Nakubaliana nawe MM,
Kuna mchezo unachezwa!
Wameendelea kuucheza, tena katika uwanja mpya wa gharama kubwa.
Afrika mashariki hakuna nchi yenye uwanja kama ule. Uwanja una kila aina ya ufahari, wachezaji wanaweza kuamua kulala uwanjani bila kuulizwa. Wakiamka wanashangilia bila kujali kuwa timu yao ndo imefungwa goli. Kwa hakika inasikitisha, lakini bado wako uwanjani wanaendelea kucheza.
Nimeangalia na kuwaona walio wengi wanacheza bila kujua kanuni, wanaamini mwalimu wao anajua na kwao hilo latosha. Ni wabishi, hudiriki hata kubishana na picha. Wamesahau kuwa watizamaji walio wengi wanajua kanuni na wanaweza kuucheza mchezo vizuri kuliko wao. Hawaamini, waendelea kucheza.
Nasikia watakutana na mkuu wao siku chache zijazo. Huenda akawakumbusha kanuni na mbinu za mchezo, japo nina uhakika hawatashika. Wana vichwa vigumu au ni wajuaji. Wamekaa na mwalimu wao mara nyingi, huwa hawamuelewi. Hata wakijitokeza walimu wa kimataifa hawaelewi zaidi ya kuwabeza. Wanaendelea kucheza mchezo wasioujua, ni hatari kwao. Watazamaji wamewachoka, wameanza kususia mchezo wao. Hawaamini, wanaomba 'wananchi tusikilizeni sisi'. Sina hakika kama watawasikia, kanuni hawazijui na wanacheza mchezo vibaya, hauvutii.
Kuna mchezo unachezwa, wanaendelea kucheza, kwamba watamaliza salama ni jambo la kufuatilia kwa makini.