Blaki Womani
JF-Expert Member
- Feb 28, 2011
- 11,229
- 13,431
Asante Sana. Naendelea kupata elimu zaidi.Mkuu zitto junior ili uweze kuelewa ni kwanini Nuhu alimlaani Caanan na siyo Ham aliyetenda kosa, kwanza unatakiwa ulielewa na kuliamini NENO la MUNGU. Ili ulielewe NENO la MUNGU, kwanza lazima uliamini. Binadamu hatuwezi kumwelewa MUNGU, lakini tunaweza kulielewa NENO lake ambalo ametupa ili litusaidie katika maisha ya sasa na yale yajayo.
Tatizo linakuja pale ambapo watu walio wengi hawataki kuielewa Biblia wala kuiamini, wengi wanaona kile kilichoandikwa kwenye Biblia ni kama hadithi tu, ni kama porojo tu ambazo hazina maana. Ukweli ni kwamba, Biblia ni zaidi ya hadithi, ni zaidi ya Historia, na ni zaidi ya Unabii ambao umekuwa ukitimia kila siku. Kwa kulitambua hili, mimi nitakupa majibu ya Kibiblia ni kwanini Nuhu alimlaani Caanani badala ya Ham. Majibu yote yapo ndani ya Biblia na nje ya Biblia huwezi kupata majibu.
Iko hivi; zamani zile Wazazi hasa baba walikuwa wanatoa baraka au laana kwa kizazi cha watoto wao na siyo kwa mtu mmoja peke yake. Kama ni baraka, baba alikuwa anatoa baraka hizi kwa watoto wake wa kiume na vizazi vyao vyote vinavyofuata kwa sababu walikuwa wanaamini kuwa kizazi hakiishii kwa watoto, bali kinaendelea na kuendelea. Pia huu ndiyo ulikuwa utaratibu waliojifunza kutoka kwa BWANA MUNGU, pale alipotoa laana ya kwanza kwa mwanadamu na nyoka;
"nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa na wewe utamponda kisigino". MWANZO 3:15
Hapo juu utaona hiyo laana siyo kwa Eva na nyoka peke yao, bali ni kwa uzao wao wote utakaotokea duniani. Hii inaonekana kuwa wazee wale wa kale walijifunza pia kutoa laana au baraka kwa kizazi na kizazi. Hebu tuone baraka ya Isaka kwa Yakobo.
"Mataifa na wakutumikie, na makabila wakusujudie. Uwe bwana wa ndugu zako, na wana wa mama yako na wakusujudie. Atakaye kulaani, alaaniwe na atakayekubariki, abarikiwe". MWANZO 27:29
Hapa pia utaona Yakobo anabarikiwa na baba yake, tena siyo baraka kwa ajili yake tu katika maisha yake yeye kama Yakobo, bali ni kwa ajili yake na uzao wake wote utakaofuatia baada yake. Hivi ndivyo ilivyokuwa, hivi ndivyo wanadamu walijifunza kutoa baraka kwa wana wao au laana. Pia unaweza ukasoma kitabu hicho cha MWANZO sura ya 49, na utaona jinsi ambavyo na yeye Yakobo alivyotoa baraka kwa watoto wake 12.
Tukirudi upande wa BWANA MUNGU, pia tutaona jinsi alivyombariki mzee Ibrahimu, hakumbariki yeye tu kwa wakati ule, bali alimbariki yeye na uzao wake wote utakaofuatia baadaye.
"Nami nitakufanya wewe kuwa Taifa kubwa na kukubariki, na kulikuza jina lako nawe uwe baraka. Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia zitabarikiwa". MWANZO 12:2-3
Mpaka hapa tutakuwa tumeona jinsi baraka na laana zilivyokuwa zinatolewa na inaonekana wazi kabisa namna ya kutoa baraka au laana, Wanadamu wa kale akiwemo mzee Nuhu walijifunza kutoka kwa MUNGU. Tukumbuke kuwa Nuhu alikuwa ni Nabii wa MUNGU, na aliongea na MUNGU mara nyingi tu katika njozi na maono. Hivyo basi Hamu alipokosea kwa kumwangalia baba yake akiwa uchi na kumcheka, alilaaniwa Caanani ambaye alikuwa ni uzao wa Hamu, yaani kizazi chote cha Hamu kikawa kimelaaniwa.
Huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa kutoa laana au baraka, tena ni utaratibu ambao ulikuwa na baraka zote toka kwa MUNGU. Caanan hakumcheka Nuhu, lakini alilaaniwa sababu yeye alikuwa ni uzao wa Hamu, Caanan alikuwa anabeba damu ya Hamu ndani yake na alipaswa kulaaniwa. Pia tukumbuke jinsi MUNGU alivyosema katika zile Amri kumi;
".........nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao na kuzishika amri zangu". KUTOKA 20:5-6
Nuhu hakukosea kumlaani Caanan, nasema hakukosea sababu Nuhu alifuata utaratibu uliokuwepo. Utaratibu ambao hata BWANA MUNGU aliutumia kwa mara ya kwanza pale Eva alipokula matunda ya mti aliokatazwa asile. Tukihoji kwanini Nuhu Nabii wa MUNGU alimlaani Caanan kwa makosa ya baba yake, itakuwa kama tunataka kuhoji pia ni kwanini sisi leo hii tunabeba laana ya Eva na Adamu wakati siyo sisi tuliokula tunda. Nafikiri hakuna mwanadamu anayeweza kusimama na kumuuliza MUNGU kwanini ulifanya hivyo, kwanini ulitulaani sisi? (Soma ISAYA 45:9 au WARUMI 9:14-21)
MUNGU hakosei na wala MUNGU hamuonei mtu wala kumpendelea mtu. Nuhu alikuwa ni Nabii wa MUNGU, hivyo basi laana ya Nuhu kwa Caanan ilipata baraka zote toka kwa MUNGU. Kama Nuhu angekuwa ametoa laana kwa uonevu bila kufuata utaratibu unaokubalika na MUNGU; basi MUNGU asingekubali Caanan alaanike, angeizuia hiyo laana isitokee.
Nina imani kwa maelezo hayo, utakuwa umeelewa ni kwanini Caanan alibeba laana ya baba yake, tena siyo Caanan tu, bali ni yeye na uzao wake wote uliofuatia. Hata sisi Waafrika tunabeba laana hiyo mpaka leo, lakini tukumbuke kwamba MUNGU aliyetupiga kwa laana, ndiye YEYE huyo huyo aliyetuletea UKOMBOZI kupitia kwa Mwanawe YESU KRISTO.
Mkuu zitto junior hatuwezi kumwelewa MUNGU hata siku moja, akili zake, wala mawazo yake, hayachunguziki na Mwanadamu wala Malaika. Lakini tunaweza kulielewa NENO lake, kuliamini na kumtii Yeye kama MUUMBA wetu."Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam Mimi ndiye, wala hapana MUNGU mwingine ila Mimi; naua Mimi, naponya Mimi, nimejeruhi tena nimeponya; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu". KUMBUKUMBU LA TORATI 32:39
Barikiwa