MAKALA YA TETESI ZA LIVERPOOL: WIKI ILIYOANZA JUMATATU
Wiki hii imeshuhudia upepo wa mabadiliko ukivuma kwa kasi kule Anfield – kuanzia mikakati ya usajili wa mastaa wapya hadi mashambulizi ya vilabu vingine kwa wachezaji wao muhimu. Haya hapa matukio moto moto yanayohusu Liverpool:
1. Florian Wirtz: Liverpool wapiga hodi rasmi kwa mfalme wa Leverkusen!
Liverpool wameongeza kasi ya kumwania kiungo fundi Florian Wirtz, huku presha yao ikitishia ndoto za Bayern Munich.
Familia ya Wirtz imeripotiwa kuvutiwa na ofa ya Liverpool, na mchezaji huyo anatarajiwa kufanya uamuzi ndani ya siku 10.
Michael Edwards tayari amewasiliana rasmi na Leverkusen na kupata ridhaa ya kukutana na familia ya Wirtz – na safari ikapangwa mara moja!
2. Milos Kerkez: Mradi wa beki wa kushoto waanza rasmi
Kerkez sasa ndiye kipaumbele cha Liverpool kwa nafasi ya beki wa kushoto. Uchambuzi wa kina umefanyika na mchezaji yuko tayari kwa uhamisho majira ya joto. Liverpool wako na matumaini – dili lipo mezani
3. Alexis Mac Allister: Madrid wanatamani lakini wanashtukia ugumu
Real Madrid wameonyesha mapenzi makubwa kwa Mac Allister, lakini uhamisho wake kwenda Bernabeu si rahisi. Liverpool wamekaa mkao wa kula – hawataki kumpoteza fundi wao wa kiungo.
4. Rayan Cherki: Kipaji cha muda mrefu chasubiri foleni
Ingawa Liverpool wamekuwa wakimfuatilia Cherki kwa muda mrefu, kwa sasa hana nafasi ya juu kwenye orodha ya vipaumbele. Florian Wirtz ndiye anayebebwa juu kwa sasa.
5. Darwin Núñez: Atletico wanapiga simu, Darwin anasema ‘poa’
Atletico Madrid wamemvutia Darwin Núñez na tayari wamewasiliana naye – na kwa mujibu wa vyanzo, ametoa ‘green light’. Kinachosubiriwa sasa ni makubaliano ya vilabu viwili.
Kwa upande mwingine, Liverpool wameanza kumchunguza Joao Pedro wa Brighton kama mrithi anayefaa endapo Darwin ataondoka.
6. Hugo Ekitike: Liverpool waingia mezani
Liverpool wamekuwa miongoni mwa vilabu vilivyowasiliana na Eintracht Frankfurt kuhusu kinda mwenye kipaji, Hugo Ekitike (miaka 22). Kwenye soko la washambuliaji, Liverpool wanacheza karata nyingi.
7. Ibrahima Konaté: Mikataba mipya yajongea
Mazungumzo mapya yamefanyika kati ya wakala wa Konaté na mkurugenzi wa michezo Richard Hughes. Pande zote zinaonesha matumaini makubwa ya kufikia makubaliano mapya ndani ya wiki moja au mbili zijazo.
8. Wellity Lucky: Kinda mwenye ndoto za Anfield
Liverpool wametoa ofa ya mkataba mpya wa miaka 4 kwa beki chipukizi Wellity Lucky (miaka 19). Inaonesha wazi kuwa klabu inajipanga kwa mustakabali wa muda mrefu.
Kwa Muhtasari:
Liverpool wapo kwenye harakati kali – wanawinda, wanahifadhi, na wanajenga upya. Florian Wirtz, Kerkez, na Joao Pedro ni majina ya kuangaliwa, huku wakiwa makini kuwabakiza Konaté na Mac Allister. Wakati huo huo, ishara za kuondoka kwa Darwin Núñez nazo zimezidi kuwa dhahiri.