JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,308
- 5,460
Kupitia taarifa yake kwa umma Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini yaani, Association of Private Health Facilities in Tanzania (APHFTA), Christian Social Service Commission (CSSC) pamoja na BAKWATA iliyotolewa tarehe 27 Februari 2024 ilibainisha bayana kwamba vituo vya afya binafsi vingeshindwa kutoa huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kutumia kitita kipya ambacho hawakubaliani nacho.
Taarifa hiyo ilienda mbali zaidi kwa kuwataka wanachama wa NHIF kuwasiliana na mfuko wa bima ya afya (NHIF) ili kupata hatima ya namna watakavyopata huduma hizo.Kwa upande wake Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupata taarifa yake kwa vyombo vya habari ya tarehe 1 Machi 2024 ulikiri kuona tangazo la kusitisha huduma kwa wanachama wa NHIF kwa baadhi ya vituo binafsi, hivyo kuwataka wanachama wake kutumia vituo mbadala ili kupata huduma wanazohitaji, pili, maofisa wake watakuwa katika vituo ili kuhakikisha wanachama wenye changamoto wanasaidiwa kupata huduma katika vituo vingine, tatu, mfuko ulikuwa umeshaanza kuwasiliana na wanachama wenye matibabu yanayohitaji mwendelezo ya huduma ili kuwaelekeza vituo mbadala kwa ajili ya kupata huduma husika.
Kwa mazingira tajwa, ni dhahiri kuwa kuna mgogoro katika watoa huduma, vituo binafsi na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mgogoro ambao moja kwa moja umeshaleta athari kwa watanzania wasio na uwezo wa kulipia vitita vya ziada au fedha taslimu kupelekea uvunjifu wa haki za binadamu kama haki ya afya na ile ya kuishi.
Kwa nyakati tofauti Mahakama kuu ya Tanzania katika shauri la Festo Balegele na wenzake 794, dhidi ya Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, shauri namba 90 la mwaka 1991 na lile la Felix Joseph Mavika dhidi ya Tume ya jiji la Dar es Salaam, shauri namba 316 la mwaka 2000, yote kwa pamoja Mahakama kuu ya Tanzania ilitamka kuwa kukiuka haki ya afya ni kukiuka haki ya kuishi kinyume na ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Tanzania ni nchi mwanachama wa mikataba mbalimbali ya kimataifa na ile ya kikanda ambayo yote kwa pamoja inazitaka nchi wanachama kulinda na kuhifadhi haki ya afya. Kwa mfano ibara ya 12 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni wa mwaka 1966, ibara ya 16 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1981 pamoja na ibara ya 16 ya Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1981, yote kwa pamoja inazitaka nchi wanachama kulinda na kuhifadhi haki ya afya.
Mwisho, kutokana na sintofahamu hii LHRC inatoa wito kwa Serikali na watoa huduma kama ifuatavyo:
i. Serikali itafute mwafaka wa mgogoro huu na watoa huduma ili
kuepusha kuvunjwa kwa haki ya afya
ii. Wakati mazungumzo yanaendelea na mwafaka ukitafutwa, watoa huduma waendelee kuwahudumia watanzania ili kuepusha madhara ya kupoteza uhai wa watanzania wasio na hatia.
iii. Serikali iweke wazi viwango vya gharama za kitita kinachobishaniwa ili kuongeza wigo wa Uwajibikaji na uwazi.
iv. Serikali iheshimu na kutekeleza maadhimio ya bunge lililoitaka Serikali kutatua mgogoro huu kwa njia za mazungumzo.
v. Watoa huduma wafuate utaratibu uliopo kisheria kuwasilisha
malalamiko yao wakati huduma zikiendelea kama kawaida.
vi. Kwa kuwa wahanga wakubwa ni wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu, tunashauri makundi haya yaendelee kupewa kipaumbele katika kipindi ambacho mazungumzo yanaendelea.