Operation Wet-i-e Counter-Coup

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Jun 28, 2016
348
843
OPERATION WET-I-E COUNTER-COUP; MAPINDUZI PEKEE AFRIKA YALIYO JIRATIBU YENYEWE, YAKAPINDUA NAYO YAKAPINDULIWA KISHA YAKAIGEUZA NIGERIA KUWA UWANJA WA MAPINDUZI.

Na. Comred Mbwana Allyamtu.
Saturday-13/06/2020.
Moshi, Kilimanjaro, Tanzania.

Nigeria ndio taifa lenye uchumi mkubwa kwa sasa barani Afrika, uchumi wake wa pato ghafi la taifa ni GDP US$ 450 billion, Pato hili inaliweka Nigeria Katika taifa lenye uchumi wa kati duniani, pato la mtu mmoja yani per capital income ni 2200 US$, nje na kuwa na uchumi mkubwa Afrika wenye pato ghafi kubwa bado nchi hiyo ina idadi kubwa sana ya masikini na ufukara wa kutupa kwa Raia wengi nchini humo.

Nigeria ndio taifa lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika, kwa sasa ina jumla ya watu milioni 210, nafasi inayoweka kuwa miongoni mwa mataifa yenye idadi kubwa ya watu duniani.

Nigeria ilipata uhuru wake tarehe 1 Oktoba 1960 kutoka kwa Uingereza, Nigeria ni nchi ya Afrika Magharibi inayopatikana kwenye pwani ya Bahari ya Atlantiki, Mji mkuu ni Abuja uliyopewa hadhi ya kuwa makao makuu ya taifa hilo tarehe 12/12/1991 baada ya kuhamishwa kutoka Lagos mwanzoni mwa miaka ya 1991.

Mji wa Abuja umepewa hadhi ya kuwa jimbo linalo jiongoza lenyewe kama ilivyo Washington DC kwa Marekani, kwa Nigeria Abuja Ni makao makuu ya nchi yenye utawala unaojiendesha yani "Federal Capital Territory (FCT)", ni Eneo maalum la utawala lisilo na mwakilishi wala seneta kwenye bunge la nchi hiyo, isipokuwa utaratibu wa uendeshwaji wake upo chini ya baraza la eneo hilo liitwalo "Federal Capital Territory Council (FCTC)".

Rais wa sasa ni Muhammadu Buhari ambae ni rais wa 15, mkuu wa nchi wa 16 na mtu wa 13 kushikilia kiti cha urais toka taifa hilo lipate uhuru mwaka 1960 na kuwa jamuhuri rasmi mwaka 1963, serikali ya kwanza iliundwa na Waziri mkuu Sir Abubakar Tafawa Balewa, na raisi Dr Benjamin Nnamdi Azikiwe na Chief Obafemi Awolowo akiwa Kama kiongozi wa kimila nchini Nigeria.

Waasisi wakubwa wa taifa hilo ni wawili, Dr Benjamin Nnamdi Azikiwe, Maarufu kama ''ZIK" aliyekuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo na Dr Sir Abubakar Tafawa Balewa, Waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo, pia viongozi wengine 11 hutambuliwa kama waasisi wa taifa hilo ambao ni Herbert Macaulay, Professor Eyo Ita, Alvan Ikoku,Chief Obafemi Awolowo, Al-Haji Sir Ahmadu Bello, Chief Anthony Enahoro, Sir Egbert Udo Udoma, Al-Haji Aminu Kano, Chief S. A. Ajayi, Joseph Tarka na Dennis Osadebay.

Operesheni Wet-i-e ilianza toka mnamo mwaka 1962 wakati Chief Ladoke Akintola na Chief Obafemi Awolowo walipoingizwa katika mzozo uliojitokeza na kusababisha kiwango cha juu cha vurugu na vitendo vya uvunjifu wa sheria kwenye bunge la jimbo la magharibi ya Nigeria, operation hii ilileta vuguvugu la mabadiliko makubwa kwenye safu nzima ya kisiasa nchini Nigeria miaka 4 baadae.

Neno "WET-I-E" lenyewe lilitumika magharibi mwa Nigeria kuelezea hisia zao juu ya mageuzi yaliyotawaliwa na chuki za kidini dhidi ya jamii ya Furani na Hausa huko kaskazini mwa nchi ya Nigeria, code hiyo ilimaanisha "Wild,Wild, West" ambayo baadaye dhana hiyo ilikuja kutumiwa na Chukwuma Kaduna Nzeogwu katika kutekeleza mapinduzi ya tarehe 15 januari 1966 ambapo yalipewa jina la "Operation Wet-i-e Counter-Coup, mwenyewe Chukwuma Kaduna Nzeogwu hakuwahi kuyaita hivyo ila wasomi wa Nigeria baade waliyapa jina hilo kutokana na chanzo chake na tukio la mapinduzi ndani ya mapinduzi la mwaka 1966 yalivyo chochewa na oparetion WET-I-E miaka 4 nyuma.

Taifa la Nigeria ndio taifa lilikumbwa na mapinduzi mengi Afrika kuliko nchi yoyote ile, mapinduzi ya kwanza ya mwaka 1966 nchini Nigeria ni mapinduzi pekee Afrika ambayo yaliongozwa na msukumo wa ndani bila kuingiliwa na misukomo ya mataifa ya magharibi au mashariki, ndio mapinduzi ambayo hayakuwa na mkono wa ubepari kwa maana yap nchi kama Marekani, Uingereza au Ufaransa.

Lakini ajabu ni kwamba miezi saba (7) baade yani Julai 1966 yakafanyika mapinduzi tena, yani mapinduzi juu ya mapinduzi kuipindua serikali ile iliyo fanya mapinduzi ya kwanza ya tarehe 15 January 1966, safari hii mkono wa Marekani ulihusika katika kuratibu mapinduzi ambayo yalibeba sura ya kulipiza kisasi kutoka wanajeshi wa kaskazini waliokuwa waislamu.

