Sehemu ya 32....
"Kumi na mbiliiiii.."
"HAHAHAHAHAA WANAWAKE NI WAUAJIIII"
Safari hii nae alicheka kwa nguvu zaidi na kuongea maneno yaliyosikiwa na kumstua Hussein babu bubu aliyekuwa upande wa pili wa seng'enge akiendelea kufyeka pasi kuwaangalia wale wafungwa wapya waliokuwa wanahesabiwa. Lakini maneno aliyoropoka yule mfungwa mpya namba kumi na mbili yalimfanya aache kila kitu na kusimama kumuangalia huyo mfungwa ni nani aliyenukuu maneno kama aliyokuwa anasema yeye. Akiwa anamtazama kwa udadisi na umakini mkubwa ndipo macho yake yalipokutana na yule kijana ambaye sasa kipigo cha mikanda kilimshukia kutoka kwa askari magereza kama bakshishi ya dharau aliyoonesha kukaidi kutaja jina lake.
Naam, huyo hakuwa mwengine bali ni kijana aliyetumwa kazi na mkuu wa majeshi. Komandoo Jumanne au CJ4 kwa jina maalum la utambulisho wa kijeshi kwenye mchoro wa bawa alilochorwa kifuani. CJ4 alifikishwa hapo kwa kazi maalum ambayo hakuna askari yeyote wa ziada aliyejua zaidi ya mkuu msaidizi wa gereza.
Hussein bubu aliendelea kumshangaa yule kijana alivyokuwa anaadhibiwa kwa kukaidi kutaja jina lake na kung'ang'ana kusema kuwa 'wanawake ni wauaji'. Kipindi mikanda ikiendelea kumparamia mwilini ndipo agizo kutoka kwa mkuu msaidizi wa gereza lilipotolewa kuwa wamuache. Ndipo alipoachwa na kujumuishwa na wafungwa wenzake kabla ya kupewa sare zao na kuchanganywa na wenzao ndani ya lile gereza gumu lenye ulinzi mkali.
Muda wote CJ4 alikuwa kimya. Alionekana mtu wa mawazo sana hata ilipokatika wiki akiwa ndani ya gereza hakuwahi kusema na yeyote. Walipokuwa wanatolewa na kupelekwa kwenye kazi za kuvunja kokoto alifanya kazi kwa nguvu na kwa hasira bila kusema na mtu. Hussein bubu akiwa kwenye kitengo cha kusambaza maji ya kunywa kwa wafungwa wenzake nafasi aliyopewa kipindi cha kamishna Shebby, aliendelea kumchunguza kwa makini mfungwa yule mpya akitamani kujua naye kulikoni nyuma ya kifungo chake.
Alijikuta Hussein bubu mwenyewe akiweka ukaribu na CJ4 huku akiamini kuwa yule ni mtu pekee anayeweza kukaa naye akihisi huenda yaliyomkuta ni makubwa kama yaliyomkuta yeye.
Hussein hakujua kichwani mwa Cj4 kama alikuwa na nia moja tu ya kutimiza kazi aliyopewa na mkuu wa majeshi iliyotoka kwa Amiri jeshi Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Sifuri tayari sasa ni moja." Alisema kichwani mwake CJ4 baada ya kufanikisha kumuweka karibu Hussein bubu pasipo kutumia nguvu wala kumuomba. Mbinu aliytumia kumuweka karibu Hussein ilifanikiwa. Hiyo ndiyo ilikuwa nia yake CJ4 ili kujua yaliyojificha nyuma ya safari ya kamishna Shebby baada ya kupewa muongozo kabla hajafika pale gerezani. Hussein ndiye aliyeanza kufunguka kumpekua Cj4 kwa maswali ya hapa na pale ili kujua kilichompata. Japo awali Cj4 alitia ngumu kusema naye akijifanya hataki ukaribu na Hussein lakini baada ya wiki mbili aliamua kuwa mpole baada ya kumjaza kiu zaidi na imani juu yake Hussein bubu ili asijue kama yupo pale kipelelezi.
Siku moja mchana kipindi cha mapumziko wakati wa chakula walikaa pamoja Cj4 na Hussein bubu. Hapo ndipo alianza kumsimulia Hussein mkasa wake mpaka kufika gerezani. Ilikuwa ndio mara ya kwanza kuzungumza naye kwa mapana toka aingie gerezani. Ingawa mkasa wake ulikuwa wa uongo lakini uliomhuzunisha sana Hussein na kujikuta naye anamsimulia mkasa wake mpaka anazeekea jela.
