Bakwata yapingana na maaskofu kuhusu OIC
Basil Msongo
Daily News; Saturday,October 25, 2008 @19:01
Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), limesikitishwa na kauli ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na kuwataka maaskofu waache kupotosha lengo sahihi la serikali la kujiunga katika Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) kwa kuwa taasisi hiyo si ya kidini.
Bakwata imeeleza kuwa ilichokisema maaskofu ni dhana na wasiwasi usio na msingi kwa kuwa hadi sasa wameshindwa kuthibitisha kuwa OIC imeleta mtafaruku wa kidini katika nchi zilizojiunga na jumuiya hiyo. Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Ally Mzee alisema jumamosi Dar es Salaam kuwa maaskofu hao hawana mamlaka au uhalali wa kuzuia jamii moja au nyingine isizungumzie jambo ambalo wao wanaliona ni muhimu.
"Bakwata inawataka maaskofu hawa waache tabia ya kuonyesha kuwa wao pekee ndio wana mamlaka ya kuiendesha serikali na viongozi wake kwani serikali na viongozi wamewekwa madarakani na Katiba ya nchi," Mzee aliwaambia wanahabari katika ofisi za Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni. Alisema Waislamu hawana tatizo na Wakristo na wamekuwa wakishirikiana, lakini kauli ya maaskofu inaleta hisia kuwa huenda kuna jambo limejificha.
"Tunachohitaji kukiangalia ni maslahi ya taifa na sio vinginevyo na sisi wakati wote tumekuwa tukiwasihi Waislamu wawe wavumilivu," alisema na kutoa mwito kwa viongozi wa dini wamrudie Mwenyezi Mungu, wahubiri umoja na mshikamano. Kwa mujibu wa Mzee, zipo nchi ambazo si za Kiislamu, zimejiunga na OIC na hazijageuzwa kuwa za Kiislamu hivyo maaskofu waache kupotosha kwa misingi ya kidini.
"Sasa tusiingize suala la udini kwenye maslahi ya taifa, sisi ni viongozi wa kiroho, tusiwafanye waumini wetu wakawa na wasiwasi badala ya kuwaondoa wasiwasi," alisema kiongozi huyo wa Bakwata. Kwa mujibu wa Mzee, OIC ni taasisi ya kimataifa kama taasisi nyingine na si taasisi ya kidini na akahoji kwa nini wanaopinga kujiunga na jumuiya hiyo hawapingi ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Waislamu (IDB).
"Kauli ya maaskofu hawa inapotosha lengo sahihi la serikali la kuletea wananchi wake maendeleo, na kuligeuza kuwa suala la kidini. Katika kufanya hivyo maaskofu hawa wanaweza kuamsha hisia za mtafaruku wa kijamii na kidini," alisema Mzee wakati akisoma tamko la Bakwata.
Baraza hilo limeiomba serikali iendelee na mpango wa kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuendelea na mchakato wa kujiunga na OIC na limemshauri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe asijiuzulu.
"Bakwata inaipongeza serikali kwa kufuata taratibu za kikatiba na utawala bora, hivyo baraza linamshauri Mheshimiwa Membe asijiuzulu kwa shinikizo la maaskofu hao kwa kisingizio cha udini kwani kujiuzulu kwake kutaigawa nchi," ilisema sehemu ya tamko la baraza hilo.
Katika tamko hilo, Bakwata pia imepinga msimamo wa maaskofu kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi kwa kusema kuwa mahakama hiyo ni suala la ibada kwa Waislamu na wala halina mjadala. Juzi, CCT ilimtaka Membe aache kuzungumzia suala la OIC na endapo anataka kuendelea kulipigia debe ajiuzulu. Maaskofu hao walidai kuwa pingamizi lao si la chuki ila wanazuia uwezekano wa taifa kugawanyika endapo Tanzania itajiunga na OIC na kwamba hilo likifanyika, pia Katiba ya nchi itavunjwa.