Mapinduzi ya kwanza ya serikali ya Nigeria ya mwaka 1966 yalianza tarehe 15 Januari mwaka 1966, wakati wanajeshi wa Nigeria walioasi wakiongozwa na Chukwuma Kaduna Nzeogwu na Emmanel Ifeajuna walipowauwa watu 22 akiwemo Waziri Mkuu wa Nigeria, wanasiasa waandamizi, maofisa wa jeshi wandamizi (wakiwemo wake zao), na walinzi waliokuwa katika zamu.

Wapanga njama za mapinduzi walishambulia miji ya Kaduna, Ibadan, na Lagos wakati huohuo pia wakiweka vizuizi katika mto Niger na Benue kwa muda wa siku mbili kabla ya wapanga njama za mapinduzi hayo kuidhibiti kabisa serikali iliyokuwa madarakani.

Mkuu wa Majeshi wa Nigeria wakati huo, Afisa Jenerali, Johnson Aguiyi-Ironsi, akalazimika kudhibiti serikali wakati nchi ilipoingia katika misukosuko ya bila kutegemea na kuiweka demokrasia ya Nigeria katika hali ya sintofahamu, Jenerali Ironsi akatangaza kuchukua nchi kwa kujitangaza kuwa mkuu wa serikali na dola.

Watu wa kaskazini mwa Nigeria kutoka kabila la Furani walidhania kuwa Jenerali Ironsi alikuwa mmoja wapo na waliokula njama za kufanya mapinduzi, ambao wengi wao walikuwa ni maofisa wa kabila la Igbo, ambao walifanya mapinduzi kumtengenezea njia Jenerali Aguiyi-Ironsi kuwa Mkuu wa nchi wa Nigeria.

Kutokana na sababu hiyo, matukio ya kulipiza kisasi kwa wanajeshi wa jeshi la Nigeria wanaotoka Kaskazini kulipelekea mauaji mengine ya wanajeshi wasio na hatia wa kabila la Igbo na raia iliyosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Nigeria.

Chanzo cha mapinduzi yenyewe...

Mwezi Agosti mwaka 1965 kundi la wanajeshi wenye vyeo vya Meja (group of Army majors) kutia ndani Emmanuel Ifeajuna, Timothy Onwuatuegwu, Chris Anuforo, Don Okafor, Humphrey Chukwuka, na Adewale Ademoyega walianza kupanga njama za mapinduzi kumpindua Waziri Mkuu aliyekuwa madarakani Sir Abubakar Tafawa Balewa.

Mapinduzi hayo yalipangwa kwa sababu kwa mujibu wa wanajeshi hao wenye vyeo vya Meja, kudai kwamba watu waliokuwa katika shuguli za uongozi walikuwa wanaiendesha Nigeria kwa njia za rushwa, Mawaziri walikuwa wanaishi maisha ya anasa na kupora raslimali za umma zilizotokana na garama za wananchi wa kawaida, ukweli ni kwamba mapinduzi hayo yalilenga kuondoa viongozi wa kiislamu kutoka jamii ya kabila la FURANI na HAUSA, ambayo ilionekana kuwa na nguvu katika nchi hiyo.

Rais wa Nigeria, Dk. Nnamdi Azikiwe yeye aliondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka 1965, kwanza akienda barani Ulaya, kisha akasafiri kwa meli ya kifahari kwenda kula "bata" huko Caribbean, kikatiba na sheria, ilibidi nafasi ya Rais ikaimiwe na mtu mwingine kwa muda ambao rais atakuwa nje ya Nigeria, Rais wa Baraza la Seneti, Nwafor Orizu, akakaimu Urais wakati Azikiwe akiwa hayupo nchini na kuwa na nguvu zote kama Rais wa nchi.

Asubuhi ya tarehe 15 Januari, mwaka 1966, katika mkutano na baadhi ya waandishi wa habari wazawa mjini Kaduna ambao Meja Nzeogwu aliuitisha kuwajuza nini kinachoendelea, Meja Nzeogwu aliwaambia kwamba habari zozote kuhusu matukio zitakuwa zile tu ambazo zitatangazwa na BBC, Nzeogwu alishangazwa kwa sababu alitegemea kuona matangazo ya redio za ndani kutoka kwa waasi jijini Lagos ambayo redio za ndani haya kuzitoa tofauti na BBC pekee.

Wakati akitoa taarifa hiyo tayari maafisa wa jeshi ambao walikuwa ni watiifu kwa Meja Nzeogwi walikuwa tayari wamemteka nyara waziri mkuu Sir Abubakar Tawafa Balewa, baada ya kutekwa nyara hakuonekana tena mpaka baada ya siku mbili baadaye mwili wake uliokotwa pembezoni mwa barabara inayoelekea ofisini kwake akiwa ameuawa tayari.

Hivyo, Nzeogwu haraka haraka akatayarisha hotuba ambayo ilitangazwa katika Radio Kaduna kwenye mida ya saa sita usiku ambapo alitangaza amri ya kijeshi kwa eneo lote la jimbo la Kaskazini ya Nigeria.

Kaimu Rais Nwafor Orizu, kuona hivyo na yeye akatoa matangazo kwa Taifa kwa njia ya redio, baada ya kuwa amemjulisha kwa njia ya simu Rais Dk. Nnamdi Azikiwe kuhusu uamuzi wa baraza la mawaziri kutangaza kukabidhi madaraka kwa vikosi vya jeshi, Meja Jenerali Johnson Aguiyi-Ironsi ambae na yeye baadaye akatoa matangazo akikubali ukaribisho huo wa kukabidhiwa mamlaka ya kuidhiti nchi isiangukie kwenye machafuko.

Tarehe 17 Januari, Meja Jenerali Ironsi aliunda Baraza la Kijeshi jijini Lagos na mara moja akazuia kutumika kwa katiba ya nchi hiyo.

Adewale Ademoyega, mmoja wa watu waliohusika na mapinduzi hayo, anasema katika kitabu chake kiitwacho "KWANINI TULIWAPIGA"

“Hakukuwa na maamuzi yoyote katika kikao chetu juu ya ukabila katika kuwaondoa" Maamuzi yetu yalikuwa ya hekima, mawazo yetu yalikuwa kwa ajili ya taifa na malengo yetu yalikuwa bora, Hata wote waliokusudiwa kutiwa mbaroni, wanne walikuwa wa kutoka Kaskazini, wawili wa Magharibi, na wawili wa kutoka Mashariki.”

