya mno. Jambo lile, la kugundua kwamba nilikuwa nimekunywa minyoo, lilinifanya nisisimke sana, nilijaribu kujitapisha lakini ilikuwa sawa mna kazi bure.
Kwa jinsi minyoo yenyewe ilivyokuwa imechangamka, muda mfupi tu baadaye, nilisikia tumbo likianza kutibuka, hofu kubwa ikanitanda ndani ya moyo wangu. Sikujua nini itakuwa hatma yangu.
Yule babu alikichukuaa kibuyo na kukifunga, akakirudisha pale chini, nikamuona akichaguachagua na muda mfupi baadaye, alichukua kibuyu kingine lakini hiki kilikuwa kidogo kuliko kile cha awali. Akawatazama wale watu wengine waliokuwa wamekaa pembeni na kutulia kisha akawapa ishara fulani, nikaona wanaume wawili wakiinuka.
Wakatembea harakaharaka kusogea mpaka pale nilipokuwa nimekalishwa. Sikutaka kuyaamini macho yangu, ilibidi nijifikiche macho nikidhani labda nipo ndotoni.
Haikuwa ndoto, ilikuwa ni kweli kabisa. Mbele yangu walikuwa wamesimama baba na baba yake Rahma. Niliwatazama mmoja baada ya mwingine, bado nikawa siamini. Nao walikuwa wamevaa kama wale watu wengine, walijistiri kidogo tu lakini sehemu kubwa ya miili yao ilikuwa wazi.
Ni hapo ndipo nilipoielewa kauli ya baba yake Rahma aliyoitoa muda mfupi kabla ya yale mauzauza hayajanitokea, kwamba eti utii ni jambo muhimu sana na la lazima kwa jamii yao. Kumbe urafiki au ukaribu wa baba na baba yake rahma ulikuwa zaidi ya vile kila mmoja alivyokuwa akiamini.
Yule mzee alimtazama baba, baba naye akamtazama kisha kichwa chake akakiinamisha kwa utii, yule babu akawa anaongea kwa lugha ambayo hata sikuwa naielewa, baba naye akawa anamfuatisha anachokisema, muda mfupi baadaye baba yake Rahma naye alikuwa akifuatisha walichokuwa wanakisema.
Muda mfupi baadaye, walinizunguka na kutengeneza kama duara jingine hivi, wakawa wanaendelea kuzungumza yale maneno kwa sauti ya juu, muda mfupi baadaye wale watu wengine nao walidakia, wakawa wanawafuatisha. Ilivyoonesha, wote walikuwa wakiielewa vizuri lugha ile maana hakuna aliyekuwa akibabaika.
Baadaye, yule mzee alitoa ishara, watu wote wakanyamaza, akaanza kuzungumza lakini safari hii, alikuwa akiongea Kiswahili japo ilionesha hakuwa akikielewa vizuri. Akawaambia watu wote kwamba anayo furaha kubwa kukutana nao usiku huo na furaha yake iliongezwa zaidi na tukio lililokuwa likifanyika usiku huo.
Aliwaambia watu wote kwamba kulikuwa na utambulisho wa mwanachama mpya, akanitaka nisimame. Nilishtuka sana, mwanachama mpya? Wa nini? Ina maana kile ni chama? Kinahusika na nini? Sikuwa na majibu. Nilimgeukia baba, naye akanigeukia, akanipa ishara kwamba nitulie.
Yule babu alimkabidhi baba kile kibuyu, nikamuona akirudi tena pale palipokuwa na vifaa vingine, akachaguachagua kisha nikamuona akichukua kitambaa cheusi, au wengine wanapenda kuita kaniki. Alimpa baba, akainamisha kichwa chake kama ishara ya utii, kisha yule babu akaendelea kuzungumza na kila mtu.
Alisema hatua ya kwanza natakiwa kukabidhiwa vifaa kwa ajili ya kazi kisha baada ya hapo, nitatawazwa rasmi kuwa mwanachama kamili, watu wote wakalipuka kwa shangwe za kila namna. Zilikuwa ni kelele kubwa sana, kila mtu akionesha kuwa na furaha sana.
