Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Bw. Edward Lowassa, ametetewa na wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).
Habari za ndani ya kikao hicho kilichojadili juzi pamoja na mambo mengine uhusika wa Bw. Lowassa katika sakata la mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Richmond, zilisema baada ya Bw. Lowassa kujieleza wajumbe waliuona ukweli na kubaini kuwa uhusika na Richmond si wa moja kwa moja.
"Sisi tunaamini kuna vikundi ndani ya CCM ndivyo vinavyoshinikiza hali hii itokee ili Bw. Lowassa aonekane mbaya mbele ya jamii, lakini tulifikia muafaka kuwa alijiuzulu si kwa kuhusika moja kwa moja na Richmond, bali aliwajibika ili kukiokoa chama kwa wadhifa wake," kilisema chanzo chetu cha habari.
Chanzo hicho kilisema kilichojitokeza ni kuwa Bw. Lowassa alionewa katika sakata hilo na kwamba la muhimu ilikuwa ni kuwasilisha ushahidi muhimu, kama upo, katika kujihusisha moja kwa moja na Richmond.
"Hata Mwenyekiti wa Kamati teule ya Bunge, Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa anahitimisha hoja yake, alisema Kamati haikubaini kuwa Bw. Lowassa alihusika moja kwa moja mbali ya kuwajibika kama Waziri Mkuu," kilisema chanzo hicho ndani ya NEC.
Mmoja wa wanachama wakongwe na kada wa siku nyingi wa CCM ambaye pia ni mjumbe wa kikao hicho, alisema maelezo yaliyotolewa na Bw. Lowassa katika NEC juzi, yalitosha kumwondoa katika kashfa ya moja kwa moja ya Richmond.
Habari zaidi zilisema wajumbe hao wa NEC walikubaliana kutoendeleza hoja hiyo na kutaka Serikali iachiwe majukumu yake na badala yake CCM ijiimarishe na iendelee kutekeleza ilani yake ya uchaguzi kwa maslahi ya wananchi.
Kauli ya wajumbe hawa ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini kutokana na sababu za kisiasa, zilikuja kutokana na mgawanyiko ambao awali ulishajitokeza ndani ya NEC.
Mgawanyiko huo ulitokana na baadhi yao kutaka waliotuhumiwa kwa ufisadi wachukuliwe hatua za kichama ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nyadhifa zao ndani ya chama; lakini kutokana na mjadala mkali, ikabainika kuwa papara zinaweza kukiathiri chama hicho na kusababisha mgawanyiko mkubwa.