Siku ya tukio Ludovick alikuwa na Mjengwa. Alitoa maelezo yake mwenyewe facebook. Kawaida kwenye matukio ya namna hii Mjengwa ndie angekuwa wa kwanza kuunganishwa naye kadiri ya maelezo ya Ludovick mwenyewe.
.
'Leo usiku, yapata saa tano na nusu, niliachana na Maggid Mjengwa maeneo ya Shekilango tukitokea Rose Garden. Yeye alielekea hotelini alikofikia sehemu fulani Kariakoo nami nikasubiri kigari kuelekea nyumbani kwangu.
Hapo Shekilango, magari yalichelewa kidogo, pembeni ilipaki bajaji ikiwa na watu wawili na dereva ndipo wakaniambia twende tuchangie mia tano tu kwenda Ubungo Mataa, nikakaa katikati ya hao jamaa.
Ghafla wakakata kona na kuanza kuelekea Mabibo huku wakiulizana kama wako kamili na mwingine kujibu yuko kamili. Nikajua tayari niko mikononi mwa majambazi na sikujua wako kamili namna gani, kwa hiyo nikaamua kuwa mtulivu.
Tulipofika relini karibu na Mabibo wakanipokonya begi lakini, hawakulifungua. Ndani yake kulikuwa na laptop, toshiba kubwa na chaji yake, kamera ndogo ya digital na USB yake, modem ya zantel na card reader. Tulipofika maeneo ya Loyola Sekondari, nikawasihi wanishushe ili nirudi mwenyewe, wakaniambia safari ile inaishia Jangwani.
Nikaingiwa na wasiwasi mkubwa na nia yao hasa, maana wameshanipokonya begi kwa nini wasiniachie? Lakini niliendelea kuwa mtulivu ili kutowaprovoke.
Tulipovuka Kigogo mwisho kwenye giza karibu na msikiti, wakasimama pembeni ya barabara na kuniamuru kushuka, nikashuka na kuanza kuwadai begi langu, ndipo mmoja akasema wamekuwa wastaarabu mimi naanza kuwadharau. Ghafla akanivuta kwa nguvu kunirudisha kwenye kibajaji akamwambia mwenzie wanisachi kama nina vitu vingine, wakanisachi na kuchukua pesa, nilikuwa na elfu 35 na simu mbili ndogo za nokia moja yenye line mbili.
Kisha mmoja akatoa ‘order' nivuliwe nguo. Nikavuliwa viatu, T-shirt na suruali nikabaki na nguo za ndani pekee. Wakanishusha na kuniacha hapo.
Kurudi nyuma kama hatua kumi tu ndipo kituo kidogo cha polisi Kigogo nikaanza kutoa maelezo hapo kwa zaidi kama ya saa mbili nikiwa uchi na nguo za ndani tu. Nikiwa hapo nikasikia polisi wakiwasiliana juu ya tukio la kupigwa vibaya Absalom Kibanda, kwenye redio calls.
Ilikuwa yapata saa nane, baada ya kuchukuliwa maelezo polisi walinipatia gari nikaelekea hotelini kwa Maggid, ambaye saa kumi aliamshwa na kunichukulia chumba hapo nikapumzika. Ameniazima nguo zake ndizo nimevaa bado hadi sasa naelekea kituo cha Polisi Magomeni kwenda kupewa mpelelezi wa kesi yangu. Namba ya kesi yangu Kigogo ni KIG/RB/318/2013, wizi kutoka maungoni.'
Wakati Ludovick akiwa ametoa maelezo hayo kwa jamii kupitia mitandao ya kijamii, polisi wameshindwa kuthibitisha taarifa za kutekwa, kuporwa na kupokea taarifa yake aliyodai kuitoa kituo kidogo cha polisi Kigogo.
Polisi katika kituo kidogo cha Kigogo waliohojiwa na MTANZANIA Jumapili kuhusiana na taarifa za Ludovick, walionekana kurushiana mpira kuzizungumzia.
Wapelelezi walio mahiri wangeunganisha Ludovick alikuwa na nani siku hiyo kabla ya tukio na baada ya tukio.