Baba aliniinamia, akaongea kwa sauti ya chini akiniambia nivue suruali niliyokuwa nimevaa maana mpaka muda huo nilikuwa kifua wazi. Niliona kama ni jambo lisilowezekana, yaani nivue nguo wakati watu wote wananitazama? Macho yakanitoka.
Ni kama baba alinielewa, alinipa na ile kaniki, akanionesha kwa ishara kwamba nijifunge juu ya suruali kisha ndiyo niiteremshe. Nilifanya hivyo, muda mfupi baadaye, nilikuwa nimeshaivua na kujifunga kaniki. Sasa na mimi nilikuwa nikifanana na wale watu isipokuwa mimi nilijifunga kaniki ndefu wakati wengine wote walikuwa wamejifunika kwa vipande vidogo.
Nilikalishwa chini, yule babu akampa ishara baba, akanisogelea na kupiga magoti, akanikabidhi kile kibuyu kilichokuwa kimevalishwa shanga, kisha akaongea kwa sauti ya chini akinitaka nisiogope chochote na nimthibitishie kwamba kweli nimekuwa mtu mzima na si mtoto kama alivyokuwa akiamini. Nilitingisha kichwa, japokuwa hakuwa ameniambia chochote, tayari nilishaelewa kilichokuwa kinaendelea.
Nilipokabidhiwa kile kibuyu, baba na baba yake Rahma waliondoka na kurudi kwenye sehemu zao, yule babu akaniambia nishike kibuyu hicho kwa mikono miwili kisha nikiinue mbele ya uso wangu.
Nilifanya kama alivyoniambia, nikamuona akichukua karai la chuma lenye maji meusi ndani yake, akanimwagia kichwani kisha kwa kutumia kisu kikali, alianza kuninyoa nywele. Sikuwahi kuona mtu akinyolewa nywele kwa siku, hata kule kijijini kwetu ambako saluni zilikuwa chache, tulikuwa tukinyolewa kwa wembe au mkasi.
Kwa kawaida nywele zangu huwa ni nguvu na wakati wa kunyoa huwa ni shughuli kwelikweli lakini huwezi kuamini, yule babu alipitisha mara kadhaa tu, kichwa kikawa cheupe kabisa. Alichukua dawa kutoka kwenye kichupa kimoja kisha akanisogelea, akarudia kunisisitiza kwamba sitakiwi kuachia kibuyu hicho kwani ndiyo maisha yangu.
Alichokifanya, kwa kutumia kilekile kisu, alianza kunichanja chake, kuanzia kichwani, akaja shingoni upande wa nyuma, akashuka mgongoni mpaka miguuni. Kiukweli maumivu niliyokuwa nayasikia yalikuwa makali sana, yote tisa, kumi ni pale alipoanza kunisugua sehemu alizonichanja kwa kutumia ile dawa iliyokuwa kwenye kile kichupa.
Maumivu ya kuchanjwa ukijumlisha na ukali wa ile dawa, nilishindwa kujizuia, nikawa nalia kwa maumivu.
“Kumbe hujakuwa mrume wewe,” alisema yule babu kwa Kiswahili kibovu lakini ambacho kilinifanya nimuelewe. Alimaanisha kwamba eti bado nilikuwa mtoto ndiyo maana nilikuwa nalia. Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakichukia kama kuitwa mtoto. Japokuwa nilikuwa nikijisikia maumivu makali, ilibidi nijikaze, akaendelea kunisugua na ile dawa huku nikigugumia kwa maumivu.
Damu nyingi ilikuwa ikinitoka kwenye majeraha yangu lakini safari hii sikujali, sikutaka kuonekana mtoto, yule babu akaendelea mpaka alipomaliza. Baada ya kumaliza, alinishika mkono na kunisimamisha, akanisogeza kwenye ule moto.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe pale kulikuwa na nyama nyingi ya kutosha imewekwa pembeni ya moto. Yule babu aliinama pale kwenye nyama, akatoka na kipande kimoja, akanifuata na kunipa.
Kwa akili yangu nilielewa kwamba ananipa ili niichome kwenye moto ikiiva ndiyo niile, nikashangaa ananiambia eti niile vilevile ikiwa mbichi. Nilishtuka sana maana ilikuwa bado na damudamu kabisa.
