Kuwa na kilimo cha kisasa ni lengo la pamoja la China na nchi za Afrika

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
d077a26fc3a04555b21d550c78b6755d.jpeg


Mkutano Mkuu wa Kazi Vijijini wa China ulifanyika wiki hii mjini Beijing. Katika miaka ya hivi karibuni, imekuwa desturi kwa Chama cha Kikomunisti cha China CPC kuitisha mkutano kama huo baada ya mkutano mkuu wa kazi za kiuchumi kila mwezi Desemba ili kupanga kazi kuhusu kilimo, vijiji na wakulima kwa ajili ya mwaka unaofuata.

Inawezekana kuwa watu wengi barani Afrika wanajua kuwa China ni nchi ya pili duniani kwa maendeleo ya kiuchumi na nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye maendeleo ya teknolojia, lakini si wengi wanaojua kuwa China pia ni nchi yenye maendeleo makubwa kwenye sekta ya kilimo ambayo watu milioni 700 wanaojishughulisha kwenye sekta hiyo. Kutoa kipaumbele kwa usalama wa chakula, na kuijenga nchi kuwa na nguvu kubwa kwenye sekta kilimo, ni maelekezo muhimu kwa Chama tawala na serikali ya China. Tangu Rais Xi Jinping aingie madarakani, amekuwa akirudia mara kwa mara kuwa usalama wa chakula ni "jambo muhimu zaidi nchini", akisisitiza kuwa haipaswi kulegeza mkazo kwenye usalama wa chakula kwa wananchi katika wakati wowote.

Huu ni ukweli kwa China, lakini pia unafaa kwa nchi za Afrika. Kilimo ndio nguzo kuu ya uchumi wa nchi nyingi za Afrika, ikichukua zaidi ya 17% ya Pato la Taifa katika nusu ya nchi za Afrika (wastani wa kiwango hiki ni 4% duniani). Msingi muhimu wa maendeleo ya Afrika upo katika sekta ya kilimo. Hata hivyo, kutokana na kuwa nyuma kiteknolojia na ongezeko la kasi la idadi ya watu, pamoja na kuongezeka kwa sintofahamu kama vile mabadiliko ya tabia nchi na migogoro ya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, sasa zaidi ya watu milioni 300 wa Afrika wanakabiliwa na tatizo la chakula, sawa na robo ya idadi ya watu wote barani Afrika. Nchi nyingi za Afrika zinatambua kuwa ili kutimiza usalama wa chakula, ni lazima ziongeze uwezo wao wa kujitosheleza kwa chakula.

Ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta ya kilimo, una historia ndefu, na jina moja ambalo ni lazima litajwe ni marehemu Yuan Longping, “baba wa mpunga chotara” wa China. Mzee Yuan aliwahi kuahidi hadharani kwamba “Usalama wa chakula lazima upatikane sio tu nchini China, bali pia barani Afrika. Mwaka 2006, mzee huyo aliongoza timu yake kufika Madagscar, na kuanza safari ya miaka 15 ya kusaidia Afrika kilimo. Tangu mwanzoni wenyeji walipouita "mchele wa miujiza" hadi kuchapishwa kwenye noti mpya ya Madagaska yenye thamani ya Ariary 20,000, mpunga chotara wa Bw. Yuan umewezesha nchi hiyo kujitosheleza kwa chakula. Kabla ya kuhudhuria Maonesho ya tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika mwezi Juni mwaka huu, aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Madagaska, Rakotoson Filiber alifika kwenye eneo la makaburi la Tangren Wanshou mjini Changsha, mkoani Hunan, na kuweka bakuli lililojaa mpunga chotara kutoka Afrika mbele ya jiwe la kaburi la mzee Yuan, akisema "Mpendwa Mwalimu Yuan Longping, tumechelewa", watu wote waliomsikia wameguswa. Hivi sasa mbali na Madagascar, mpunga chotara wa China umefanikiwa katika nchi 16 za Afrika ikiwemo Tanzania.

Kwa msingi wa kuongeza uzalishaji wa chakula, uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia sasa unakuwa nguvu mpya inayoongoza ushirikiano wa kilimo cha kisasa kati ya China na Afrika. Baada ya Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika yaliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu, China ilitoa "Mpango wa China wa Kusaidia Kilimo cha Kisasa cha Afrika", ambao ulitaja kuwa utaongeza ushirikiano wa teknolojia ya kilimo na kuboresha mnyororo wa sekta ya kilimo barani Afrika na kuinua thamani ya mazao ya kilimo. Kwa sasa, China imejenga vituo 24 vya vielelezo vya teknolojia ya kilimo barani Afrika. Huku ikiongeza uzalishaji wa chakula, pia imepeleka huko teknolojia za hali ya juu zinazofaa. Na kuhusu sekta ya mnyororo wa mazao ya kilimo yenye sifa za Kiafrika, kwa upande mmoja, makampuni ya China yameanzisha vituo vya ushirikiano wa kilimo na viwanda vya kusindika barani Afrika, ili kuunganisha masoko na mashamba na kubadilisha mavuno ya wakulima kuwa mapato yao, na kwa upande mwingine, China imeendelea kupanua uagizaji wa bidhaa za kilimo za Afrika na kutoa sera kama vile msamaha wa ushuru na "njia ya kijani" kwa mazao hayo kuingia China ili kusaidia maendeleo ya kilimo cha kisasa barani Afrika.

Inaaminika kuwa China na nchi za Afrika zikishirikiana katika shughuli za kujijenga kuwa za kisasa, Waafrika sio tu wataweza kuwa na usalama wa chakula kama Wachina, bali pia watatumia ipasavyo maliasili zao bora na kujumuika vizuri katika mnyororo wa uzalishaji wa chakula duniani, ili kufikia maendeleo ya kisasa. Kwa sababu nchi yenye nguvu lazima kwanza iimarishe kilimo chake, na hapo ndipo inaweza kuwa na nguvu.
 
Back
Top Bottom