Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) chalaani kilichofanywa na TANAPA na TAWA kuhusu uvunjifu wa Haki za Binadamu

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,308
5,460

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinalaani matukio ya uvunjifu wa Haki za binadamu yanayodaiwa kufanywa na Askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori (TAWA) baada ya kuwepo vitendo vya kupigwa na kuuwawa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa (LHRC), Dkt. Anna Henga ambaye ni Wakili, wakati akizungumza waandishi wa habari kulaani matukio ya Uvunjifu wa Haki za Binadamu yanayofanywa na Askari wa TANAPA, TAWA, TFS kwa wananchi wanaoishi karibu na Maeneo ya Hifadhi za Taifa na Mapori Tengefu.
Anna 1.JPG

Mkurugenzi Mtendaji wa (LHRC), Dkt. Anna Henga

Aidha, Henga amesema mara baada LHRC kupata taarifa juu ya vitendo hivyo ilituma timu ya maofisa wa kituo hicho walibaini kuwepo kwa vitendo vya kupigwa,vitendo vya mauaji, kudhalilishwa,kufukuzwa kwenye maeneo yao na kunyang'anywa mifugo kinyume na Sheria.

"Vitendo hivi vya kikatili vilihusisha watu kutoka familia moja ambao ni Doris milakon Saturu,Anna Milakon Saturu,Rehema milakon Saturu pamoja na wanaume ambao ni Golyama chimya na Mage Ntalamila,” amesema Henga.

Hata hivyo, Henga amesema matukio hayo ni miongoni mwa matukio mengi yanayotokea katika jamii za wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi ambapo kwa mwaka huu LHRC kwa mwaka huu imepokea matukio manne ambapo ni kinyume na Haki za Binadamu zilizoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 14-16 ya mwaka 1977.

Sanjari na hayo LHRC imeitaka serikali kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa vitendo hivi wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

"Pia Serikali iunde tume maalum au kikosi kazi kitakochofanya kazi ya Uhakiki yaani (Special Audit) wa mipaka katika maeneo yote ya hifadhi na mapori tengefu ambayo kwa muda mrefu na nyakati tofauti yamekuwa yakisababisha migogoro,” ameshauri Henga.


==================== =================

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinasikitishwa na taarifa za matukio ya ukikwaji wa Haki za Binadamu yanayofanywa na askari wa TANAPA, TAWA na wakala wa misitu Tanzania katika jamii za watu wanaoishi karibu na hifadhi za taifa na mapori tengefu. Matukio haya yamekuwa yakijumuisha, kupigwa, vitendo vya mauaji, kudhalilishwa, kufukuzwa kwenye maeneo yao na kunyang’anywa mifugo kinyume cha sheria.

Tukio mojawapo ni la tarehe 6 Mei, 2023 lililotokea kijiji cha Mwanavala Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, ambapo watu watano walipigwa na kujeruhiwa na Askari wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) watu hao walikua wanawake watatu na wanaume wawili, walivuliwa nguo, kupigwa na mapanga ya moto na kusababishiwa majereha makubwa sehemu mbali mbali za miili yao, watu hao wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 21 mpaka 39.

Vitendo hivi vya kikatili vilihusisha watu kutoka familia moja ambao ni Doris Milakon Saturu, Anna Milakon Saturu na Rehema Milakon Saturu, pamoja na wanaume ambao ni Golyama Chimya na Mage Ntalamila.

Ndugu wanahabari,
Baada ya taarifa hizi kusambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilichukua hatua ya kufanya utafiti wa kina ili kubaini ukweli juu ya taarifa hizi za kusikitisha ambapo kwa mujibu wa utafiti wetu tulibaini kuwa taarifa hizi ni za kweli kwani zilithibitishwa na mamlaka za serikali ya wilaya ya Mbarali akiwemo Mkuu wa Wilaya na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, sambamba na taarifa hizo kuthibitishwa na serikali ya wilaya ya mbarali, wakati huohuo taarifa hizo zilithibitishwa na Waziri wa maliasili na utalii Mhe Mohamed Mchengerwa ambapo wizara ilitoa kiasi cha shillingi million moja 1,000,000 kwa wahanga wote waliojeruhiwa na vitendo hivi vya kikatili kama mkono wa pole.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu baada ya kufika eneo la tukio na kuongea na wahanga wa matukio hayo ya udhalilishaji na ukiukwaji wa Haki za Binadamu pamoja na mamlaka ya eneo husika kilibaini kwamba ni kweli watu hao walipigwa, kuvuliwa nguo na kuchomewa vitu vyao na askari wa TANAPA, lakini sio hao tu waliotendewa vitendo hivyo vya kikatili kwani afisa wa kituo baada ya kuongea na wanakijiji wa Mwanavala alibaini kuwa matukio haya ya unyanyasaji ikiwemo kuporwa kwa mifugo na kuuwawa kwa wafugaji ni matukio endelevu katika eneo hilo.