Nilitamani kumuuliza kwanza ile ni nyama ya nini lakini nilikumbuka kauli ya baba yake rahma na aliyoniambia baba muda mfupi uliopita kwamba natakiwa kuwa mtiifu, ikabidi nifumbe macho, nikaitia mdomoni na kutaka kuimeza bila kutafuna lakini ilikuwa kubwa, ikabidi nipige moyo konde, nikaanza kuitafuna kisha harakaharaka nikameza.
“Twive umile,” alisema yule mzee huku akinionesha kwa ishara kwamba nifumbue mdomo. Sijui kile ni kilugha alichokuwa akizungumza, nilifanya kama alivyoniambia, nikafumbua mdomo. Nadhani alitaka kuhakikisha kama nimemeza, alipohakikisha, alinishika mkono na kuuinua juu kama wanavyofanya waamuzi wa mapambano ya ndondi wanapomtangaza msshi ulingoni.
Watu wote walishangilia kwa nguvu, wengine nikawaona wakirukaruka kwa furaha, ikabidi na mimi nifurahi ingawa bado nilikuwa gizani. Yule mzee aliniachia mkono na kuanza kuzungumza na wale watu, akiwataka wanipe ushirikiano na kunifundisha yale nisiyoyajua.
Wakati anaongea hayo, sijui nini kilinituma nitazame pale zilipokuwepo zile nyama, nikashtuka kuliko kawaida kuona kuna viungo vya binadamu, viganja vya mikono na miguu. Ile nyama aliyonipa aliichukua palepale, kwa hiyo alikuwa amenipa nyama ya mtu? Macho yalinitoka nikiwa siamini macho yangu.
Nikiwa bado nashangaa, mwili ukiwa unatetemeka kwa hofu, nilishtukia wale watu wakikimbilia pale kwenye moto na kujipanga foleni, yule babu akasogea kwenye zile nyama, akawa anagawa, kila mmoja anapita na kupewa kipande chake kisha anatafuta sehemu ya kwenda kukaa na kuanza kula. Nilihisi kama nipo ndotoni lakini haikuwa hivyo.
“Hongera, umekuwa sasa,” alisema baba huku akinikumbatia, akanishika mkono na kunipeleka kwenye foleni, akaniingiza kwenye foleni.
Je, nini kitafuatia? Usikose
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 41
ILIPOISHIA:
Nikiwa bado nashangaa, mwili ukiwa unatetemeka kwa hofu, nilishtukia wale watu wakikimbilia pale kwenye moto na kujipanga foleni, yule babu akasogea kwenye zile nyama, akawa anagawa, kila mmoja anapita na kupewa kipande chake kisha anatafuta sehemu ya kwenda kukaa na kuanza kula. Nilihisi kama nipo ndotoni lakini haikuwa hivyo.
“Hongera, umekuwa sasa,” alisema baba huku akinikumbatia, akanishika mkono na kunipeleka kwenye foleni, akaniingiza kwenye foleni.
SASA ENDELEA...

“Hapana baba, siwezi! Siwezi...” nilisema huku nikitaka kutoka kwenye foleni lakini baba alinishika mkono kwa nguvu. Nilikuwa natafuta upenyo ili nijitie vidole mdomoni kujitapisha ile nyama lakini ni kama baba alinishtukia.
Hakunipa upenyo hata kidogo, nikawa naendelea kutetemeka kwa hofu kubwa, nikiwa sielewi hatima ya yote yale itakuwa nini. Tofauti na mimi, watu wengine wote waliokuwepo eneo lile, akiwemo baba, baba yake Rahma na wale watu wengine wote, walikuwa na furaha kubwa ndani ya mioyo yao.
Kingine kilichonishangaza na kuniacha na maswali mengi, kila mtu aliyekuwa akifika pale mbele kwa yule babu aliyekuwa akigawa nyama, akikabidhiwa yake alikuwa akifurahi sana na kwenda kukaa pembeni na kuanza kuila bila wasiwasi wowote.