"Usiumie sana mwanangu! yaliyokukuta yanawakuta wanaume wengi sana juu ya hawa wanawake. Pole sana hata mimi nilikuwa kama wewe siku za nyuma na niliishi maisha kama yako kwa zaidi ya miaka 20 humu gerezani. Laiti isingekuwa mkuu mpya wa gereza ambaye alipata matatizo miezi michache nyuma, basi pengine mpaka sasa ningelikuwa kama awali... Daaa!" Alisema kwa huzuni Hussein bubu na kumsimulia mkasa mzima CJ4. Mkasa ambao ndio aliutaka kuujua pasipo Hussein kubaini. Alipomaliza kusimulia Hussein CJ4 alijikuta akilaani yaliyomkuta na kumpa pole pia.
"Hakika kama ulivyoonewa wewe nami nimeonewa pia na sitamani kufia humu gerezani ikiwa sijafanya lolote baya dhidi ya yeyote." Alilalama CJ4 na kuendelea
"Laiti kungekuwa na askari muelewa na mwenye roho nzuri nadhani angesikia kilio changu na kunisaidia lakini daaah!! nawachukia sana hawa askari wetu wooote wapuuzi na makatili tu"
"Mh! pole mwanangu lakini kumbuka si askari wote wabaya. Hata mimi awali niliamini hivyo lakini sasa imani hiyo sina tena." Alisema Hussein bubu.
"Hapana mzee we kufungwa kote huku na kuteseka kwa kesi usiyoitenda hadi unafikia umri huo mbona hajatokea hata askari mmoja kujipendekeza hata ki-uongo na kweli kukuonea huruma ama kukusaidia kivyovyote? Hawa wanyama tu usiwaamini mzee wanapelekwa pelekwa tu." Alizidi kukazia msimamo Cj4 kumchota akili Hussein bubu. Kila alichokifanya na kukisema CJ4 kilikuwa ndani ya mbinu maalum za kumfanya Hussein aseme kile alichotaka kukijua toka kwake pasipo kumuuliza. Na ndipo Hussein ili atetee vyema hoja yake na aaminike na Cj4 alijikuta akifunguka zaidi siri ya urafiki wake na Kamishna Shebby ambayo ndiyo hasa aliitaka kuijua CJ4.
"Sikia nikwambie mwanangu. Mi mwenyewe awali niliamini hivyo na nilikaa kimya zaidi ya miaka ishirini lakini baadae alitokea askari ambaye sikuwahi kuwaza hapo awali kama anaweza kuwepo askari mwenye roho ya imani tena mkubwa kama huyo. Alinihurumia na kufanya kila jitihada za kunisaidia baada ya kunishawishi mpaka nikamuhadithia yaliyonikuta na kujiapiza kuutafuta ukweli wa kesi yangu japo ni ya miaka mingi sana. Aaah! usihofu mwanangu wewe kesi yako bado changa sana usijikatie tamaa hivyo naamini kama yule kijana asingepatwa matatizo na angekuwepo nadhani toka siku ile ya kwanza unaingizwa hapa angeshakwita kutaka kujua kilichokusibu na ungestaajabu mwenyewe."
"Mh! siamini mzee kama kuna mtu kama huyo... yaani atake kukusaidia juu ya kesi yako ya miaka mingi? angeanzia wapi?"
"Aaagh! baba inabidi uamini tu kwani hiki nikuambiacho si ndoto."
"Mh! basi huenda atakuwa alikuongopea tu! kwa kuwa wewe upo ndani usingejua chochote anachokifanya nje ya gereza."
"Naamini asilimia zote hakuwahi kuniongopea. Nina hakika na hilo kutokana na matatizo yaliyompata ambayo yamesababisha asiwepo hapa leo hii yote kwa sababu yangu."
Aliropoka zaidi Hussein na kuitupa sahani ya chakula na kusogea pembeni huku machozi yakianza kumtoka baada ya kujitonesha kidonda chake makusudi na kuanza kumkumbuka Kamishna Shebby ambaye mpaka muda huo hakujua anaendeleaje japo alijua kuwa alinusurika kwenye shambulizi Mkuyuni.
CJ4 alimfata pembeni huku akiwa anazidi kumpekua Hussein kiakili atakavyo na kuelewa kila kitu alichoahidi kukifanya kamishna Shebby na kilichokuwa kinatokea nyuma kila alipokuwa anafatilia kwa kuwa alimjuza Hussein kila aliporudi gerezani.
Ingawa Hussein alijitahidi kumficha jina na kuficha mahala palipotokea matukio ya huyo askari aliyekuwa anamzungumza bila kujua anayemuhadithia anajua kila kitu.
"Basi mzee achana nayo kama Mungu katupangia tufie huku tutafia huku lakini kama sivyo siko tayari kufia gerezani. Nitatoroka tu kama sheria isipoona kama sina hatia." Alisema CJ4 huku akimfariji Hussein bubu.
*****
Upande wa pili ukaribu wa Dokta Asha na Kamishna Shebby ulianza kuwavuta katika hisia moja mioyoni mwao japo kila mmoja alimficha mwenzake.
Hata mzee Mwinchande na mkewe walibaini kitu hiko na walitamani mtoto wao amuoe yule doktari. Dokta Asha alizidi kumuhudumia Kamishna Shebby kwa upendo na ilikuwa kawaida halali mpaka muda Shebby amelala. Pia kabla Shebby hajaamka yeye alikuwa tayari yuko macho. Yaani kwa jinsi dokta Asha alivyojituma kumuhudumia Shebby hadi mzee Mwinchande akaona kile kiasi anachomlipa hakitoshi japo ilikuwa ni zaidi ya milioni kumi kwa wiki.
Siku moja ambayo ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Kamishna Shebby ambayo wakialikwa watu wachache katika hoteli maaalum waliyoikodi. Kipindi hiko ingawa kumbukumbu bado zilimsaliti kichwani lakini tayari Shebby aliweza kumudu kutembea pasipo msaada wa magongo. Dokta Asha alimuongoza Shebby katika kila hatua wakati tafrija ilipokuwa inaendelea hadi wakati wa zoezi la kukata keki. Ki ukweli Asha na Kamishna Shaaban walipendezana sana hata wahudumu wa hoteli walijua kuwa ni wapenzi lakini haikuwa hivyo. Kabla Shebby hajamlisha yeyote keki mshereheshaji alimuomba azungumze chochote kuhusu siku yake ile ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake. Hapo ndipo taratibu baada ya kukamata kinasa sauti na kuangalia huku na huko Kamishna Shebby alianza kuzungumza huku waalikwa wakiwa wametulia wakimtazama na kumsikiliza kwa umakini.
"Kwa kweli kikubwa namshukuru sana Mungu kwa kunifikisha umri huu. Japo bado naumia moyoni mwangu kwa kushindwa kukumbuka yaliyonikuta hadi muda huu ila napenda nichukue nafasi hii kumshukuru sana tabibu wangu aliyejitoa kwa hali na mali kuhakikisha nakuwa mzima na kutembea kama zamani. Ila ningependa pia nimwambie kitu kilicho moyoni mwangu na kila mtu nataka asikie ili nimuaminishe na nimuhakikishie kuwa hiki ninachoongea kinatoka kweli moyoni mwangu na si vinginevyo..." Alipofika hapa Shebby alinyamaza kidogo na kumtazama dk Asha aliyeonesha aliyemkodolea kwa shauku kubwa ya kusikia hiko kitu alichotaka kusema. Aligeuza shingo kuwatazama wazazi wake na waalikwa kisha akaendelea mwanaume kubonga mbele ya kidamnasi.
"Dokta Asha.. Dokta Asha hakika nakupenda sana. Naomba ukubali niwe wako ili tuunganike na kuwa mwili mmoja kama Mungu alivyoagiza wanadamu wenye jinsia tofauti tuishi duniani. Nahitaji uwe mke halali siku za usoni ili tuzidi kutengeneza ukaribu na kuzalisha familia bora pamoja. Naomba unikubali Asha na kama utanikataa naomba uthibitishe mbele ya wote wanaonisikia sasa hivi humu ndani. Kwanini niutese moyo wangu kwa kuficha ukweli halisi uliomo? Nakupenda sana dokta Asha nikubali tafadhali..!"
Maneno ya Shebby yalimstua kila mtu aliyekuwa ukumbini na kufanya watu wote wamgeukie Dokta Asha ambae alijikuta anainamia chini kwa aibu na mshangao. Hakuamini wala kufikiri kama kweli mgonjwa wake angekuwa na ujasiri mkubwa kiasi kile kumtongoza mbele za watu tena kwa kipaza sauti japo hata yeye mwenyewe alishaanza kuwa na hisia nae. Kila mtu alitamani kumsikia Dokta Asha nini atasema baada ya Shebby kutumbua ukweli wa moyo wake na kuuweka hadharani.
..........