Ndugu wanahabari,
Matukio haya ni miongoni mwa matukio mengi yanayotokea katika jamii za wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi za Taifa. LHRC kwa mwaka huu pekee imepokea matukio ya uvunjifu wa Haki za binadamu yasiyopungua manne, matukio hayo ni pamoja na kuuwawa kwa wananchi, kufukuzwa kwenye maeneo yao pasipo kulipwa fidia, kunyang’anywa mifugo kinyume cha sheria pamoja na kujeruhiwa na kudhalilishwa. Matukio hayo ni kinyume na Haki za Binadamu zilizoainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 14-16 ya mwaka 1977.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani vikali matukio hayo yanayoendelea nchini kwani matukio hayo yanapoka Haki za Binadamu.

Ndugu wanahabari,
Matukio haya ya migogoro baina ya mamlaka za hifadhi na wananchi yamekua chanzo kikubwa cha uvunjifu wa Haki za Binadamu kwa kipindi kirefu. Aidha migogoro baina ya wananchi na mamlaka za hifadhi za Taifa hususani hifadhi ya Ruaha iliyoko wilayani Mbarali mkoani Mbeya ni mfano hai wa migogoro ya muda mrefu na waathirika wakubwa wamekuwa ni kina mama, na watoto. Kwa bahati mbaya kumekuwa na uzito kiasi fulani kwa Serikali katika kuchukua hatua stahiki kumaliza migorogo hiyo na kuepusha mauaji yanayoweza kuepukika.

Ndugu wanahabari,
Sambamba na mgogoro wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, migogoro inayofanana na hiyo ambayo pia imeripotiwa kusababisha vifo na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu ikiwemo kujeruhiwa kwa wananchi ni ule wa Hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara ambapo wavuvi watatu wanaripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara mkoani Manyara. Matukio kama hayo yanaripotiwa kutokea katika pori tengefu lilipo wilaya ya Geita mkoani Geita, tunazo taarifa za matukio kama hayo kutokea katika Hifadhi ya Taifa ya Kilamanjaro (KINAPA) ambapo huu ni moja ya migogoro ya muda mrefu ambayo inaonekana kuleta mvutano mkubwa kati ya wananchi wanaoishi Jirani na maeneo ya hifadhi hiyo.

Ndugu wanahabari,
Tunaomba ifahamike kwamba LHRC kama taasisi ya haki za binadamu hatuungi mkono na wala hatuna nia ya kuunga mkono wananchi kuvamia katika maeneo ya hifadhi yaliyoanishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania lakini tunazitaka mamlaka zinazohusika na uhifadhi ikiwemo TANAPA, TAWA na Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) kuzingatia misingi ya haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa amri za kuwaondoa na kuwahamisha wananchi katika maeneo ya hifadhi.

LHRC inatoa wito kwa serikali na jamii kama ifuatavyo:
  • Kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa vitendo hivi wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
  • Askari wa Hifadhi za Taifa na misitu kuzingatia misingi ya haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa amri za kuwaondoa na kuwahamisha wananchi wanaovamia katika hifadhi za taifa na misitu kinyume cha sheria
  • Wananchi wanaoishi Jirani na maeneno ya hifadhi kuacha kuvamia katika maeneo yalianishwa kama hifadhi au mapori tengefu kwa mujibu wa sheria.
  • Serikali iunde tume maalum au kikosi kazi kitakachofanya kazi ya uhakiki yaani( special Audit) wa mipaka katika maeneno yote ya hifadhi na mapori tengefu ambayo kwa muda mrefu na kwa nyakati tofauti tofauti yamekuwa yakisababisha migogoro kati ya wananchi na askari wa mamlaka za wanayamapori.
Imetolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu:
Dkt. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji.
 
Back
Top Bottom