Nimewahi kusikia sana kuhusu stori za watu wanaokula nyama za watu lakini siku zote nilikuwa naona kama ni mambo ya kutunga, iweje mtu amle mwenzake? Ni hapo ndipo nilipoelewa kwamba kumbe siyo stori za kusadikika tu bali ni mambo ambayo yapo na yanafanyika kwa wingi.
Nilijiuliza sana, wale waliokuwa wakiliwa nyama ni akina nani? Walifanya makosa gani mpaka waliwe? Walikuwa wanaishi wapi na nyama zao zilifikishwaje pale? Je, walikuwa wanaume au wanawake, wakubwa au wadogo? Sikuwa na majibu.
Foleni ikawa ikazidi kusogea mbele, mwili wangu ulikuwa na maumivu sehemu mbalimbali, hasa yale maeneo ambayo yule babu alikuwa amenichanja lakini huwezi amini, kwa jinsi nilivyokuwa na hofu, wala sikuwa nasikia chochote.
Foleni iliendelea kusogea mbele, hofu ikazidi kunijaa lakini sikuwa na cha kufanya. Mara nilipata wazo, kwamba nikifika na kupewa nyama yangu, nijifanye naenda pembeni kuila lakini nikifika pembeni niitupe na tukirudi nyumbani, nitoroke na kurudi Chunya maana sikuwa tayari kwa kile kilichokuwa mbele yangu.
Ni kweli mara kadhaa nilijikuta nikitamani kuzijua mbinu mbalimbali za kichawi, kama kuweza kujilinda kwenye nyakati za hatari au kumuadhibu anayekuudhi lakini sikuwa tayari kuona nakuwa sehemu ya jamii hiyo iliyokuwa na mambo ya kutisha kiasi hicho.
Hatimaye zamu yangu iliwadia, yule mzee mgawaji, huku akijitafuna na damudamu zikiwa zimelowanisha mdomo wake, alinitazama usoni huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Kuna kipande alikuwa amekishika mkononi lakini alipoona ni mimi, nilimuona akikirudisha pale chini palipokuwa na nyama nyingine nyingi, zikiwa zimewekwa juu ya majani ya migomba, akachaguachagua na muda mfupi baadaye, aliibuka na mnofu mkubwa wenye damudamu, akanipa huku akiinamisha kichwa kama ishara ya heshima.
Huku nikitetemeka nilipokea, macho yangu yakiwa hayatulii, nilikuwa nikilichunguza kwa umakini lile rundo la nyama pale chini ambalo sasa lilikuwa limepungua sana. Nilichokiona awali ndicho nilichokiona tena, kulikuwa na miguu iliyokatwa, viganja vya mikono na viungo vingine vya mwili.
Nikiri kwamba moyo wangu haujawahi kupatwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kilichonitisha zaidi, ni pale nilipogundua kwamba katika rundo lile, kulikuwa na miguu na mikono ya watoto wadogo kabisa. Maskini... hawakuwa na hatia yoyote!
Baba naye alipewa kipande chake, akanishika mkono huku akiniongelesha kwa sauti ya chini. Aliniambia kwamba nina bahati sana kupewa heshima kubwa kama hiyo na mzee huyo ambaye baba aliniambia huwa wanamuita Mkuu kwa sababu ndiye kiongozi wao wa kanda. Akaniambia kwamba kitendo cha yeye kuinamisha kichwa chake tu, ilikuwa ni ishara kwamba amenikubali mno.
Hatukwenda mbali, tulikaa chini huku baba akinielekeza namna ya kukaa. Haukuwa ukaaji wa kawaida, mguu wa kushoto ulikuwa ukitangulia chini, kisha unakuja wa kulia halafu unakaa juu ya vifundo vya miguu yote miwili huku ukiwa umeikunja na kutengeneza alama ya V mbili.
Nilijaribu lakini miguu ikawa inaniuma sana, nilipowatazama watu wengine, wote walikuwa wamekaa kwa mtindo huo na wala hakukuwa na aliyekuwa akibabaika kama mimi, walikuwa wakiendelea kupiga stori za hapa na pale huku wakifurahia ‘kitoweo’, baba akaniambia atanifundisha taratibu.
Lile wazo langu la kwenda kuitupa ile nyama liliyeyuka kutokana na baba alivyonibana, ambapo muda mfupi baadaye, baba yake Rahma naye alikuja na kuungana na sisi pamoja na wanaume wengine watatu ambao sikuwa nawafahamu.
