SoC03 Jinsi ninavyofaidika na uzalishaji wa hizi bidhaa nilizojifunza mtaani kuliko Elimu yangu lakini tatizo ni kwamba ...

Stories of Change - 2023 Competition

DON YRN

JF-Expert Member
Jan 14, 2019
474
999
Jina langu naitwa DON YRN. Mwaka 2012 nilihitimu elimu yangu ya kidato cha nne katika mkoa mmoja wapo ndani ya nchi yetu. Matokeo ya mtihani hayakuweza kufikia kiwango cha mimi kuingia kidato cha tano hivyo kulingana na shinikizo na ushauri mbalimbali wa wazazi, ndugu na jamaa niliamua kuangalia ustaarabu mwingine kama kutafuta nafasi ya chuo cha ualimu wa shule ya msingi kilichopo mkoani Mwanza. Ni kweli nafasi ya kwenda chuo binafsi cha ualimu ilipatikana lakini kipengele kikawa ni ada yake kuwa kubwa kuliko uwezo wa wazazi wangu hivyo nafasi ya kwenda chuo ilifeli. Binafsi nilifurahi kutokwenda Chuo cha ualimu kwa sababu ualimu siyo kazi niliyokuwa nikiipenda na wala siyo wito wangu(ualimu ni wito).

NAFASI NYINGINE YA KUSOMA CHUO YAPATIKANA JIJINI DAR ES SALAAM.
Baada ya kukaa kwa muda wa miaka miwili pale nyumbani bila shule (2013 & 2014) huku nikikusanya hela iliyotokana na kilimo na vibarua mbalimbali, nilipata nafasi ya kujiunga na chuo kimojawapo kilichopo mkoani Dar es Salaam kwa ngazi ya Astashahada ya sheria kwa mwaka wa masomo 2015/2016. Nilijiunga na chuo huku nikiamini mambo yangekuwa rahisi, haikuwa rahisi. Nilihitimu masomo yangu baada ya mwaka mmoja nikapata matokeo ya GPA 2.5.

Baada ya kuhitimu, sikuwa na chaguo zaidi ya kuanza kupambana tena mtaani jijini Dar es Salaam ili nipate ada ya kuendelea na stashahada lakini sikupata zaidi ya kupata hela ya matumizi madogo madogo tu.

NAFASI NA KAZI YA KUJIFUNZA KUTENGENEZA NA KUZALISHA MIKANDA YA GYPSUM YAPATIKANA.
Katika kutangatanga huku na kule kutafuta kazi zozote ila kuna siku nilifanikiwa kupata nafasi ya kujifunza kutengeneza mikanda ya jipsam(gysum)(2019). Niliwakuta vijana watatu wakiwa wafanyakazi kwa mwajiri mmoja, wahitimu wa darasa la saba na hawa vijana ndio walinifundisha namna ya kutengeneza na kuzalisha mikanda ya Jipsam(Gypsum) kwa muda wa wiki nne(4) tu. Mikanda ya Gypsum ni mikanda inayowekwa au ndani ya nyumba kama urembo kwa kutumia ufundi maalum ili kupendezesha nyumba.

Ni miaka minne sasa nafanya hii kazi yangu na hata mabadiliko ya kiuchumi nayaona ikiwa ni pamoja na kusaidia ndugu na wazazi wangu. Ni kazi inayonifanya nilipe kodi mbalimbali, ujenzi na hata kulipia ada za shule kwa wadogo zangu.

Faida nyingine ni kwamba nimekuwa mtegemewa zaidi kwa wahitaji wa kuzalishiwa bidhaa, sihitaji kwenda kutafuta kazi bali waajiri ndio wao hunitafuta ili niwazalishie bidhaa.
Elimu yangu ya kidato cha nne na chuo haijanisaidia kwa lolote mpaka sasa zaidi ya kupoteza muda tu.

20230720_112916.jpg

20230707_071141.jpg
20230720_112553.jpg
20230707_071253.jpg
20230707_071201.jpg
Baadhi ya mikanda ya Gypsum ambayo huwa nazalisha.

FURSA ZA KUJIFUNZA KAZI MBALIMBALI ZA UJASIRIAMALI YAPATIKANA.
Kuna siku nilikuwa napitia kwenye mtandao wa Instagram nikaona tangazo la mafunzo ya kujifunza kazi mbalimbali za ujasiriamali wa kutengeneza bidhaa kama Sabuni za magadi, sabuni za vipande, sabuni za kusafishia marumaru(tiles), batiki, sabuni za unga, jiki, sabuni za kuogea, n.k. Niliamua kufuatilia namna ya kujiunga na yale masomo nikafanikiwa.