Idadi ya walio uwawa katika mapinduzi hayo ni Waziri Mkuu Sir Abubakar Tafawa Balewa, Waziri Ahmadu Bello, Waziri Samuel Ladoke Akintola, Waziri wa Fedha Festus Okotie-Eboh, Ahmed Ben Musa (Katibu Msaidizi Mwandamizi wa Usalama wa Taifa), Hafsatu Bello, Mrs Latifat Ademulegun, Zarumi Sardauna, Ahmed Pategi, (dereva wa serikali).

Huku idadi ya polisi na askari wa jeshi walio uwawa ni Brigedia Samuel Ademulegun, Brigedia Zakariya Maimalari, Kanali Ralph Shodeinde, Kanali Kur Mohammed, Luteni Kanali Abogo Largema, Luteni Kanali James Pam, Luteni Kanali Arthur Unegbe, Sajenti Daramola Oyegoke (alimsaidia Nzeogwu katika mashambulizi kwenye lodge ya Sardauna na kutokana na ripoti ya Polisi aliuawa na Nzeogwu mwenyewe), Koplo wa Polisi Yohana Garkawa, Lansi Koplo Musa Nimzo, Koplo wa Polisi Akpan Anduka, Koplo wa Polisi Hagai Lai, Philip Lewande.

Hivyo hiyo ndiyo hali halisi ilivyokuwa katika mapinduzi ya kwanza nchini Nigeria mnamo Januari 15, mwaka 1966, lakini siku chache tu baada ya mapinduzi ya kwanza kutekelezwa kukaibuka uasi mwingine ambao ulitekeleza mapinduzi ya pili ya Julai 1966 yani miezi 7 baadae, haya yalikuwa ni mapinduzi ya pili, katika mapinduzi mengi ya kijeshi yaliyokuja kutokea nchini Nigeria, Mapinduzi haya yaliratibiwa na Luteni Kanali Murtala Muhammed na maofisa wengi wa jeshi waliokuwa wanatokea kaskazini.

Huyu Murtala Ramat Mohammed ndiye aliyekuja kumpindua Jenerali Yakubu Gowon miaka tisa baadaye mwaka 1975, wakati Gowon akihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi huru za Afrika OAU, jijini Kampala Uganda, Murtala naye akaja kuuawa katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa mnamo mwaka 1976 lililofanywa na Luteni Kanali Buka Suka Dimka.

Turudi Lagos kushudia mapinduzi ya pili yalivyo ratibiwa.....

Mapinduzi haya yalianza kama uasi usiku wa Julai 28, mwaka 1966 na ilikuwa ni kama kulipiza kisasi kwa mauaji ya wanasiasa na maafisa wa jeshi kutoka Kaskazini yaliyofanywa na wanajeshi wengi wao wakiwa ni wa kabila la Igbo mnamo Januari 15, mwaka 1966, huu uasi wa mwezi Julai/mapinduzi ndani ya mapinduzi (counter coup) ulipelekea kuuawa kwa Mkuu wa kwanza wa nchi wa Kijeshi wa Nigeria Jenerali Johnson Aguiyi-Ironsi na Luteni Kanali Adekunle Fajuyi (ambaye alikuwa mwenyeji wa Aguiyi-Ironsi katika ziara yake) mjini Ibadan alikokwenda kama kuondoa aibu ya kutowapandisha vyeo maofisa wa jeshi wa kaskazini.

Baada ya kumaliza kazi ya kuiondoa madarakani serikali ya Ironsi, Luteni Kanali Yakubu Gowon alichaguliwa kuwa Mkuu wa nchi na wapanga njama za mapinduzi ya mwezi Julai, mwaka 1966.

Kwa mujibu wa Mwanahistoria Max Siollun wanajeshi kutoka kaskazini walikuwa na orodha ya msululu wa malalamiko kufuatia kutengwa baada ya mapinduzi ya Januari 15, mwaka 1966, mapinduzi ambayo yalipelekea kupanga mapinduzi ndani ya mapinduzi (counter-coup). Orodha ya msululu wa malalamiko yao ilikuwa kama ifuatavyo:

Mauaji ya viongozi wa kiraia na maafisa wa jeshi kutoka kaskazini baada ya kutengwa katika mapinduzi ya kijeshi ya Januari 15, mwaka 1966.

Wapanga njama za mapinduzi ya Januari 15, 1966, (wengi wao wakiwa wanajeshi wenye vyeo vya Meja) hawakushtakiwa kwa uhaini walioufanya na bado walikuwa wanalipwa pamoja na kuwa walikuwa kizuizini.

Tetesi za kuwepo kwa kifungu cha amri ya umoja wa "mapinduzi ya Waigbo" kuwaondoa wanajeshi kutoka kaskazini.

Kupandishwa vyeo kwa wanajeshi mbalimbali wa kabila la Igbo kutoka ngazi ya Meja kwenda Luteni Kanali.

Tetesi kwamba Jenerali Aguiyi-Ironsi kuwa na upendeleo wa ukabila kwa watu wa kabila la Igbo.

Mpango wa kuzibadilisha bataliani ya 1 na ya 4 na mpango wa magavana wa jeshi kutawala kwa kuzunguka mikoa mbalimbali.

Kutokana sababu hizo wapanga njama wakuu wa mapinduzi walikuwa ni Luteni Kanali Joseph Akahan (Kamanda, Bataliani ya 4 Kaduna), Luteni Kanali Murtala Muhammed (Mkaguzi wa mawasiliano, Lagos, ambaye kama nilivyoeleza hapo juu yeye ndiye aliyeratibu mapinduzi hayo na pia alikuja kuwa mkuu wa nchi miaka tisa baadaye kwa kumpindua Jenerali Yakubu Gowon aliyekuwa mkutanoni jijini Kampala nchini Uganda), tuatona hili baadae.

Meja Theophilus Danjuma (Principal Staff Officer, Makao Makuu ya Jeshi, Lagos), Meja Abba Kyari (Kikosi cha Mizinga, Kaduna), Meja Martin Adamu (Bataliani ya 2, Lagos),Meja Shittu Alao (Makao Makuu ya Jeshi la Anga la Nigeria, Lagos), Meja Musa Usman (Jeshi la Anga la Nigeria, Lagos), Kapteni Joseph Garba (Ulinzi wa Shirikisho (Federal Guards) Lagos), Kapteni Isa Bukar (Ulinzi wa Shirikisho (Federal Guards) Lagos), Kapteni Ibrahim Taiwo (kutoka Ngome (Garrison) Lagos Yaba), Kapteni Baba Usman GSO (Daraja la II, Makao Makuu ya Jeshi, Lagos), Kapteni Abdul D.S. Wya (Bataliani ya 3, Kaduna).

Pia walikuwepo Luteni Muhammadu Buhari (Brigedi ya 2 Lagos, huyu ndiye Rais wa sasa na pia aliwahi kumpindua Rais wa serikali ya kiraia Alhaj Shehu Shagari mwaka 1983 na kuwa Mkuu wa Nchi kisha naye kuja kupinduliwa na Ibrahim Babanginda mwaka 1985), Luteni Ibrahim Babangida (Kikosi cha kwanza cha upepelezi (1st Reconnaissance Squadron), Kaduna, Babangida naye alikuja kumpindua Mohammadu Buhari na kuwa Mkuu wa Nchi mwaka 1985), Luteni Ibrahim Bako (Bataliani ya 4, Ibadan), Luteni William Walbe (Bataliani ya 2, Lagos), Luteni Mamman Vatsa (Bataliani ya 4, Ibadan), Luteni Buka Suka Dimka (Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Nigeria Kaduna, huyu yeye ndiye aliyekuja kufanya jaribio la mapinduzi lililoshindwa na kupelekea kuuawa kwa Mkuu wa nchi Murtala Muhammad miaka kumi baadaye mwaka 1976 na yeye Dimka kuhukumiwa kunyongwa kwa kupigwa risasi mwaka huo huo wa 1976).

Pia wengine ni Luteni Yakubu Dambo (Bataliani ya 3 Kaduna), Luteni Garba A. Dada (Adjutant Bataliani ya 4 Ibadan), Luteni Garba Duba (Kikosi cha kwanza cha upelelezi (1 Reconnaissance Squadron) Kaduna), Luteni Mohammed Balarabe Haladu (Bataliani ya 4, Ibadan), Luteni Malami Mahe Nassarawa (Bataliani ya 2, Lagos), Luteni James Onoja (Bataliani ya 4, Ibadan), Luteni Abdulahhi Shelleng (Company Commander, Bataliani ya 4, Ibadan), Luteni Paul Chabri Tarfa (Ulinzi wa Shirikisho (Federal Guards), Lagos), Luteni D.S. Abubakar (Ngome (Garrison) Abeokuta), Luteni Usu Sani Abacha (Bataliani ya 3 Kaduna, yeye alikuja kufanya mapinduzi mwaka 1993 kwa kumpindua Ibrahim Babangida na kuwa Mkuu wa Nchi mpaka alipofariki mwaka 1998).

Pia orodha ya askari wengine ni Luteni Usu Muhammadu Gado Nasko (Kikosi cha Mizinga, Kaduna), Sajenti Paul Dickson, Sajenti Sabo Kwale (Ngome (Garrison) Abeokuta) na wa mwisho ni Koplo John Shagaya (Kikosi cha pili cha upelelezi (2nd Reconnaissance Squadron), Abeokuta).

Hiyo ndiyo orodha ya wanajeshi wote walioshiriki mapinduzi ndani ya mapinduzi ambayo ni maarufu kama Counter-Coup ya mwaka 1966 kwa kuiondoa madarakani serikali ya Jenerali Ironsi.

Sababu ya mapinduzi na kifo cha Generali Johnson Aguiyi Ironsi ni kisasi cha wanajeshi wa kaskazini dhidi ya kifo cha Waziri Mkuu Sir Abubakar Balewa Tafawa kama nilivyoeleza hapo juu.

Baada ya mauaji ya Generali Johnson Aguiyi Ironsi nchi ya Nigeria ikawa mikononi mwa mbabe wa vita kutoka kaskazini Jenerali Yakubu Gowon ambaye aliongoza nchi ya Nigeria kuanzia mwaka 1966 mpaka 1975, Vita vya Biafra vilitokea chini ya utawala wa Gawon, ambapo chokochoko na vita yenyewe ilianza mwaka 1966 na kumalizika mwaka 1970 kati ya makabila ya kaskazini hasa Hausa na fulani dhidi ya Igbo vilichagizwa na sababu nyingi ikiwemo visasi vya Waislamu dhidi ya wakristo, harakati za watu wa Biafra kutaka kujitenga na utajiri wa mafuta kutoka jimbo la River state.

Hata hivyo watu wa kaskazini yani jamii za Furani na Hausa bado walikuwa na kisasi na watu wa kusini hasa kabila la Igbo ambao ndio walimuua Sir Abubakar Balewa Tafawa. Katika vita hivyo zaidi ya watu millioni tatu walipoteza maisha vitani na baada ya vita kutokana na athari za kivita ikiwemo njaa, hata hivyo Jenerali Yakubu Gowon alifanikiwa kuyazima maasi ya Biafra kujitenga na mpango wa Waislamu wa kaskazini kujitenga ili wajitawale kwa mujibu wa sheria zao za kiislamu.

Pamoja na yote Jenerali Yakubu Gawon alipinduliwa tarehe 29/7/1975 wakati akiwa nchini Uganda kwenye mkutano wa 12 wa umoja wa nchi huru za Afrika ulioandaliwa na kiongozi wa Uganda kipindi hicho Iddi Amini Dada wakati huo Iddi Amini alikuwa Mwenyekiti wa umoja wa mataifa huru Afrika.

Hivyo basi........

Ilikuwa siku ya Jumanne asubuhi ya Julai 29, 1975, ambapo wakuu wa Afrika wakiwa mjini Kampala, Uganda, walipatwa na huzuni kufuatia kupokea habari za mwenzao, Yakubu Gowon, kuondolewa kwa nguvu kutoka madarakani huko mjini Lagos, Gawon aliondolewa na jeshi wakati akihudhuria mkutano wa wakuu hao wa Jumuiya ya Nchi Huru za Afrika (OAU) uliokuwa ukiendelea mjini Kampala.