Kwa muda wote huo nilikuwa nikizugazuga tu kwani kiukweli sikuwa tayari kuila ile nyama ambayo ilikuwa ikichuruzika damu, mara kwa mara nilikuwa nikiitazama kwa woga, nikitamani hata niirushe mbali na kupiga kelele kwa hofu lakini haikuwezekana.
“Kula, muda unaenda,” baba aliniambia kwa kunihimiza, wale watu wengine ambao sikuwa nawafahamu, wakawa wanamuuliza baba mimi ni nani.
“Ni mwanangu, hamuoni tunavyofanana,” aliwajibu na wote wakawa wanampongeza kwa hatua ya kunisajili rasmi, wakawa wananipongeza na mimi wakiniambia kwamba sitajuta kujiunga na jamii yao. Kwa kuwa wote sasa walikuwa wakinitazama huku wakiendelea kunisifia, ilibidi nijikaze kiume maana baba alikuwa akinitazama kwa jicho kama la kunidharau hivi au kuonesha kwamba zile sifa nilizokuwa napewa sistahili.
“Umekua sasa si ndiyo?” baba yake Rahma aliniambia huku akinipigapiga begani na mkono wake uliokuwa na damu, mdomoni akiendelea kujitafuna. Nadhani aliongea hivyo kama kunikumbusha kile tulichokuwa tukitofautiana mara kwa mara na baba, akidai kwamba mimi bado nina akili za kitoto.
“Ndiyo,” nilimjibu kwa msisitizo, nikafumba macho na kupeleka ule mnofu mdomoni, nikaziba pua ili nisisikie hata harufu nikaanza kutafuna huku nikijikaza kisawasawa, sikuwa nataka kuonekana bado nina akili za kitoto kwa hiyo nilijikuta nikifanya kitu nisichopenda kukifanya ilimradi tu nimdhihirishie baba na baba yake Rahma kwamba sikuwa mtoto tena.
Mara kadhaa nilikuwa nikitaka kutapika lakini mwisho, hatimaye nilifanikiwa kuitia yote tumboni mwangu na kuufanya mwili wangu usisimke sana.
“Tafuna hii,” alisema baba yake Rahma huku akinipa vitu kama mizizi fulani hivi, nikavitafuna haraka na kuvimeza. Cha ajabu, mpaka muda huo, kumbe mimi ndiye niliyekuwa wa mwisho kumaliza ‘shea’ yangu, watu wote walikuwa wameshamaliza na sasa walikuwa wakipiga stori za hapa na pale.
“Vipi una swali lolote kwa kijana?” baba yake Rahma alimwambia baba kwa kejeli, nilishaelewa kwa nini amesema vile. Kwamba kwa sababu baba alikuwa ananiona kama nina akili za kitoto, je alikuwa na swali lingine lolote baada ya mimi kuonesha kile nilichokionesha pale mbele yao?
“Umenitoa aibu mwanangu, zawadi nitakayokupa hautakuja kuisahau maishani mwako,” aliniambia baba akionesha kuwa na furaha kubwa.
Mara sauti ya kama pembe la ng’ombe lililopulizwa kwa nguvu ilisikika, watu wote wakainuka walipokuwa wamekaa na kuanza kujipanga kwa mtindo wa duara kama ilivyokuwa mwanzo.
“Sasa hivi unaenda kukabidhiwa rasmi nguvu za giza ili uwe kama sisi, naomba ujasiri uliouonesha kwenye kula uuoneshe hapa pia, nenda pale ulipokuwa umekaa mwanzo,” baba aliniambia huku akinipigapiga begani kwa upole.
Kwa akili yangu nilijua kwamba tayari kazi imekwisha, kumbe kulikuwa na kazi nyingine, nikaanza kutetemeka tena huku nikigeuka huku na kule kuwatazama wale watu ambao wote walikuwa na nyuso za furaha. Nilipogeuka upande wa kushoto, nilimuona mtu aliyenifanya nishtuke mno, nilifikicha macho nikiwa ni kama siamini.
Je, nini kitafuatia?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom