Prof Safari ataka CCM iweke bayana sera ya ufisadi
Na Waandishi Wetu
MTAALAMU wa masuala ya sheria na wakili wa kujitegemea, Profesa Abdallah Safari ameitaka CCM iweke bayana kuwa ina sera ya ufisadi baada ya chama hicho tawala kuweka mikakati ya kumdhibiti Spika Samuel Sitta ili asiruhusu mijadala inayoikosoa serikali.
Sitta, ambaye bunge lake limekuwa likiipeleka mchakamchaka serikali kiasi cha kusababisha Edward Lowassa ajiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu, aliwekwa kiti moto na kikao cha Halmashauri Kuu kwa madai ya kuruhusu mijadala inayokichafua chama na serikali na kupendelea kikundi cha wabunge wanaoshambulia baadhi ya wanachama wa CCM.
Habari zinadai kuwa wajumbe wa Nec walitaka spika arejeshe kadi ya CCM, lakini baada ya kuongea na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete Sitta alilazimika kuomba radhi.
Akizungumza na Mwananchi jana, Prof Safari alisema chama hicho sasa kinapaswa kutangaza hadharani kwamba falsafa yake ni kutetea mafisadi.
Prof Safari alisema uamuzi huo wa kikao cha juu kabisa cha chama hicho, umeonyesha kuwa ndani ya CCM hakuna kiongozi msafi, wote ni mafisadi isipokuwa wanazidiana viwango.
Naye mhadhiri mwandamizi, Idara ya Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema hatua iliyofikiwa na CCM ni matokeo ya kuwepo kwa makundi ndani ya chama hicho.
"Udhibiti ndani ya chama ni jambo la muhimu, lakini pia usikivu wa chama kwenye hoja za msingi ni muhimu zaidi…iweje mtu aliyepigiwa kura na CCM wenyewe kuwa spika, leo awe amegeukwa," alihoji Bashiru.
Profesa Issa Shivji alisema kuwa kitendo cha kutaka kumpokonya spika kadi ya uanachama ambacho kingesababisha apoteze ubunge na kuvuliwa nafasi hiyo ya kuongoza moja ya mihimili mikuu mitatu ya serikali, si sahihi kwa sababu kingeweza kusababisha mgongano ndani ya chama, hivyo wajumbe wa NEC walipaswa kuangalia adhabu nyingine.
Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahimu Lipumba alimponda Spika Sitta kwa kitendo kilichoripotiwa kuwa cha kuomba radhi kwa wajumbe wa Nec, akida kimedhihirisha kuwa spika ni kiongozi laini na dhaifu.
Prof Lipumba alisema kama Sitta ni kiongozi jasiri kwa Watanzania angesimamia haki ambayo anaifanya katika kusimamia bunge.
Alisema kwa vile Sitta alikuwa anapambana na ufisadi na kuwapatia fursa wabunge kufichua ufisadi uliokuwa unafanywa na baadhi ya viongozi wa serikali na wa CCM, basi angetetea utendaji wake.
"Kama Sitta angekuwa madhubuti na jasiri angekubali kuadhibiwa na baadaye akalishitaki hilo kwa wananchi kwa kuwa alichokuwa anakifanya ni cha haki," alisema Lipumba na kuongeza spika alishindwa kusimamia haki.
Alisema hilo linadhibitisha wazi kuwa CCM haina nia na uwezo wa kupambana na ufisadi.
"Hii ni aibu kwa CCM; badala ya kupambana na ufisadi na mafisadi, sasa wameamua kupambana na kuwapiga vita wenzao wanaopambana na ufisadi," alisema Lipumba. Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Claud Mshana, Sadick Mtulya, James Magai na Salim Said