Muhtasari wa alichosema kocha Arne Slot baada ya mechi ya Community Shield kati ya Liverpool na Crystal Palace:
Kuhusu "tatizo kuu" kwa Liverpool katika mechi hiyo...
Slot alisema:
"Hakukuwa na tatizo kuu moja, isipokuwa kama timu pinzani inapoteza penati mbili halafu bado unashindwa baada ya penati tano, hilo halisaidii. Kwa mtazamo wangu, tulikuwa mbele kwa mabao mara mbili na tulikuwa tunadhibiti mchezo vizuri hadi waliposawazisha 2-2. Tulikuwa na nafasi kubwa kwa Mo Salah lakini pia tulikuwa karibu kupoteza mchezo. Kabla ya bao la pili la Palace, nilikuwa na kila sababu ya kuamini tungeweza kushinda."
Kuhusu kujifunza chochote kutoka kwenye mechi licha ya kupoteza...*
Slot alieleza kuwa:
"Si jambo jipya. Katika maandalizi ya msimu huu, tumeona timu ikiwa bora zaidi kushambulia, tunauweka mpira vizuri zaidi, tunatengeneza nafasi nyingi zaidi na tunatawala mchezo vizuri. Tofauti na msimu uliopita ambapo tulikuwa na umiliki mwingi wa mpira lakini hatukuwa na nafasi nyingi za uhakika."
Hata hivyo, aliongeza: "Tumekuwa tukiruhusu mabao mengi tuliruhusu manne dhidi ya Milan, moja dhidi ya timu ya Japan, mawili dhidi ya Bilbao na tena mawili leo. Msimu uliopita tulishinda mechi nyingi kwa bao moja tu, hasa kwa sababu tulikuwa tunalinda vizuri. Leo tumefunga mara mbili dhidi ya Palace, jambo ambalo hatukuweza msimu uliopita—tulishinda 1-0 na kutoka sare 1-1."
Hitimisho:
Kuna mafanikio upande wa mashambulizi, lakini Arne Slot alisisitiza umuhimu wa kuboresha safu ya ulinzi ili kurejesha uthabiti wa timu kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Kuhusu ujumbe wake kwa wachezaji kati ya muda wa kawaida na mikwaju ya penati…*
Slot alisema:
"Hakukuwa na ujumbe mkubwa. Ilikuwa ni kuhakikisha kila mmoja anatulia na hajachanganyikiwa, ili aweze kupiga penati yake vizuri. Ilikuwa wazi kabisa ni akina nani watano watakaopiga penati, kilichobaki ilikuwa ni kupanga tu mfuatano wao na hivyo ndivyo tulivyofanya. Halafu ni juu ya wachezaji kujielekeza kwa kila penati, na walifanya hivyo. Ilikuwa wazi tangu mwanzo nani atapiga, hakuna mtu aliyekuwa na mashaka, ingawa haikusaidia kufunga zote tano."
Kuhusu jinsi Liverpool inaweza kupata uwiano sahihi kati ya kutengeneza nafasi na kuwa imara katika ulinzi…*
Alijibu:
"Tumebadilisha wachezaji wanne, na mara nyingine inahitajika muda kuzoeana katika mashambulizi au ulinzi. Lakini dhidi ya Bilbao hatukuruhusu nafasi nyingi kabisa labda moja lakini tulifungwa mabao mawili kwa mipira ya kutengwa, ambayo nayo ni sehemu muhimu ya mchezo. Sio kwa mashambulizi ya moja kwa moja. Leo pia sikuhisi tumetoa nafasi nyingi, lakini tulifungwa magoli mawili. Nafasi yao kubwa ya kwanza ilisababisha penati, na ile ya pili ilikuwa dakika ya 78."
Slot aliongeza: "Kwa ujumla hawakuwa na nafasi nyingi kwa sababu walirudi nyuma (low block) na sisi tulikuwa na umiliki mkubwa wa mpira. Lakini baada ya 2-2 wao walitengeneza nafasi. Hivyo, bado tunahitaji marekebisho kidogo upande wa ulinzi kwa sababu haturuhusu nafasi nyingi, lakini bado tunafungwa mabao.
Kuhusu kiwango cha Ekitike na athari ya bao lake kwa maendeleo yake ya baadaye…*
“Nadhani ni jambo zuri kila mara kufunga bao si kwa Ekitike tu, bali pia kwa Jeremie Frimpong hasa unapokuwa unaanza maisha kwenye klabu mpya. Lakini ingekuwa bora zaidi kama tungeweza kushinda mechi, kwa sababu hilo ndilo jambo muhimu zaidi kuliko kufunga goli.
Ameonyesha mchango mzuri, lakini pia ni mfano wa mchezaji aliyejiunga nasi wiki moja na nusu au mbili zilizopita, mwishoni mwa ziara yetu ya Asia. Kwa hiyo kwangu mimi, akiwa na siku tatu au nne tu kabla ya mechi ya Ijumaa, haingekuwa busara kumchezesha dakika 90, kwa sababu… tunaye Federico [Chiesa], lakini naye hakushiriki ziara ya Asia, kwa hiyo hatuna mbadala wengi.
Kama Ekitike angepata majeraha kipindi hiki, ingekuwa hatari kubwa kuelekea mechi dhidi ya Bournemouth, Newcastle na Arsenal. Ndiyo maana nilimtoa uwanjani, lakini kwa kweli leo amecheza vizuri sana.”