Wadau wa Haki za Binadamu wazungumzia Umuhimu wa Utawala Bora wa Sheria

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
WASHIRIKI.JPG
WADAU wa Haki za Binadamu Zanzibar wameshauri kuimarisha mifumo ya utawala bora wa sheria ili kuhakikisha uwajibikaji na upatikanaji wa haki kwa wote unafikiwa katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Wametoa maoni hayo katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) kuhusu utawala bora wa sheria, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto.

Dkt. Salum Suleiman, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar akiwasilisha mada juu ya Utawala wa Sheria na upatikanaji wa sheria bora alisisitiza umuhimu wa sheria zilizopo kuhafamika na watu wote ili kuondoa mianya ya ukandamizaji wa haki za wengine.

Alieleza ikiwa kundi la wananchi wengi watakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya sheria zilizopo katika masuala mbalimbali itarahisisha kuepukana na makosa mbalimbali hasa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Alieleza, "moja ya misingi ya utawala wa sheria ni lazima sheria zinazotumika zifahamike na watu wote, na ili hilo liweze kufikiwa ni lazima kuwe na mfumo imara wa kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa rahisi.”

Akifungua mdahalo huo, mwenyekiti wa TAMWA ZNZ, Asha Abdi, alieleza katika kampeni hiyo, TAMWA ZNZ inatumia siku hizo 16 kuhimiza jamii kuwekeza katika utawala wa sheria kwa upatikanaji wa haki sawa kwa kila mtu bila kujali hali zao.

"Leo tunaadhimisha siku hii ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili, ambapo TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wetu tumeamua kuja na ujumbe unaohimiza kuwekeza katika utawala bora wa sheria kwa upatikanaji haki sawa kwa wote ili kukabiliana na changamoto zinazopelekea uvunjifu wa haki za binaadamu."

Nabir Mohamed Mussa kutoka ZAFAYCO, alisisitiza wadau hasa serikali kubadili mwelekeo wa kukabiliana na tatizo la ukatili kwa kutazama zaidi chanzo cha watu hasa vijana kujiingiza katika vitendo vya udhalilishaji kuliko kupambana na utoaji wa hukumu kali jambo ambalo wakati mwingine halisaidii kutatua tatizo.

Alieleza, “ukifuatilia utagundua kesi za udhalilishaji zimeshindwa kumalizika kutokana na serikali imewekeza nguvu zaidi katika kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa badala ya kuwekeza katika kutibu mizizi ya chanzo cha vitendo hivyo, watu wanafungwa lakini ukikaa chini na kuangalia utagundua tatizo sio kuwafunga tatizo lipo huku kwenye jamii yenyewe kuanzia malezi, tunahitaji kurekebisha kuanzia huku.”

Nae Rashid Mwinyi, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Pamoja Youth Initiative, alieleza upatikanaji wa sheria zinazotungwa ni changamoto kwa wananchi wa kawaida kutokana na kukosekana kwa mfumo maalum unaowezesha watu wanapohitaji kusoma sheria kuzipata kwa urahisi jambo linalopelekea wengi kushindwa kuzijua sheria zinazowahusu.

Alieleza, "Sheria nyingi zilizopo hazipatikani kwa wote, lazima kuwe na mfumo ambao unatoa fursa kwa kila mmoja kuzipata na kusoma kwa urahisi, lakini leo ukitaka sheria fulani unaweza kwenda hadi ofisi husika hata wale wafanyakazi wakakwambia hawana hadi mtu fulani jambo ambalo ni shida sana.”

Awali, Tatu Abdalla Msellem, Mratibu wa Taasisi ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE), alishauri umuhimu wa kupatikana sheria moja ya kusimamia kesi za udhalilishaji ili kuondoa changangamoto zinazokwaza upatikanaji wa haki wa waathirika wa vitendo hivyo.

"Kuna umuhimu mkubwa sana kupatikana sheria moja ya kesi za udhalilishaji, na hii itasaidia kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye usimamizi wa kesi hizo kutokana na kukosa sheria moja inayosimamia kupata hukumu kwani wengi wanatumia mwanya huu kujiondoa," alieleza Tatu.

Katika hatua nyingine, Said Suleiman Ali, mmoja wa washiriki, alitoa wito wa sheria zinazotungwa kutafsiriwa kwa lugha rafiki kwaajili ya watu wenye ulemavu ili kuwapa nafasi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi.

"Ukifuatilia hizi sheria tulizonazo utagundua hakuna hata sheria moja iliyoandikwa kwa lugha za nukta ili kuwawezesha watu wenye ulemavu nao kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi hizi sheria, kuna haja sasa ya sheria huzi zitafsiriwe kwa lugha ya nukta, huu ndio utawala bora wa sheria wenyewe kwa upatikanaji wa haki sawa kwa wote.”

Awali akichangia kwenye mdahalo huo, Sarah Omar, Hakimu wa Mahkama ya Mkoa, alisema mahakama hutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria zilizotungwa bila kujali matakwa ya mtu au kundi fulani.

Alieleza hakimu huyo, "Mahakama ni zao la sheria, kila kinachofanyika mahakamani kinafanywa kwa mjibu wa sheria na sio matakwa ya mtu Fulani.”

Mdahalo huo ambao umeandaliwa na chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Shirika la Foundation For Civil Society (FCS) umewaleta pamoja wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali na kiraia wakiwemo mahakimu, waendesha mashtaka, Polisi Dawati, viongozi wa dini, wanamtandao wa kupinga udhalilishaji na maafisa ustawi wa jamii.
 
Back
Top Bottom