Masomo yalikuwa yakifundishwa kwa njia ya mtandao wa WhatsApp na hadi muda huu naandika andiko langu hili, bado nazidi kujifunza. Kwenye yale mafunzo nilikutana na watu mbalimbali ambao huwa wanafanya ujasiriamali wa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama nilivyoziorodhesha hapo awali hivyo kusaidia kuongeza uelewa zaidi. Wengi wa wanafunzi ni wahitimu wa vyuo vikuu.

Kwa sasa nimeweza kufanya majaribio ya kutengeneza aina mbalimbali za batiki kama batiki za kuchovya na kufinyanga ambazo hutumia mchanganyiko wa Maji, Caustic soda, Sodium hydrosulphate na rangi ya batiki.

Pia, nimeweza kujifunza namna ya kutengeneza sabuni za magadi ambazo mchanganyiko wake ni maji, mafuta ya mawese/mise, Caustic soda(kemikali), Sodium silicate(kemikali) na rangi ya sabuni(Hii nimeamua niiweke pembeni kwanza hadi nijiridhishe na kushirikisha wataalamu zaidi).

Kwa sasa nipo naendelea kujiimarisha zaidi kwenye ujasiriamali wa kuremba batiki maana ndiyo nimeamua nifanye .

20230719_104401.jpg
20230719_104207.jpg
20230719_104531.jpg
20230719_103954.jpg
Baadhi ya batiki nilizojifunza kuremba.

NINI KIFANYIKE?.
Ni kweli suala la ukosefu wa ajira limekuwa sugu katika jamii, ajira za serikali na sekta binafsi hazitoshelezi kwa maelfu ya vijana wanaohitimu masomo yao ya elimu za kati na vyuo vikuu kila mwaka.

Lengo la elimu kwa dunia ya sasa, ni msomi afaidike na elimu yake aliyoisotea kwa miaka mingi yaani elimu iwe kitega uchumi cha kumuingizia pesa, kinyume na hapo ni mateso.

Kulingana na mabadiliko ya mazingira na ongezeko la watu nchini, siyo vijana wote watatoshea kwenye ajira bali inatakiwa iwepo mbinu mbadala kwenye elimu ya kumwezesha kijana asitegemee kuajiriwa bali ajiajiri.

Hebu fikiria, kuna haja gani ya mtu kusoma hadi chuo kikuu na kusomea uhasibu halafu baada ya kuhitimu masomo anarudi mtaani kujiajiri kwa kutengeneza mikanda ya gypsum, sabuni au kuremba batiki na ikawa kazi ya kumuingizia kipato kuliko kile alichopoteza miaka mingi kusomea?!. Hii haileti maana na siyo jambo la kujivunia kwamba kijana kajiajiri baada ya kuhitimu chuo kikuu.

Ni bora kukawepo na vyuo vinavyofundisha kwa weledi masuala ya ujasiriamali na utengenezaji wa bidhaa ndogo ndogo kama sabuni mbadala wa VETA kuliko ilivyo sasa watu kujifundisha mtaani.

Hii inaweza pia kupewa kipaumbele hasa kwa wanafunzi wanaofeli kidato cha nne kuliko ilivyo sasa wakifeli wanakuwa mtaani matokeo yake ni vijana kujihusisha na makundi ya kihalifu na utumiaji wa dawa za kulevya.

Wakifundishwa elimu ya ujasiriamali na utengenezaji wa bidhaa, baada ya kuhitimu Serikali inaweza kupata vibali na kuwawezesha mikopo ya riba nafuu ya kufungua viwanda vidogo serikali ikapata faida, kodi, kupungua kwa uagizaji wa baadhi ya bidhaa nje ya nchi na kupata fedha za kigeni kutokana na watu wa nje kununua bidhaa nchini kwetu.

Leo hii, bidhaa nyingi za matumizi ya kila siku kama mafuta ya kujipaka, sabuni za kuogea, mafuta ya nywele, n.k., zisizo na kiwango ambazo hazijathibitishwa kitaalamu zimetapakaa kwenye maduka na zinanunuliwa.

Watu wanajitengenezea tu huku mtaani pasipokuwa na ujuzi maalum wa Kisayansi kwa kigezo na kivuli cha "WAJASIRIAMALI WADOGO". Hebu fikiria, mtu anajifunza leo kutengeneza mafuta kwa njia ya whatsApp, baada ya siku tatu eti tayari kaelewa kutengeneza na anaenda kutafuta malighafi zake Kariakoo anakuja kutengeneza, siku ya nne tayari kaingiza bidhaa sokoni!.

Kwa mtindo huu, magonjwa ya ngozi na saratani hayawezi kuisha sababu watu wanatumia sumu.

Wako katika ujenzi wa Taifa,
DON YRN.
 
Back
Top Bottom