Jenerali Gowon katika enzi hiyo ya utawala wake, alikuwa ni miongoni mwa viongozi maarufu barani Afrika, siku hiyo asubuhi akiwa tayari ameketi ndani ya ukumbi wa mikutano sanjari na wakuu wenzake, alipokea ujumbe wa barua fupi, maarufu kama kimemo, kutoka kwa mmoja wa wasaidizi wake kumwarifu kuhusu kuzuka hali tete nchini mwake.

Kwahiyo.........

Msaidizi huyo mahsusi aliweza kumfikia Gowon akitokea nyuma ya kiti chake na kumgusa begani, ambapo baada ya kuteta kwa ufupi alimkabidhi "kimemo" hicho, Jenerali Gowon alisoma ujumbe huo na kuonekana kupigwa na butwaa, na kuamua kuvua kifaa maaluma cha maskioni alichokuwa akitumia kupokea tafsiri ya hotuba ya Rais Idi Amin wa Uganda, aliyekuwa akihutubia wakati huo.

Baada ya kuinamisha kichwa kutafakari kwa muda mfupi, kiongozi huyo alisimama na kutoka nje ya ukumbi huo wa mkutano, nje ya ukumbi alikuta tayari habari za kupinduliwa kwake zimeenea kwa waandishi wa habari, ambao walimkabili kutaka kufahamu kulikoni, na pia nini hatima yake kuanzia hapo.

Aliwapuuza waandishi hao na kupanda ngazi kwelekea kwenye chumba kidogo maalumu cha mikutano ya faragha, jirani na ukumbi mkuu wa mkutano wa wakuu, kwa muda wa takribani dakika 20 hivi kiongozi huyo aliteta na wajumbe wa serikali yake aliokuwa ameandamana nao mjini Kampala, ambapo pia alipokea taarifa rasmi kutoka kwa ofisa mkuu wa itifaki yake.

Ofisa huyo akiwa tayari amefuatilia usahihi wa habari hizo kutoka vyanzo vya uhakika mjini Lagos, alithibitisha kuondolewa kiongozi huyo, aidha, alimhakikishia kiongozi huyo kuwa familia yake ipo salama, na kwamba mke wake na watoto waliweza kuondoka mapema kuelekea London, Uingereza, kabla ya kuzuka mapinduzi hayo, ofisa huyo alitanabaisha kuwa hali ilikuwa bado ni tete, na kwamba kulikuwa na nafasi ndogo ya kuchukua hatua za kukabili mapinduzi hayo katika hatua zake za awali.

Ofisa huyo alisema kuwa mhusika mkuu wa mapinduzi hayo alikuwa ni mkuu wa kikosi cha jeshi, kilichokuwa na jukumu la ulinzi wa makazi ya Rais huyo.

Baada ya kupokea taarifa hiyo fupi, wajumbe hao wa Gowon walijadili na kuona kuwa mazingira hayakuwa rafiki kufanya jitihada zozote dhidi ya mapinduzi hayo, Gowon alipotoka nje ya kikao hicho cha faragha aliwaambia waandishi wa habari kwamba:

"I have seen the various reports, but look gentlemen, I have no comments to make in this state...." (Kwamba, "Nimeona ripoti kadhaa kuhusiana na tukio hili, lakini hebu angalia, kwa sasa sina cha ziada kuwaeleza).

Alirejea ukumbini na kwenda moja kwa moja kwa Mwenyekiti wa Kikao cha Wakuu, yaani Idi Amin, na kuteta naye kwa ufupi kabla ya kuondoka mkutanoni kwenda hoteli aliyokuwa amefikia mjini Kampala, akiwa na msafara wake kule hotelini, kwa mara nyingine alijadiliana na wajumbe wake kwa kirefu kuhusiana na mustakabali wa hali ya mambo mjini Lagos, baadaye, aliiomba serikali ya Uganda kuwasaidia wajumbe wa Nigeria waliokuwa Kampala ili waweze kupata usafiri wa kurejea nyumbani.

Yeye Jenerali Yakubu Gawon aliendelea kusalia kwa siku kadhaa nchini Uganda, ambapo ilidhihirika kuwa hakuwa na kiasi chochote cha pesa kwa ajili ya kujikimu ugenini, ilibidi wajumbe wake na baadhi ya wakuu wenzake kumchangia fedha, ikiwemo Serikali ya Uganda ili aweze kuondoka chini humo.

Akisimulia mkasa huo, alieleza kuwa hakwenda Uganda akiwa na magunia ya fedha, kwani fedha za Nigeria zilikuwa si zake, alisema kuwa fedha za Nigeria zilikuwa ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa nchini mwake, na hazikuwa zake wala za familia yake, hata hivyo, hatimaye baada ya kupewa ufadhili na serikali ya Uganda aliweza kuondoka nchini humo kwenda kuishi uhamishoni nchini Uingereza kuungana na familia yake.

Kwahiyo basi.................

Mapinduzi hayo ya mwaka 1975 kuuondoa utawala wake ndiyo yalimuweka madarakani Brigedia-Jenerali Murtala Mohammed, ambaye kabla ya hapo alikuwa Mkuu wa Kamisheni ya Mawasiliano ya Kijeshi ndani ya jeshi la nchi hiyo.

Makamu wake alikuwa Olusegun Obasanjo, ambapo wakiwa na baraza tawala la kijeshi walianza kuongoza nchi hiyo kwa amri za kijeshi.

Murtala ndiye alifanya mageuzi makubwa, ikiwemo ya kisiasa nchini humo, kwa muda mfupi aliokaa madarakani, mojawapo ya mageuzi hayo, hususan ya kisiasa, ni uamuzi wa kuweka ukomo wa serikali za kijeshi kutawala nchi hiyo, hatua nyingine ni kuyasafisha majeshi ya nchi hiyo, kutokana na ufisadi na tuhuma mbalimbali za rushwa, uonevu kwa raia, kutojali kazi na uwajibikaji duni, Maofisa wengi serikalini walifukuzwa kazi au kustaafishwa, kwa nia ya kurejesha nidhamu kazini, katika ripoti ya uwajibishaji watumishi wa umma nchini humo, huonesha kuwa jumla ya watumishi takribani 10,000 waliondolewa kazini kutokana na tuhuma mbalimbali.

