Jaji mkuu Prof. Ibrahim Juma: Majaji mzingatie mizani ya haki, msiyumbishwe na mitazamo ya watu baada ya hukumu kusomwa

bagamoyo

JF-Expert Member
Jan 14, 2010
21,318
24,214
26 February 2024
PROF. JUMA - HAKI SIO USHINDI, BALI NI USHAHIDI ULIOLETWA MAHAKAMANI UKAWEKWA KATIKA MIZANI

View: https://m.youtube.com/watch?v=STdxA1gIJ7c
Video courtesy of millard ayo

Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wote nchini kutoa haki kwa kuzingatia mizani ya haki bila kuyumbishwa na mitazamo inayotolewa na watu baada ya hukumu kusomwa.

Mhe. Prof. Juma ameyasema hayo leo tarehe 26 Februari, 2024 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo pia ametoa rai kwa watu wasioridhishwa na maamuzi yanayotolewa kukata rufaa kwa kuwa ni haki yao.

“Moja ya kazi za Majaji Wafawidhi ni kusimamia eneo la utoaji haki, na haki sio ushindi bali ni ushahidi unaotolewa kwa kuangalia mizani ya haki hivyo msikatishwe tamaa na wanaopinga maamuzi yanayotolewa,” amesema Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Prof. Juma amewakumbusha Majaji hao kusimamia haki kwa kuhakikisha kuwa wanasoma taarifa mbalimbali zinazowasilishwa kwao ili kutatua changamoto zinazojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi.

“Mnatakiwa kusimamia utoaji haki sio kuwa sehemu ya malalamiko au kukaa na kusubiri taarifa za viongozi wanaowasaidia, mfano Wasajili, Watendaji na Mahakimu Wafawidhi, lazima unapopokea taarifa, ni muhimu utafute changamoto zilizojificha ambazo wewe kiongozi mkuu wa Kanda au Divisheni unatakiwa kuzifahamu na kuzitafutia ufumbuzi,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Pamoja na hayo, Mhe. Prof. Juma hakusita kuwakumbusha Majaji Wafawidhi kuhusu matumizi ya TEHAMA hususani katika kipindi hiki ambacho Mahakama ipo kwenye safari ya kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.

“Matumizi ya Teknolojia ni eneo la msisitizo ambalo uwekezaji mkubwa umefanywa. Ni wajibu wetu Viongozi kuhakikisha kuwa, miundombinu yote ya TEHAMA na vifaa vilivyofungwa vinatumika kuleta manufaa makubwa na kutusaidia kuifikisha Mahakama katika hadhi ya Mahakama Mtandao,” ameeleza Mhe. Prof. Juma.

Ameongeza kwamba, matumizi ya Teknolojia ndio nyenzo ya karne ya 21 ya kuleta matokeo makubwa ya kusogeza huduma za haki zilizo bora, hivyo Taaluma ya Sheria na Mifumo ya utoaji haki haiwezi kukwepa mapinduzi makubwa yanayotokana na Teknolojia kukua kwa kasi.

Amewasihi Majaji hao kuwa sehemu ya safari ya Mahakama ya Tanzania inayolenga kutumia mifumo ya teknolojia kudijiti nyaraka zote za Mahakama ili kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji huduma.

Ametaja faida kadhaa zitakazopatikana endapo Mahakama itadijiti nyaraka zake, ambazo ni pamoja na kuondoa changamoto za nyaraka kutoonekana kwa kuhakikisha kuwa nyaraka zote zinatunzwa katika mifumo ya kielektroniki, kuimarisha ufanisi katika hatua za kimahakama zinazopitiwa hadi haki kupatikana.

Faida nyingine ni kuimarisha upatikanaji wa taarifa muhimu za mashauri ya wadau, Majaji, Mahakimu, Wanasheria, Wadaawa na wananchi kwa ujumla, kuongeza uwazi kwa kuweka kumbukumbu kuhusu usajili wa mashauri, amri na maamuzi mbalimbali yanayotolewa, kuongeza uwajibikaji pamoja na kuiwezesha Mahakama kukusanya na kuchambua takwimu kuhusu mashauri.

