Bila umeme kwenye shule za Serikali tutaendelea kubaki nyuma kidigitali

Bull Bucka

Member
Oct 5, 2023
34
46
Ujumuishaji wa kidigitali katika sekta ya elimu ni suala linalokubalika kuwa na umuhimu mkubwa katika kuleta mageuzi ya kielimu na kufanikisha maendeleo ya kitaifa. Hata hivyo, ni dhahiri kuwa mchakato huu utachukuwa muda mrefu kufikia mafanikio makubwa hapa nchini kwetu. Kuna changamoto kadhaa za muhimu ambazo zinahitaji kushughulikiwa kwa kina ili kuhakikisha teknolojia ya digitali inakuwa na athari chanya katika mfumo wa elimu nchini Tanzania.

Shule nyingi za serikali, ambazo ndizo zinazowahudumia idadi kubwa ya wanafunzi nchini, zinakumbwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme. Bila umeme, matumizi ya vifaa vya kidigitali yanakuwa hayawezekani kabisa. Hii inaweka pengo kubwa kati ya shule za serikali na zile za binafsi ambazo mara nyingi zina rasilimali za kutosha kwa ujumuishaji wa kidigitali.

Najua kuna wengi wetu tunawafahamu wanafunzi ambao walikutana na kompyuta kwa mara ya kwanza wakiwa chuo kikuu kwa sababu ya vikwazo vinavyoweza kupatiwa ufumbuzi katika elimu ya msingi na sekondari.

Teknolojia ya kidigitali ni sehemu muhimu ya elimu katika dunia wa leo. Wanafunzi wanahitaji kujifunza jinsi ya kutumia kompyuta, intaneti, na programu mbalimbali ili kuwa tayari kwa ajira/ajira binafsi.

Serikali inapaswa kuwekeza katika miundombinu ya umeme na vifaa vya kidigitali katika shule za serikali ili kuwezesha wanafunzi kupata elimu bora zaidi na kujifunza jinsi ya kutumia teknolojia mapema. Hii itawawezesha wanafunzi kuwa na ujuzi wa kidigitali mapema na kuwa tayari kwa changamoto za ulimwengu wa kisasa.

Lakini pia, walimu wengi bado wanategemea mbinu za kizamani kama vile kuhifadhi taarifa za wanafunzi kwenye mafaili ya karatasi. Kutoa mafunzo ya kutosha kwa walimu na kuwawekea mazingira ya kubadilika na kuendana na mazingira ya kidigitali ni jambo la lazima kwakweli.

Changamoto nyingine inayojitokeza ni pengo kubwa la upatikanaji wa teknolojia kati ya wanafunzi wa shule za vijijini na wale wa mijini. Wanafunzi wanaosoma katika mazingira ya vijijini wanapata fursa ndogo ya kujifunza na kutumia kompyuta na vifaa vya kidigitali pengine kwa sababu ya kutopatikana kwa umeme au kutokuwepo kabisa kwa vifaa hivyo. Hii inawaweka nyuma katika enzi hizi ambapo teknolojia na digitali ndizo mihimili ya dunia.

Teknolojia inaweza kutoa ufikiaji wa elimu bora zaidi na vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi. Pia, inaweza kusaidia kuongeza ubunifu kwa walimu na wanafunzi, kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo ya wanafunzi, na kuboresha upatikanaji wa rasilimali za kielimu.

Kupitia uwekezaji wa kutosha katika miundombinu, mafunzo kwa walimu, na kuhakikisha upatikanaji wa teknolojia kwa wanafunzi wote, tunaweza kufanikisha lengo la kuleta mapinduzi ya kidigitali katika elimu ya Tanzania na kuandaa vizazi vyetu kwa ulimwengu wa digitali na ubunifu.
 
Back
Top Bottom