Tumeona mara baada ya tukio hilo Ludovick alienda Iringa kwa kuitwa na Mjengwa, na Polisi walimkamata akiwa Iringa kwa kazi za Mjengwa.
Ndugu zangu,
Usiku huu nikiwa kwenye shughuli ya shule ya watoto wangu pale Highlands Hall Iringa nilifikiwa na habari kuwa Kijana Ludovick amekamatwa na polisi kuhusiana na tuhuma za kuhusika na kuteswa mwandishi Absalom Kibanda.
Namfahamu kijana Ludovik tangu akiwa Chuo Kikuu ( DUCE). Ni mmoja wa Watanzania wengi walionifahamu kupitia kazi zangu za magazetini.
Kwangu Ludovick ni kijana mtaratibu na mpole sana, na hata niliposikia habari hizi kwa namna fulani nimeshtushwa nazo.
Ludovick ambaye amekuwa akiishi Dar ni mmoja wa vijana waliokuwa wakinisaidia kwa kujitolea kwenye kazi zangu za mitandaoni, hususan kwenye Mjengwablog na website ya Kwanza Jamii. Amekuwa na mchango mkubwa, na hata katika miezi ya karibuni,ndiye yeye aliyekuwa akifanya kazi ya kuingiza magazeti kwenye Mjengwablog kila asubuhi.
Akiwa Dar na mimi nikiwa Iringa, Ludovick hakuwa mwajiriwa wangu kama wanavyodhani wengine, bali , amekuwa ni mmoja wa vijana waliokuwa tayari kunisaidia kwa kazi za hapa na pale ikiwamo kunipelekea invoice kwa watangazaji kwenye Mjengwablog.
Mara nyingi nimekuwa nikimtambulisha kama ' Msaidizi wa Mwenyekiti'.
Na jana nilimwomba aje Iringa aniletee vitabu vyangu vya invoice na risiti kwa vile nilitarajia ugeni wa kutoka TMF- Mfuko wa Ruzuku kwa vyombo vya habari. Kwamba huenda vitabu hivyo vingehitajika wakati wa mazungumzo na watendaji wa TMF yaliyofanyika leo asubuhi.
Hata hivyo, katika hili lililomtokea, siwezi hapa kumtetea wala kumtia hatiani. Maana, naye ni binadamu kama wengine, siwezi kusema kuwa ninamfahamu sana. Kwa vile yuko mikononi mwa vyombo vya usalama , nina imani, kuwa vyombo hivyo vitafanya kazi yake ili kutusaidia katika kupata ukweli wa jambo zima.
Na kama ni kweli kwa namna yoyote ile itathibitishwa kuwa ameshiriki njama za kupanga mikakati hiyo ya kigaidi, basi, ahukumiwe kwa dhambi hiyo.
Ni mimi:
MAGID MJENGWA
Credit: Mjengwablog
Hatimaye Mjengwa alitoa tamko rasmi
TAARIFA RASMI KUTOKA Mtandao Wa Kijamii Wa MJENGWABLOG
Sunday, 17 March 2013 | Written by Mjengwa Blog
Ndugu zangu,
Kutokana na kuwepo kwa taarifa rasmi za kipolisi zenye kumtuhumu Ludovic Joseph kuhusika na matukio ya kigaidi.
Uongozi wa Mtandao wa Kijamii wa Mjengwablog unasitisha rasmi, kuanzia leo Jumapili, Machi, 17,2013, kuwa na Ludovick Joseph kama msaidizi wa Mtandao wa Kijamii wa Mjengwablog na website ya Kwanza Jamii.
Maggid Mjengwa,
Mmiliki wa Mjengwablog /Kwanzajamii
Kwa hiyo Ludo alikuwa ana shughuli nyingi tu. Chadema alikuwa Volunteer, kwa Mjengwa alikuwa Msaidizi wa Blog.
Katika tukio la Kibanda sijui wapi pa kuanzia uchunguzi hapo, yule waliyekuwa naye siku hiyo na ambaye baadaye alimwita Iringa au kule ambako ni volunteer!
Tafakari mwenyewe na usiache akili ya mwingine ikuamulie