Pia, ndiye aliamua kuwa makao makuu mapya ya serikali yahamishwe kutoka mji wa bandari wa Lagos kwenda mji wa Abuja uliopo katikati ya nchi hiyo, hata hivyo, licha ya jitihada hizo na nyinginezo nyingi, serikali ya kiongozi huyo haikuwapendeza baadhi ya watu, wakiwemo baadhi ya maofisa wa kijeshi, hivyo wakaandaa njama za kumpindua mapinduzi ambayo hata hivyo yalishindwa lakini yaliweza kusababisha kifo cha Jenerali Murtala.

Jaribu la mapinduzi na kifo cha Jenerali Murtala Mohammed....

Asubuhi ya Februari 13, 1976 wakati raisi Murtala Mohammed akielekea ofisini kwake akiwa na gari moja bila ulinzi wa ziada, alishambuliwa katika makutano ya barabara mojawapo na kupoteza maisha, Maelezo ya tukio hilo huonesha kuwa ilikuwa majira saa mbili asubuhi, ambapo gari lake lilipofika katika mzunguko wa barabara za njiapanda, yalikuta askari wa usalama barabarani amesimamisha magari ili kuruhusu ya upande mwingine wa barabara.

Gari la kiongozi huyo likiwa limesimama kwenye foleni, ndipo ghafla watu 6 waliovalia mavazi maarufu nchini humo, mithili ya kanzu, walijitokeza kutoka upande mmoja wa barabara na kuchomoa bunduki za SMG kulimiminia risasi gari lake, ndani ya gari hilo aina ya Benzi alikuwemo kiongozi huyo ameketi kiti cha nyuma pamoja na mpambe wake, ambapo kiti cha mbele aliketi dereva na ofisa mmoja wa usalama, kwa mujibu wa maelezo ya ofisa huyo wa usalama ambaye ndiye pekee alinusurika kwa kujifanya amekufa, washambuliaji walifanikiwa kumuua dereva na kuwajeruhi wengine ndani ya gari hilo.

Hivyo..........

Baada ya mashambulizi hayo kutulia, huku washambuliaji wakianza kuondoka katika eneo hilo, ndipo mpambe aliwahi mno kufungua mlango ili kutaka kuwahi kutoa msaada kwa mkuu, inaelezwa kuwa washambuliaji hao waliweza kuona mlango wa gari hilo ukifunguliwa, na ndipo waliitana na kurejea kulishambulia na kuhakikisha kuwa wamekamilisha lengo lao.

Afisa huyo alieleza kuwa aliwasikia washambuliaji wakipeana taarifa za kusubiri msafara wa Obasanjo (Makamu wa Murtala), ili wamshambulie, hata hivyo, taarifa zilizosikika haraka kwenye vyombo vya habari (kuwa Murtala ameshambuliwa), ndizo zilimnusuru Obasanjo kwa vile alikuwa apite katika barabara hiyo, mara baada ya kufika wasamaria wema kuokoa, taarifa ziliweza kuenea wakati wahanga wa tukio hilo wakiwahishwa hospitali.

Hospitalini ndipo ilithibitishwa kuwa Murtala, mpambe wake pamoja na dereva wao walikuwa wamefariki pale kwenye tukio, kufuatia mauaji ya kiongozi huyo, wauaji wake wakiongozwa na ofisa mmoja aitwaye Luteni-Kanali Dimka, walikwenda kwenye kituo cha redio ya taifa kuutangazia umma kuwa serikali ya Murtala imeangushwa, kadhalika, Dimka ambaye alipata mafunzo yake ya kijeshi nchini Australia, akiongoza wenzake walikwenda ubalozi wa Uingereza mjini Lagos na kumtumia ujumbe Gowon ili aweze kurejea nchini humo kushika madaraka.

Katika ujumbe huo, walimwambia Gowon kuwa asafiri hadi nchi jirani ya Togo ili apokelewe na kwenda kushika hatamu za utawala, hata hivyo, Gowon hukanusha kuhusika katika njama za mapinduzi hayo, ingawa hivyo, wakuu wa baadhi ya vikosi vya jeshi ambavyo havikuridhia tangazo hilo la Dimka, walifanya jitihada kuweza kufika kwenye kituo cha redio hiyo ya taifa ambacho kilikuwa chini ya waasi.

Amri ilikuwa kwamba endapo waasi hao wangegoma kujisalimisha na kusitisha matangazo yao ya mapinduzi, kituo hicho kingepigwa kwa makombora na kusambaratishwa bila ajizi, kuliwasili kikosi maalumu chenye vifaru nje ya jengo hilo kikiongozwa na Ibrahim Babangida, kulisababisha akina Dimka kutoroka, kumbuka kuwa miaka ya baadaye kuanzia 1985 hadi 1993, Babangida akiwa Jenerali alikuwa Rais wa 8 wa Nigeria.

Hata hivyo...........

Babangida ushutumiwa kuwa mwaka huo wa 1976 akiwa rafiki yake Dimka, alihusika kumwezesha kutoroka kiongozi huyo wa jaribio hilo la mapinduzi, wakati akitoroka, Dimka akisaidiwa na rafiki yake wa kike alifaulu kukwepa vizuizi kadhaa vya upekuzi wa kijeshi hadi alipokamatwa akikaribia kuvuka mpaka wa nchi hiyo na nchi jirani ya Cameron.

Aidha, katika kesi dhidi ya wahusika wa jaribio hilo lijulikanalo kama la mapinduzi ya Dimka, yeye mwenyewe Dimka alihukumiwa kifo, huku mwanamke aliyekuwa akimtorosha alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani, kufuatia kifo cha Murtala, baadaye wakuu wa kijeshi walifanya mkutano wao na kumteua Luteni-Jenerali Olusegun Obasanjo kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo.

