The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,801
WATANZANIA NA TAARIFA ZA USALAMA WA KIDIGITALI banner.jpg


Tanzania, kama nchi nyingine nyingi duniani, inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa elimu ya usalama wa kidigitali miongoni mwa raia wake. Hali hii inamaanisha kuwa watu wengi nchini hawana uelewa wa kutosha juu ya jinsi ya kujilinda na kuhakikisha usalama wao katika ulimwengu wa kidigitali. Tatizo hili linaweza kuwa na athari kubwa kwa haki za binadamu.

Ukosefu wa elimu ya usalama wa kidigitali unawaweka watu katika hatari ya ukiukwaji wa haki zao za faragha. Watu wasioelimika katika masuala ya usalama wa kidigitali mara nyingi hujikuta wakitoa taarifa zao binafsi kwa urahisi bila kuzingatia hatari zinazoweza kutokea. Hii inawafanya kuwa target rahisi kwa wadukuzi na matapeli mtandaoni ambao wanaweza kutumia taarifa hizo kwa njia mbaya.

Pia, watu wasio na elimu ya ulinzi wa kidigitali wanakabiliwa na hatari ya kuathiriwa na vitisho vya mtandaoni. Kwa sababu hawana ufahamu wa kutosha juu ya aina za mashambulizi ya kidijitali, wanaweza kuwa wahanga wa ulaghai wa mtandaoni, kudukuliwa akaunti zao za mitandao ya kijamii au hata kuibiwa taarifa zao za kifedha. Hii inaweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha yao kifedha, na hata kisheria.

Kwa kuwa mawasiliano na biashara nyingi zimehamia katika mazingira ya kidigitali, watu ambao hawajui jinsi ya kujilinda wanaweza kukosa fursa za ajira au biashara mtandaoni. Pia, wanaweza kukosa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli ambazo zinaweza kuboresha maisha yao na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Tatizo ni kubwa Tanzania
Watu wasio na ufahamu wa kutosha juu ya masuala ya usalama wa kidijitali wanaweza kusita kutumia mitandao ya kijamii au kushiriki katika majukwaa ya kidigitali kwa hofu ya kushambuliwa.

Hata hivyo, katika ulimwengu wa kidijitali ambao tunaishi sasa, ambao ni matokeo ya maendeleo katika sayansi na teknolojia, usalama wa kidigitali ni muhimu katika kulinda haki mbalimbali za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya faragha, uhuru wa kujieleza, na haki ya usalama binafsi. Ni muhimu katika kulinda utambulisho wa mtandaoni, data, na mali zingine. Hii ni kwa mujibu wa Utafiti wa Haki za Binadamu wa LHRC wa mwaka 2022 uliojumuisha suala zima la usalama wa kidigitali.

Washiriki katika utafiti huo walipewa maswali kadhaa kuhusu usalama na uhakika wa kidijitali, haswa wale ambao wana vifaa vya kidigitali kama vile kompyuta za mezani, kompyuta ndogo, Vishkwambi (tablets), na simu za mkononi. Walihimizwa kutoa maoni yao kuhusu jinsi wanavyojisikia wameelimishwa vizuri kuhusu usalama wa kidigitali; ufahamu wao kuhusu sheria za usalama wa kidijitali; mashambulizi ya mtandaoni waliyoyapitia au kushuhudia; aina za kawaida za mashambulizi ya kidijitali; na matumizi na kugawana nywila (password).

WATANZANIA NA TAARIFA ZA USALAMA WA KIDIGITALI.jpg

Asilimia 83 ya waliojibu utafiti walisema wanatumia kati kifaa kimoja au viwili vya kidijitali, yaani simu za mkononi au kompyuta. Walipoulizwa jinsi walivyoelimishwa kuhusu usalama wa kidigitali, ni 15% tu ya washiriki waliosema walikuwa wameelimishwa vizuri sana au vizuri. Zaidi ya nusu yao (55%) walisema hawakuwa wameelimishwa au hawakujua kabisa kuhusu usalama wa kidigitali.

Mwiba kwa wanaoishi vijijini
Kwa sasa, kuna zaidi ya watumiaji milioni 30 wa mtandao nchini Tanzania, ambapo angalau 90% wanapata huduma ya mtandao kupitia simu zao za mkononi. Hii inamaanisha kuwa angalau nusu ya idadi ya watu wanatumia mtandao, hivyo kutumia vifaa vya kidigitali kama vile simu za mkononi na kompyuta.

Ufahamu mdogo kuhusu usalama wa kidigitali unawafanya Watanzania hawa kuwa hatarini zaidi kwa mashambulizi ya kidigitali na ukiukwaji wa haki za kidigitali na za binadamu. Mashambulizi haya ya kidigitali ni pamoja na mashambulizi ya programu hasidi, mashambulizi ya nywila, mashambulizi ya udukuzi wa taarifa binafsi, na wizi wa utambulisho.

Utafiti huo pia unaonesha kuwa ufahamu kuhusu usalama wa kidigitali ulionekana kuwa mdogo zaidi katika mikoa ya Mtwara, Njombe, Mara, Geita, Kigoma, Katavi, na Rukwa, ambapo 70% na zaidi ya washiriki walisema hawakuwa wameelimishwa/kutokuelimishwa kabisa. Idadi ya waliotaja kutokuelimishwa kuhusu usalama wa kidigitali pia ilikuwa kubwa zaidi katika maeneo ya vijijini (75%) ikilinganishwa na maeneo ya mijini (asilimia 35%).

“Ukiwachukua vijana 10 na kuwauliza kuhusu ufahamu wao kuhusu usalama na uhakika wa kidijitali, huenda ukapata ni 2 au 3 tu ambao wana ufahamu. Hii ni kutokana na ukosefu wa ufahamu wa umma kwa ujumla kuhusu masuala haya na kutokuwa na majadiliano ya kutosha kuhusu hayo katika mazingira yetu ya sasa,” alinukuliwa mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano mkoani Kigoma.

Mtaalamu mwingine wa Teknolojia ya Habari wilayani Chunya, mkoani Mbeya, amenukuliwa pia akisema, “Zaidi ya 40% ya raia katika Wilaya ya Chunya hawajali kuhusu usalama wa taarifa zao kwenye majukwaa ya mtandaoni, wakijitia hatarini kuwa waathirika wa mashambulizi ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na wizi wa kitambulisho.”

Wito wa LHRC
Katika ulimwengu wa leo, upatikanaji wa mtandao na matumizi ya majukwaa ya kidigitali yamekuwa ni mahitaji muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na utekelezaji wa haki za binadamu. Majukwaa hayo yanahitaji kuwa salama kwa kila mtu, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na ulinzi wa haki za binadamu za msingi, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza, uhuru kuepukana na ukatili, na haki ya uhuru na usalama binafsi.

LHRC inashauri Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na taasisi ya kitaifa za haki za binadamu, kuongeza programu za kukuza uelewa wa umma kuhusu masuala ya usalama wa kidigitali.
 
Back
Top Bottom