Yannick Carrasco (Atletico Madrid)
Kiwango cha Mbelgiji huyo kimekuwa kikikuwa siku hadi siku tangu alipoanza kucheza kwenye kikosi cha Atletico Madrid ya Diego Simeone.
Tangu msimu uliopita, Carrasco amekuwa sehemu muhimu kabisa ya kikosi cha Atletico akicheza mechi 53. Msimu huu amekumbana na balaa la kuumia goti Oktoba mwaka jana na baada ya hapo bado hajarudi katika ubora wake ule wa awali. Staa huyo ataipa Liverpool machaguo yote kwenye sehemu ya mbele, akicheza kushoto au kulia na wakati mwingine anaweza pia kucheza katikati jambo litakalomfanya Klopp kuingiza mtu muhimu kabisa kwenye kikosi chake.
Manuel Lanzini (West Ham)
Licha ya Wilfried Zaha na Riyad Mahrez ndiyo wanaonekana kuwa ni wachezaji bora zaidi kwenye Ligi Kuu England kwa wakali wasiokuwa wa timu za Top Six, lakini hakuna ubishi Lanzini ndiye mwenye kiwango kinachofanana na Coutinho. Staa huyo miguu yake imejaa ufundi mkubwa na hakika ni mchezaji anayevutia kumtazama wakati mpira unapokuwa kwenye miguu yake.
Ubora wa Lanzini unaonyesha ni mchezaji anayeweza kuboresha kiwango chake na kuwa msaada kama atakwenda kuichezea Liverpool.
Christian Pulisic (Borussia Dortmund)
Ni mmoja kati ya wachezaji wenye viwango bora kabisa barani Ulaya kwa sasa, akifunga mabao kama anavyopenda na kuwa mchezaji mwenye hadhi kubwa.
Liverpool ikipata huduma yake itakuwa imefanya kitu cha maana kwelikweli kwa sababu itavuna mengi mazuri kutoka kwake.
Klopp amekuwa akivutiwa sana na mchezaji huyo, lakini alichoambiwa na Borussia Dortmund, Pulisic hauzwi.
Lakini kwa sababu mambo yanaweza kuwa tofauti, kama Liverpool ikipata pesa za kumuuza Coutinho, basi haitakuwa na kisiki chochote mbele yake itakapohitaji mchezaji, pesa itakuwa inaongea.
Nabil Fekir (Lyon)
Chaguo jingine ambalo Klopp anaweza kulifanya katika kuziba pengo la Coutinho ni kumsajili Fekir.
Kiwango cha staa huyo kipo wazi kiasi cha kuivutia hadi Real Madrid ya Zinedine Zidane. Takwimu za Fekir zinavutia kwelikweli, amefunga mabao 13 katika mechi 16 za Ligi Kuu alizocheza msimu huu.
Fekir amefunga mara mbili pia kwenye Europa League na moja ya mabao yake aliifunga Everton. Fekir atakuwa msaada mkubwa kwenye kikosi hicho kama Klopp atafanikiwa kuipata huduma yake.