Kabla ya uteuzi huo Obasanjo alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la nchi, ambalo husifika kuwa na askari wengi wasomi waliopata mafunzo yao nje ya nchi hiyo, msako mkali ulioanzishwa na vyombo vya usalama uliweza kuwakamata watu 125, akiwemo Waziri wa Ulinzi, Meja-Jenerali Iliya Bisala, katika mchujo uliofanywa na Mahakama ya Kijeshi ya nchi hiyo, jumla ya askari 31 na raia mmoja walidaiwa kupatikana na hatia ya kupanga jaribio hilo na kuhukumiwa kifo, raia aliyehukuliwa kifo ni mwandishi wa habari katika kituo cha redio ya taifa, ambaye ilidaiwa kuwa aliwapa ushirikiano askari waliovamia kituo hicho kutangaza mapinduzi hayo dhidi ya serikali ya Murtala.

Watuhumiwa wote hao 32, waliuawa kwa kupigwa risasi hadharani mwaka huohuo wa 1976, aidha, kutokana na mapenzi ya wananchi wa nchi hiyo kwa kiongozi huyo, ndio sababu ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa nchini humo ukapewa jina lake kama kumbukumbu maalumu, uwanja huo uliopo mjini Lagos, unafahamika kwa jina la ''Murtala Mohammed International Airport' (MMIA).

Hivyo basi..............

Baada ya mauaji ya Jenerali Murtala Mohammed Ramat nchi ya Nigeria ilienda chini ya mnadhimu Mkuu wa majeshi Chief Olusegun Matthew Obasanjo ambaye aliiongoza Nigeria kuanzia mwaka 1976 mpaka 1979, Mwaka 1979 ulifanyika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambapo Shehu Usman Aliyu Shagari, alishinda uchaguzi, utawala wa Shehu Shagari ulikumbwa na kashfa nyingi za rushwa, madawa ya kulevya na urasimu huku ahadi zake kwa Waislamu zikawa ni hewa, mwaka 1983 Shehu Shagari alikuwa anatetea nafasi yake ya uraisi, katika uchaguzi huo udini ukanda na ukabila vilitawala sana Nigeria.

Matokeo ya uchaguzi yalipo tangazwa Shehu Shagari alishinda kwa matokeo ya udanganyifu yaani asilimia 47.5% huku Chief wa kabila la Yoruba Obafemi Awolowo akipata 31.2% na Rais wa kwanza wa Nigeria Dr Nnamdi Azikiwe akipata asilimia 14%, waangalizi wa uchaguzi walidai kwamba uchaguzi huo ulikuwa na mapungufu mengi sana kwa sababu baadhi ya vituo vya kura kura hazikuhesabiwa, Katika uchaguzi huo kanisa la Katoliki liliweka nguvu kwa Chief Obafemi Awolowo na Dr Nnamdi Azikiwe ingawa Azikiwe alikuwa akizomewa na Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria kwamba huenda alihusika na kifo cha Waziri wake mkuu Sir Abubakar Balewa Tafawa januari 15 1966.

Baada ya Waislamu kugundua kwamba kanisa la Katoliki limeweka fedha kwa Awolowo na Azikiwe ikabidi wamchagua muislamu mwenzao Shehu Shagari ingawa walikuwa hawamtaki.

Hata hivyo.............

Tarehe 31/12/1983 Raisi wa Nigeria Shehu Shagari alipinduliwa na Jenerali Muhammadu Buhari (ambaye ni raisi wa sasa wa Nigeria) Generali Buhari alihitilafiana na serikali ya Shehu Shagari Kuhusu mzozo kati ya Nigeria na Chad kwenye mzozo wa mipaka ambapo Jeshi la Chad lilitaka kuchukua eneo hilo chini ya Jenerali Hissen Habrew mbabe wa vita.

Jenerali Muhamad Buhari aliiongoza Nigeria kwa miaka 2 kuanzia tarehe 31/12/1983 mpaka tarehe 27/8/1985 Jenerali Buhari aliongoza Nigeria kijeshi huku akijitahidi kukuza uchumi na uzalishaji, aliamua kuanza vita dhidi ya wahujumu uchumi na wanasiasa walioficha fedha ughaibuni, Buhari alishauri Jeshi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima hali hiyo ikapelekea sintofahamu nyingi kati ya Jeshi na serikali ya Nigeria, hatimae tarehe 27 /8/1985 Jenerali Muhammad Buhari alipinduliwa na Jenerali Ibrahim Badamas Babangida.

Babangida nae aliongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1985 mpaka alipojiuzulu mwaka 1993 ambapo alimteua Mwanasheria Oloye Ernest Adegunle Shonekan kuwa Raisi wa nchi hiyo kuanzia tarehe 26/8/1993 mpaka alipopinduliwa tarehe 17/11/1993 na Jenerali San Abacha ambae alichukua nchi kijeshi kuanzia mwaka 1993 mpaka alipo fariki dunia gafla kwenye ikulu ya Villa Park huko Abuja mwaka 1998.

Tarehe 8/6/1998 Jenerali San Abacha alikufa kifo cha utata akiwa ikulu na alizikwa bila mwili wake kufanyiwa uchunguzi yaani autopsy, ipo dhana inayo husisha kifo cha Abacha, dhana hiyo inaeleza kuwa Jeshi la Nigeria, yani Jenerali Abubakar akiwemo, waliamua kumuua Abacha ili kuruhusu mwanzo mpya wa kusuka amani ya Nigeria, kwani hali ilikuwa mbaya na wasiwasi ulikuwa mkubwa mitaani kutokana na mvutano mkubwa uliokuwepo baina ya Abacha na Abiola, hivyo jeshi la nchi likaamua kuwaua Abacha na Abiola kwani inatajwa kuwa kipindi cha vifo vya Abacha na Abiola wametofautiana siku 29 tu, na wote vifo vyao vimejaa utata.

Baada ya kifo cha Generali San Abacha, Generali Abdulsalami Abubakar akaongoza Nigeria kwa muda yaani kuanzia mwaka 1998 mpaka mwaka 1999.

Jenerali Abdisalami Abubakar ambaye alianza kazi kwa kuwashughulikia wasaidizi wa Abacha, akiwemo Meja Mustapha ambaye alifukuzwa kazi na kunyang’anywa hati ya kusafiria. Pamoja na hivyo, Jenerali Abubakar analaumiwa kwa kuchelewa kuchukua hatua za haraka kumtoa gerezani Abiola, hivyo kusababisha mauti yamfike.

