Kodi ya Meza na Akili za Katoro: Stori ya Jumanne ya "Kibachela" hapa Goba
Jumanne, Julai 14, 2026
Saa 2:30 Usiku | Goba, Dar es Salaam
Jioni imeshakaa vizuri hapa Goba. Kama unavyojua, sisi mabachela wa muda mfupi mambo ya kujipikilisha jioni wakati mwingine yanakuwaga mzigo mzito kweli kweli. Unawaza kuosha vyombo, kumenya vitunguu... hapana, unaghairi tu! Njia rahisi na ya haraka ikawa ni kunyoosha miguu hadi kwenye cafe moja ya jirani kupata mlo wa usiku.
Sisi wanaume huwa hatuna baya kabisa. Hata ugenini, mkikutana mezani na kuanza kupiga stori, sekunde mbili tu mmeshakuwa washikaji wa tangu utotoni.
Tukiwa bado tunasubiri misosi, mara homeboy mmoja akavunja ukimya:
"Aisee, mimi leo nina hamu sana na mboga ya tembele bwana... Ila sisi tusiooa bwana tunapata sana shida kwenye hivi vyakula."
Dada wa pale mgahawani kusikia vile,
akacheka na kumtolea macho ya utani:
"Ebo! Na ukubwa huo wote bado hujaoa tu? Unasubiri nini sasa?"
Mwamba akatabasamu kwanza, kisha akajibu kwa kujiamini sana:
"Dada, mtu hakudai, hamna biashara yoyote inayowaunganisha, lakini kila siku asubuhi unatakiwa umuachie hela ya matumizi. Hiyo inakaaje?"
Ila mimi nikashindwa kuvumilia, ikabidi niingilie kati kumchokoza:
"Kwahiyo mwamba, hutaki kuoa kwa sababu tu ya kuacha 'kodi ya meza' kila siku asubuhi?"
Akajibu kwa msisitizo:
"Sio hiyo tu! Hapo hapo ukichelewa kurudi usiku, unaanza kuulizwa maswali ya kipolisi: 'Mbona umechelewa? Ulikuwa wapi?' Sitaki kabisa!"
Mwamba alitisha sana! Msimamo wake ulikuwa umenyooka kama rula: maadamu ndoa inalazimisha kodi ya meza kila kukicha na kuhojiwa masaa ya kurudi, basi kwake yeye suala la kuoa litabaki kuwa ndoto ya mchana.
Tukiwa tunamalizia misosi yetu huku tukicheka tabia za bachela mwenzetu, mdau mwingine mezani akahamisha mada na kutuletea habari za Katoro (Geita).
Akasema huko kuna watu wanatafuta na kutumia pesa kama hawana akili nzuri, yaani kufanya kufuru kabisa, wakati kuna familia nyingine huko nje hata mlo mmoja kwa siku ni mtihani.
Mimi nikachangia kwa masikitiko:
"Kiukweli, watu kama hao wangekuwa wanachangia hata kidogo tu kwenye familia maskini, hakika maisha ya wengi yangekuwa na ahueni kubwa sana."
Hapo hapo, yule mwamba wetu asiyependa kodi ya meza akamalizia stori kwa bonge moja la punchline ambalo lilituacha sote midomo wazi:
"Siku zote hela huenda kwa watu ambao hawana akili!"
Tulitazama, tukagonga glasi, na kila mtu akabeba chake.
Alamsiki kutoka Goba!