Kadhalika amewataka, Majaji hao kuwatumia Maafisa TEHAMA kikamilifu ili kutoa suluhisho ya changamoto mbalimbali za Mifumo ya Kieletroniki inayotumika mahakamani ikiwemo Mfumo wa Kieletroniki ya Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) na mingine.

Akizungumzia kuhusu Mfumo wa ‘e-CMS’ Jaji Mkuu amewataka Majaji hao kuendelea kuutumia na kubaini changamoto zinazohusiana na Mfumo huo. Hata hivyo amesema amepata changamoto na mapendekezo kuhusu Mfumo huo kutoka kwa Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza.

“Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza, alipendekeza suluhisho katika changamoto za Mfumo wa ‘e-CMS’, ambapo amependekeza Wataalamu wa Mahakama wafuatilie kwa karibu na kwa haraka uwezekano wa kuongezewa uwezo wa kuhifadhi ‘data’,” ameeleza Jaji Mkuu.

Mkutano huo wa siku tatu (3) ambao umeshirikisha Majaji Wafawidhi wote nchini pamoja na Majaji kadhaa wa Mahakama Kuu ya Tanzania unalenga kukumbushana na kubadilishana uzoefu kuhusu majukumu ya Majaji hao na nafasi zao katika maboresho ya Mahakama na kupitia maboresho ya Mhimili huo ili kufanikisha ustawi wa wananchi kwa ujumla.

Source: judiciary.go.tz
 
Ujumbe wa Benki ya Dunia -WB watembelea Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room)


Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma


Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) leo tarehe 20 Februari, 2024 umetembelea Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room) kilichopo katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania (Judiciary Square) jijini Dodoma.

Ziara fupi ya Ujumbe huo wenye takribani Maafisa watano kutoka Benki ya Dunia umeongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. jaji Dkt. Angelo Rumisha pamoja na Maafisa kadhaa wa Mhimili huo.

Mara baada ya kuwasili katika Chumba hicho, Maafisa hao walionesha kustaajabu na kufurahishwa na hatua ambayo Mahakama imepiga ya uwekaji wa chumba hicho ambacho kimesheheni taarifa nyingi za Mhimili huo.

Akitoa maelezo kuhusu Chumba hicho, Afisa TEHAMA na Msimamizi wa Mifumo ya TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Witness Ndenza amewaeleza Maafisa hao kuwa, chumba hicho kinazalisha na kuweka taarifa za viwango vya utendaji vya kitaasisi ikiwa ni pamoja na ripoti za utendaji wa mtu binafsi na dashibodi zinazotolewa kupitia kazi data ya utoaji taarifa ya Mahakama (Judiciary Business Intelligent (BI) Report Engine).

Amesema kwamba, Chumba hicho pia kinasimamia, kuendesha na kuhakikisha usalama na upatikanaji wa mtandao wa Mahakama sambamba na Ufuatiliaji wa Miundombinu ya Mawasiliano kwa ajili ya usimamizi mzuri wa wa rasilimali za TEHAMA.

Kazi nyingine za Chumba hicho maalum ni kuchakata na kutoa taarifa mbalimbali za kijinsia au vikundi maalum vinavyotolewa kupitia kanzi data ya Mahakama (Judiciary Business Intelligent (BI) Report Engine), kutayarisha na kutoa taarifa za Kanda za Kimahakama kwa kila ngazi ili kuwezesha shughuli za kimahakama na kazi nyingine.

Wakiwa ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama, Ujumbe huo ulipata fursa pia ya kutembelea chumba cha Kituo cha Huduma kwa Mteja (Judiciary Call Centre) ambacho pia kimeambatana na Chumba maalum cha Mifumo ya Kutolea Taarifa mbalimbali za Mahakama (Judiciary Situation Room).

Ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya ujumbe huo, walianza kwa kuwasilishiwa taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa ya Kurugenzi ya TEHAMA, Kurugenzi ya Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili pamoja na Kitengo cha Usimamizi wa Majengo.

Ujumbe huo unaendelea na ziara yake ambapo wamepanga kutembelea baadhi miradi ya ujenzi wa Vituo Jumuishi ikiwemo Geita na Simiyu na tarehe 24 Februari, 2024 watahitimisha kwa kufanya majumuisho katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Source : judiciary.go.tz
 
Back
Top Bottom