JamiiForums Usiku wa manane

JamiiForums Usiku wa manane

HE WATCHED MY BACK, NOW I'M WATCHING HIS BACK

Karibu sana mtaani kwetu Usiku wa Manane. Huku tunaishi kwa amani, tuna pepo yetu, nyoyo zetu ni safi, na hatuna baya na mtu isipokuwa kama wewe mwenyewe utaamua kuuleta.

Ilikuwa ni takribani mwaka mmoja na miezi mitatu tangu nijiunge na kampuni mpya. Siku za mwanzo nilikutana na homeboy mmoja ambaye tulikuwa tunashare ofisi. Yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu.

Hakunifundisha kazi tu, bali alinipa ramani nzima ya maisha ya pale ofisini.


Alinionyesha nini cha kufanya na nini cha kuepuka ili niweze kuendana vizuri na mazingira ya kazi. Alinipokea kwa mikono miwili, kwa heshima na upendo wa kweli.

Kuna wakati hata nilipokuwa bado sijastahili sifa fulani kutokana na ugeni wangu, aliamua kunisukuma mbele.


Alipoulizwa nani kafanya kazi fulani vizuri, alisema, "Hii kazi ameifanya Ertugrul Bey."
Ukweli ni kwamba nilibaki na mshangao.

Kuna watu wameumbwa na moyo wa kuinua wenzao kuliko kujitafutia sifa.

Lakini kama ilivyo kawaida ya maisha, kila mmoja ana nguvu zake na maeneo yake ya kujifunza. Kutokana na uzoefu wangu wa kazi na changamoto nilizowahi kupitia huko nyuma, ilinijengea uwezo wa kuwa makini, mwepesi wa kuchanganua mambo na kutatua changamoto kwa haraka.

Sasa hivi hali imebadilika kidogo. Kuna majukumu mapya ambayo amepewa, na kwa namna yalivyo, yanaonekana kumzidi kidogo kwa sasa. Badala ya kusimama pembeni na kutazama mambo yakiharibika, nimeamua kusimama naye bega kwa bega.

Ninamsaidia kimya kimya kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, huku sifa na pongezi zikiendelea kwenda kwake.
Huo ndio ushikaji wa kweli.
Huo ndio upendo wa watu wenye roho safi.
Kumsaidia mwenzako hakupunguzi thamani yako. Kinyume chake, kunaifanya timu nzima ishinde.

Mfano rahisi ni kama kwenye mbio za kupokezana kijiti. Mshindi si yule anayekimbia kwa kasi zaidi peke yake, bali ni timu inayojua kupokezana kwa usahihi. Vivyo hivyo maishani, wakati mwingine mafanikio ya mwenzako yanakuwa sehemu ya ushindi wako pia.

Au fikiria mtu aliyekufundisha kutumia kompyuta ulipoanza kazi. Leo unaweza ukawa wewe ndiye unayemfundisha teknolojia mpya. Hivyo ndivyo maisha yanavyozunguka.

Kwa hiyo, msomaji wangu, usisite kuwa msaada kwa wengine. Waonyeshe njia, wainue na washike mkono wanapokwama. Huwezi kujua ni lini au wapi watu hao hao watakuwa msaada kwako. Na hata kama siku hiyo haitafika, utakuwa umeacha alama nzuri katika maisha yao, na hiyo peke yake ni ushindi mkubwa.

Alamsiki!
 
Back
Top Bottom