Mchango wa Mheshimiwa Cheyo Bungeni
"Mheshimiwa Spika, la pili, upande wa watumishi. Mimi hapo nafikiri tumekosea kwa muda mrefu tangu tumeanza. Labda kwa ushauri wa Wafadhili wetu, kitu ambacho kinaitwa Manpower Reform katika nchi yetu, tumepoteza taswira au mtazamo wa mtumishi wa Umma. Zamani na mimi nakumbuka nilipokuwa kijana, mtu alikuwa akiingia Serikalini kuwa mtumishi kwa sababu alikuwa na uhakika kwamba, kwanza atakuwa ni permanent employee, atakuwa na kazi ambayo ni ya kudumu, hata kama ni mshahara ni mdogo, lakini ana uhakika kwamba atakuwa na ajira.
Mheshimiwa Spika, la pili, alikuwa anaingia mle akijua kwamba kuwa mtumishi wa Serikali ni career, yaani ni utumishi unaodumu tangu labda una miaka 18, kuna watu wengine wameingia kutoka Shule tu na wameendelea wamekuwa Ma-Commissioner ndani ya Serikali. Anajua kwamba akishafika hapa, atafundishwa ndani ya Serikali, atapata promotion ndani ya Serikali, ataendelea na mpaka mwisho anaweza akastaafu na hali yake ikiwa nzuri. Huu ndio ulikuwa mtazamo wa watu wengi hapo zamani.
Mheshimiwa Spika, lakini, leo hakuna mtu ambaye anaweza sasa hivi akajivunia kuomba kazi ya Serikali. Hana uhakika kama mtumishi wa kudumu, kama ni mtumishi labda wa muda, kama ni mtumishi ambaye leo ataambiwa kazi yako imekwisha au anakuwa ni mtumishi ambaye ni wa Contract. Kwa hiyo, ni shaghala baghala tu, mambo yote yameharibika.
Mheshimiwa Spika, mimi nashauri tungerudi tena kule ambako tulipoteza njia. Kweli tuanze kuwandaa hao vijana wanaoingia Civil Service na wanabaki kuwa Civil Servants na wanafundishwa maadili ya ki-Civil Servant. Leo hii, hujui nani ni mwanasiasa, hujui nani ni Civil Servant. Siku moja mimi nilipokuwa napeleka Form yangu pale Bariadi nikigombea Ubunge, napeleka ile Form, mtu anasema, aha! Unajua na mimi nilikuwa nataka kugombea sijui Jimbo la x, y, z. Nikasema, wewe! Akasema ndiyo! Wewe ni Chama gani? CCM! Sasa wewe ni mtumishi wa Umma au wewe ni mwanasiasa?
Mheshimiwa Spika, hali hii kusema kweli inaleta wasiwasi hata namna ya watumishi hawa wa Umma kuweza kuwa watu ambao watafanya kazi bila upendeleo wa aina yoyote. Kwa hiyo, turudi kule.
Mimi nashauri kwamba, katika sehemu ya Utumishi wa Umma ambayo Wazungu wanasema kwamba ni Professional, kwa mfano Watumishi wa Umma - Mapolisi, hii ni taaluma. Kwa hiyo, wako Polisi na wanajua mtu wao ni IGP mpaka chini. Watumishi wa Umma - Jeshi, wanajua wana Kamanda wao tangu juu mpaka chini. Leo pia tungekwenda hata kwa Watumishi wa Afya, wajue kwamba Principal Sectretary Wizara ya Afya, ndiye Boss wao na akiingia kwenye Kituo cha Mafunzo kama Unesi au kama Daktari, mara moja anajua kwamba mimi nakwenda mkondo huu na kwamba Permanent Secretary Wizara ya Afya, yule ndiye atakuwa Mwajiri wangu.
"