Kuwezesha Ufikiaji Stahiki wa Elimu ya Digitali Katika Taasisi za Elimu ni Utekelezaji wa Haki ya Msingi ya Watoto, Vijana

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
IMG_20220427_143111_411.png


Katika zama hizi za digitali, moja ya mambo yanayoibua mijadala sana ni pamoja na suala la ‘ujumuishaji wa digitali’ au mfumo jumuishi katika masuala ya kidigitali (digital inclusion).

Hii inatafsiriwa kama dhana inayoshughulikia masuala yanayohusiana na ujuzi wa kidigitali na ufikiaji wa teknolojia – yaani uwezo wa kufikia na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) bila kujali vipato, umri, au uwezo.

Kwa kuzingatia kiwango ambacho dunia yetu inategemea zana za kidigitali kwa ustawi, mikakati ya kuimarisha uhusishaji wa kidigitali inahitaji kuimarishwa. Hapa tunazungumzia kuhakikisha kuwa sera zinatii kanuni na viwango vya haki za binadamu.

Kuna haja ya kuhakikisha kuwa kila mtu anapata mtandao kwa bei nafuu, upatikanaji wa miundombinu ya TEHAMA kwa wote unaridhisha, na kuna ufahamu wa faida za kuwa mtandaoni.

Hali ilivyo sasa
Ripoti nyingi zinaonesha uwepo wa tatizo la kutojumuishwa kidigitali kwenye mifumo ya elimu, hususan katika nchi zinazoendelea. Lakini pia kutokana na umasikini, tatizo hilo linaanzia chini kabisa.

Kwa mfano, kwa upande wa ufikiaji wa intaneti, Shirika la Muungano wa Mawasiliano duniani (ITU) linasema inakadiriwa kuwa bilioni 2.2 - au theluthi mbili - ya watoto na vijana ulimwenguni kote hawana ufikiaji wa intaneti nyumbani. Watoto hawa kwa kiasi kikubwa wanaishi katika nchi zenye maendeleo duni ambapo mitandao ya simu ya 4G inashughulikia asilimia 40 pekee ya watu wote.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linasema katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 89 ya wanafunzi hawana kompyuta za nyumbani na 82% hawana ufikiaji wa mtandao.

Hali_ilivyo_Duniani,_Kusini_mwa_Jangwa_la_Sahara_Transparent.png

Zaidi ya hayo, wakati simu za mkononi zinaweza kuwawezesha wanafunzi kupata taarifa, kuunganishwa na walimu wao na wao kwa wao, wanafunzi wapatao milioni 56 wanaishi katika maeneo ambayo hayana na mitandao ya simu – hii ni karibu nusu ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Elimu ya digitali ni hitaji muhimu la mafanikio katika mazingira ya kisasa yanayoendeshwa na teknolojia. Kwa mujibu wa Population Pyramid (2018) katika mataifa ya Afrika ni asilimia 30 hadi 50 ya watu wako chini ya umri wa miaka 15. Hiyo ina maana sehemu kubwa ya wakazi wa Afrika wapo katika umri sahihi wa kupata ujuzi wa TEHAMA.

Hata hivyo, wanafunzi wanaotaka kupata ujuzi huo unaohitajika kwa kazi nyingi hawana njia nyingine ila kulazimika kulipia mafunzo ya ziada katika "shule za kompyuta" kwa wale wanaomudu gharama hizo. Hiki ni kikwazo kikubwa kwa wale ambao hawawezi kujikimu kimaisha.

Mafunzo na vifaa vinavyotolewa katika shule na vyuo vingi vya Afrika bado havijaweza kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia. Madarasa ya TEHAMA hayawatayarishi wahitimu vya kutosha kwa nafasi kama hizo.

Mara nyingi, ndani ya mfumo wa shule na vyuo hivyo hakuna vifaa kabisa (au visivyotosha) kwa ajili ya vijana kujifunza. Katika kuhitimu, wengi wa wanafunzi hao wanakuwa hawajawahi kutumia kabisa kompyuta.

Habari kuhusu mwalimu huko nchini Ghana aliyefundisha darasa la kompyuta kwenye ubao kwa sababu hakukuwa na kompyuta halisi za kutumia liliibua hisia mbalimbali duniani. Shule aliyokuwa akifundisha Mwalimu huyo, Owura Kwadwo haikuwa na kompyuta yoyote tangu 2011, licha ya hitaji la vijana kufaulu mtihani wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kama sehemu ya kuendelea na shule ya upili.

Kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali, nchi za Afrika zitahitaji watu wenye ujuzi wa teknolojia. Kwa kuzingatia hili, juhudi zozote za kukuza uwezo wa kuweka jamii ya Kiafrika katika mfumo wa kidijitali lazima iwe inayozingatia watu. Mbinu ya ukuzaji wa uwezo huo inapaswa kuruhusu ujenzi endelevu wa ujuzi unaohitajika kuishi na kustawi katika ulimwengu wa kidijitali wa kimataifa.

Ingawa ujumuishaji wa kidijitali sio silaha pekee katika vita dhidi ya umaskini na ukosefu wa usawa, imekuwa sehemu ya msingi ya kukuza ushirikishwaji wa kijamii. Kwa hivyo, ujumuishaji huu ni msingi wa dhamira ya dunia ya kutomwacha yeyote nyuma katika utekelezaji wa Ajenda ya 2030.

Kinachopaswa kufanyika
Mtazamo wa serikali na jamii nzima unahitajika ili kupata suluhisho la kuziba mgawanyiko wa kidijitali na kuhakikisha kuwa TEHAMA inanufaisha kila mtu na kushughulikia mahitaji ya walio hatarini zaidi katika jamii.

Serikali, taasisi za umma, jumuiya ya kimataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, sekta binafsi, wasomi, mashirika ya kiraia, wawakilishi na wanachama wa makundi yaliyotengwa na maskini, na mashirika ya uhisani na ya kidini n.k, wanahitaji kufanya kazi pamoja kila mmoja akileta mitazamo, utaalamu na uwezo wake mezani.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema kutochukua hatua stahiki sio tu kunatishia juhudi za kufikia Lengo la 4 la Maendeleo Endelevu (SDG's) - la kuhakikisha elimu bora iliyo jumuishi na yenye usawa - lakini pia ni kinyume na Mkataba kuhusu Haki za Mtoto na Maoni ya Jumla No. 25 kuhusu haki za watoto katika mazingira ya kidigitali.

Kwa kutambua umuhimu wa upatikanaji wa maana wa teknolojia ya kidigitali, ikiwa ni pamoja na katika mazingira ya kielimu, UNICEF inabainisha kwamba “ikiwa ujumuishaji wa kidigitali haupatikani, ukosefu wa usawa huenda ukaongezeka...”
 
Back
Top Bottom