Imeandikwa na Namsembaeli Mduma; Tarehe: 25th July 2011
HOTELI kubwa mbili za kitalii jijini Dar es Salaam zenye hadhi ya juu nchini zitabadilishwa majina yake ya sasa kwa mara nyingine kutokana na kuuzwa kwa mojawapo na nyingine kwa sababu ya kubadilisha kampuni inayosimamia masuala ya uongozi.
Hoteli hizo, Kilimanjaro Kempinski na Royal Movenpick ndizo zinazoelezwa kuwa mbioni kubatizwa majina mapya ifikapo Agosti mosi mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Utalii nchini, Ibrahim Musa alisema taarifa rasmi alizonazo ni za kubadilishwa kwa jina la Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski kuwa Kilimanjaro Hyatt mwezi ujao.
Musa alisema suala la Movenpick bado lipo mikononi mwa wenye hoteli wenyewe na kwamba ni vigumu kwake kulizungumzia kwa sasa kwa sababu taarifa rasmi hazijaifikia meza yake.
"Nitazungumzia Kempinski pekee kwa sasa kwa sababu hiyo ya Movenpick bado wenyewe hawajatuletea taarifa rasmi kuihusu. Nina taarifa ya kuwepo kwa mazungumzo kati ya wanaoendesha Movenpick na wadau wengine, lakini siwezi kuyasema kwa kuwa sio rasmi," alisema Mkurugenzi wa Utalii.
Hata hivyo, pamoja na maelezo hayo ya Mkurugenzi wa Utalii, gazeti hili lilipata taarifa za kuwepo kwa mpango wa kubadilishwa jina kwa hoteli hiyo ya Movenpick kuwa Serena endapo wauzaji (Movenpick) na wanunuzi (Serena) watafikia makubaliano.
Aidha, imefahamika kuwa pande hizo mbili zipo katika mazungumzo ya mwisho kuhusu kuuziana hoteli hiyo ili utekelezaji wake ufanikishwe ifikapo mwanzoni mwa mwezi ujao.
Akifafanua kuhusu Hoteli ya Kempinski, Mkurugenzi huyo alisema kitakachofanyika hakitakuwa na athari zozote katika uwekezaji wala ulipaji wa kodi kwa sababu umiliki unakuwa bado ni wa mhusika wa awali.
"Tuliliangalia suala la kodi kwa kina na kujiridhisha kuwa halitaathiriwa kwa namna yoyote kwa kubadilishwa jina kutoka Kempinski kwenda Hyatt. Kitakachobadilika ni kampuni inayoshughulika na masuala ya uongozi wa hoteli hiyo kutokana na kumalizika kwa mkataba wake na wamiliki," alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema kampuni hiyo mpya iitwayo Hyatt ni ya Kimarekani na kwamba wamekubaliana nao wasiondoe jina la Kilimanjaro ili kulinda historia ya Mlima wa Kilimanjaro ambao ni fahari ya Tanzania.
"Pamoja na kuangalia masuala ya kodi, pia tuliwaomba wahusika wasiliondoe jina hilo Kilimanjaro kama njia moja ya kulinda historia ya mlima wetu. Walikubali kwa kweli na kutufahamisha kuwa jina hilo litaendelea kutumika kwa kuwa ndio linalowavutia wateja wengi wanaofika kupata huduma katika hoteli hiyo," alisema.
Juhudi za kumpata Meneja wa Hoteli wa Kempinski aliyejulikana kwa jina moja la Trevo, ziligonga mwamba baada ya Ofisa wa Mapokezi aliyejitambulisha kwa jina Oswald Akyoo, kumzuia mwandishi wa habari hizi kumwona kwa maelezo kuwa haikuwa siku ya kazi. Kuhusu uwezekano wa kuwepo athari katika makusanyo ya kodi kutokana na kuuzwa kwa Hoteli ya Movenpick endapo suala hilo litatekelezwa, Mkurugenzi wa Utalii nchini alisema itakuwa vema likizungumzwa wakati litakapotokea.
"Kwa kuwa wapo kwenye mazungumzo, hatuwezi kusema imeuzwa, tusubiri watupe taarifa ndio tuzungumzie suala hilo. Lakini kwa vyovyote, Serikali haiwezi kuruhusu athari katika uchumi wake hivyo sitegemei zitokee," alifafanua Musa.
Kumekuwa na hofu miongoni mwa Watanzania kuhusu kubadilishwa kwa majina ya hoteli nchini huku wengi wakidhani ni njama za kukwepa kulipa kodi katika miaka mitano ya uwekezaji wa kwanza.
Lakini Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), Dk. Adelhelm Meru aliwahi kusema mabadiliko ya majina ya uwekezaji pekee hayana athari katika kodi.