TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI, OKTOBA 26, 2015
CCM inapenda kutoa taarifa
ifuatayo kwa wanachama,
wapenzi na washabiki wake
na kwa umma Watanzania.
Tathmini ya Upigaji Kura
Kama tulivyoeleza jana,
tumeridhishwa na amani na
utulivu uliotawala katika
sehemu kubwa ya nchi yetu
wakati wa zoezi la upigaji
kura. Licha ya changamoto
zilizojitokeza, ambazo
baadhi zimeshughulikiwa,
kwa jinsi zoezi la kupiga na
kuhesabu kura
lilivyoendeshwa kwa uwazi,
matokeo ya uchaguzi huu
yatakuwa ni kielelezo cha
utashi halisi wa Watanzania
na kutakuwa hakuna sababu
ya mtu yoyote kukataa
matokeo.
Kupokea na Kutangaza
Matokeo
Kipindi cha kupokea na
kutangazwa matokeo ni
muhimu kama ilivyo kipindi
cha kampeni na siku ya
kupiga kura. CCM inahimiza
utulivu kwa wafuasi wake na
wananchi kwa ujumla na
kuziachia mamlaka husika
zifanye kazi yake. Katika
kipindi hiki, kazi za vyama ni
kupokea matokeo na na kazi
ya Tume ni kutangaza
matokeo.
Tunasikitishwa na
propaganda zinazoendeshwa
na wapinzani wetu kuhusu
matokeo ya uchaguzi.
Tunaona matokeo
yanayotangazwa na wafuasi
wa vyama vya upinzani, hasa
mitandaoni. Bahati nzuri,
propaganda hizi zinakosa
maarifa kiasi cha kutoa hata
matokeo ya Ubunge katika
majimbo ambayo uchaguzi
wa Wabunge haukufanyika,
mfano Handeni na Masasi.
Tunawataka wana-CCM
wapuuze matokeo
yanayotembezwa kwenye
mitandao ya kijamii.
Matokeo rasmi yatatolewa
na Tume. Bahati mbaya
sana, wenzetu wanatoa
matokeo ya uongo mapema
ili Tume ikitoa matokeo
rasmi waseme wameibiwa
kura na kutafuta kisingizio
cha kuingia mitaani na
kufanya vurugu. Pia
tunabaini jitihada na nguvu
kubwa za wapinzani wetu
kupeleka kilio chao kwa
waandishi wa habari wa nje
ya nchi pamoja na mataifa
ya nje kwa ujumla.
Wameajiri magwiji wa
propaganda kutoka nje ya
nchi kwa fedha nyingi
kujenga taswira kwenye
Jumuiya ya Kimataifa
kwamba Tanzania ni kama
nchi nyingine yoyote ya
Kiafrika ambapo hakuna
ustaarabu wala utaratibu wa
kidemokrasia na Serikali
hukandamiza watu wake.
Mkakati wao ni kuitaka
Jumuiya ya Kimataifa itumie
nguvu yake ya misaada kwa
nchi yetu kulazimisha
matokeo ambayo hayatokani
na utashi wa Watanzania.
CCM haitalikubali jambo hili.
Matokeo ya CCM
Kwa kuwa matokeo kwenye
vituo vya kupigia kura
matokeo yamebandikwa
hadharani na Wasimamizi
wa Vituo, na nakala kupewa
mawakala wetu, kwa mujibu
wa matokeo yaliyobandikwa
vituoni , CCM hadi sasa
imekwishapata majimbo 176
kati ya majimbo 264 katika
mikoa kadhaa ambayo
tumefanikiwa kujumlisha
hadi sasa. Pia, hadi sasa,
tumeweza kukomboa
majimbo 11 ambayo
yalikuwa upinzani katika
kipindi cha miaka mitano
iliyopita.
Tunawaomba wana-CCM
watulie, wasiwe na hofu,
wawe na subira hadi Tume
imalize kazi yake. Matokeo
ya Urais, ambayo
yanaendelea kutangazwa na
Tume, hayana tofauti na
mwenendo tunaouona katika
kura za Ubunge.
Imetolewa:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya
Kampeni ya CCM
26.10.2015