Basi......

Jenerali Abdisalami Abubakar aliongoza nchi mpaka mwaka 1999 ambapo aliitisha uchaguzi mwingine wa kidemokrasia, katika uchaguzi huu Obasanjo alishinda kwa asilimia 62.5% kupitia chama cha People’s Democratic Party, Utawala wa Obasanjo ulianzia mwaka 1999 mpaka 2007 ambao ulifanyika uchaguzi mwingine wa kidemokrasia na Umaru Yaradua wa chama hicho hicho cha Obasanjo alishinda lakini alifariki akiwa madarakani mwaka 2010 na makamu wake Goodluck Ebele Jonathan kuchukua nafasi ambae nae alishindwa kutetea kiti chake katika uchaguzi wa March 2015 ambapo Muhamadu Buhari kutoka chama cha All Progressives Congress (APP) alishinda katika uchaguzi huo, na kumshinda mpinzani wake ambae alikuwa ni raisi aliyekuwa madarakani, na kufanyia kuwa mara ya kwanza nchini Nigeria rais aliye madarakani kukubali kumpisha mshindi katika uchaguzi wa kidemokrasia.

Lakini pia....

Buhari alishinda tena uchaguzi wa February 2019, ambapo Buhari alichaguliwa tena na kumshinda mpinzani Atiku Abubakar kwa ushindi wa tofauti ya kura 3 millioni.

PS:CREDITS/ACKNOWLEDGEMENTS
------------------------------------------------------------
1- Kperogi, Farooq (22 January 2016). "Gere: Sir Abubakar Tafawa Balewa's Real Ethnic Group".
2- Omotola, Balogun (10 November 2017). "BIOGRAPHY OF SIR ABUBAKAR TAFAWA BALEWA, KBE".
3- Sani., Umar, Muhammad (2006). Islam and colonialism : intellectual responses of Muslims of Northern Nigeria to British colonial rule. Leiden: Brill.
4- Joseph, Richard (6 February 2014). Democracy and prebendal politics in Nigeria : the rise and fall of the Second Republic.
5- Maka Patrick Mwasomola, kutoka makala yake ya "Mapinduzi ndani ya Mapinduzi ya Nigeria 1966"
6- Lugete Gulu Maester, kutoka makala yake ya "Chimbuko la Boko Haram na historia ya Nigeria"

Ukinakili kazi zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
Wako Mjoli wa Historia na diplomasia ya ulimwengu.

Ndimi: Comred Mbwana Allyamtu
Copyrights of this article reserved
written by Comred Mbwana Allyamtu
•Napatika Kwa mawasliano
Comred Mbwana Allyamtu
Kwa Tanzania
+255679555526.
+255765026057.

Kwa Rwanda
+250733153930
+250788214234

Kwa DRC
+243 977 860 824
Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com

Copyright 2020, All Rights Reserved.

Maktaba Kuu
IMG_20200613_200542.jpeg
 
Ah siku ya leo naianza vizur sana kwa hisani ya andiko lako comrade mbwana!nimekumbuka mbali sana na nimekumbuka watu wengi sana ambao wengi wao wapo mbele ya haki kutokana na kupoteza uhai wakati wakitekeleza majukumu ya kuijenga&kuilinda nchi hii!!!pia nimejikuta naikumbuka isman(iringa) ya wakat ule ambayo ilizalisha maindi ya kulisha nchi nzima.
#Farm 17
#5th Reconnaissance Squadron(X)
#Mission Fort ikoma 199X
 
Murtala Muhammed alikuwa kiongozi anaejua jinsi ya kuongoza ingawa tabia ya kutaka kuonekana shujaa imemponza haiwezekani kwa akili timamu na hali ilivyokuwa Nigeria yeye akawa anataka kutembea na magari manne tu halafu akawa anataka kuwa msafara wake unasimama kwenye foleni
 
Rais wa Nigeria, Dk. Nnamdi Azikiwe yeye aliondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka 1965, kwanza akienda barani Ulaya, kisha akasafiri kwa meli ya kifahari kwenda kula "bata" huko Caribbean
Asante sana.
Lakini,
Ilikuwaje, huyu ndugu tukampa mtaa kwa kuupachika jina lake pale mkoani Dar es Salaam , wakati aliwaacha wanajeria kwenye msukosuko na yeye kwenda kula " bata"?

Mwanahistoria ebu shusha nondo juu ya hili.
Ingawa nimepitia uzi bandiko lako kwa haraka, haujagusa kabisa habari za "biafra"!
 
Kwanini mapinduzi yamepungua siku hizi?
Matukio mengi ya mapinduzi ya kijeshi barani Afrika yalikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na vita baridi baina ya ngome ya mashariki (USSR) na magharibi (USA-NATO), ndio maana kuanzia miaka ya 1990s na kuvunjiaka kwa umoja wa Soviet sijawahi tena kusikia mapinduzi ya mara kwa mara huku Afrika.
 
Shukrani sana. Mada yako imenikumbusha mbali sana miaka ya 1990 ambapo Mada kama hii mimi na wenzangu tuliitumia kwenye Project yetu ya kidato cha sita ikiwa na kichwa cha habari "Military coups as a cause of political instability in West Africa: The Case of Nigeria".
 
Matukio mengi ya mapinduzi ya kijeshi barani Afrika yalikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na vita baridi baina ya ngome ya mashariki (USSR) na magharibi (USA-NATO), ndio maana kuanzia miaka ya 1990s na kuvunjiaka kwa umoja wa Soviet sijawahi tena kusikia mapinduzi ya mara kwa mara huku Afrika.


Mkuu Infantry soldier mapinduzi hata hapa TZ yanaweza kutokea au popote pale barani Africa ikiwa mataifa husika hayajipanga kukabiliana nayo

Mapinduzi hayatokei sana siku hizi sababu nchi nyingi zimesha adopt sheria za kimfumo na weledi wa kupambana na matukio hayo although nakubaliana nawe kuwa Vita baridi ilichangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa mapinduzi mara kwa mara
 
12 Reactions
Reply
Back
Top Bottom