Nchi sita zaidi za Afrika kunufaika na soko la China

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG111258465500.jpg


Kuanzia tarehe 25 Desemba mwaka huu Angola, Gambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Madagascar, Mali, na Mauritania zitaungana na nchi nyingine za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China katika kunufaika na soko la China kwa asilimia 98 ya bidhaa zake za kilimo kuingia bila kutozwa ushuru wa forodha. Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za China katika kuimarisha mafungamano ya kiuchumi na nchi za Afrika, na kufanikisha ujenzi wa jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.

Kwa kipindi cha karibu miongo miwili sasa, China imekuwa inaendelea kuimarisha mafungamano ya uchumi na nchi za Afrika, na kujitahidi kuleta uwiano kwenye urari wa biashara kati yake na nchi za Afrika. Kwenye mkutano wa 8 wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika mjini Dakar mwishoni mwa mwaka 2021, Rais Xi aliahidi kuwa China itaendelea kuongeza uagizaji bidhaa kutoka Afrika, na kufanya thamani yake iongezeke kutoka dola za Marekani bilioni 100 kwa mwaka za 2022 na kufikia dola za kimarekani bilioni 300 ifikapo mwaka 2024.

Kutokana na udhaifu wa sekta ya viwanda katika nchi nyingi za Afrika, ni wazi kuwa uwezekano wa nchi za Afrika kuuza bidhaa za viwanda nchini China ni mdogo, lakini kutokana na manufaa ya kijiografia ya nchi za Afrika kuwa katika eneo la kitropiki, na kutokana na kuwa watu wengi zaidi wa Afrika wanajihusisha na sekta ya kilimo, China kufungua soko la bidhaa za kilimo ni njia ya moja kwa moja na yenye ufanisi kwa China kuhimiza maendeleo ya nchi za Afrika, na hata maendeleo ya mkulima mmoja mmoja wa Afrika.

Mbali na kuchukua hatua hii, China pia imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kusaidia uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka nchi za Afrika, Katika muongo mmoja uliopita, China imekuwa ikiandaa maonyesho mbalimbali ya biashara na kutoa vipaumbele mbalimbali kwa nchi za Afrika kutumia maonyesho hayo katika kutangaza bidhaa zake. Lakini imepiga hatua zaidi na kuufanya mji wa Changsha, Mkoani Hunan kuwa kituo muhimu na cha kudumu cha kuhimiza biashara ya mazao ya kilimo na nchi za Afrika.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita China pia imekuwa ikitumia TEHAMA na majukwaa ya biashara kwenye mtandao wa internet, kuhimiza uagizaji wa bidhaa za kilimo moja kwa moja kutoka kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo wadogo wa bidhaa za kilimo wa Afrika. Nchi mbalimbali zinaendelea kunufaika na fursa hizo, na kuweza kujiendeleza kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Tukiangalia kwa undani, tunaweza kuona kuwa juhudi za China hazijaishia tu kwenye kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa hizo za kilimo. Changamoto kubwa ambayo imekuwa inazikabili nchi za Afrika kutumia fursa hiyo, imekuwa ni changamoto ya kukidhi vigezo vya karantini, yaani bidhaa hizo ziweze kupita kwenye forodha za China zikiwa salama na kutoleta hatari yoyote ya kiafya kwa wateja wa China.

Kupitia ushirikiano wa pande mbili, sio kama tu China imekuwa ikisaidia kuongeza kiasi na ubora za mazao yanayozalishwa barani Afrika kwa ajili ya soko la China, lakini pia imekuwa ikishirikiana na mamlaka za nchi za Afrika kuwezesha wakulima na kukidhi vigezo hivyo. Bila shaka kadiri bidhaa za Afrika zenye fursa ya kuingia kwenye soko la China bila ushuru zitakavyokidhi vigezo vya karantini, ndio bidhaa nyingi zaidi za Afrika zitaweza kuingia kwenye soko la China, na hatimaye kutimiza lengo la kuweka uwiano kwenye urari wa biashara kati ya pande mbili.
 
Back
Top Bottom