Profesa Ibrahim Juma kuendelea kuwa Jaji Mkuu, Rais Samia anavunja Katiba ya JMT?

lord atkin

Senior Member
Sep 30, 2018
197
683
Waungwana salaam

Ni bayana kwa mujibu wa katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 118 Ikisomwa pamoja na ibara ya 120 zinaweka wazi kuwa Jaji Mkuu atastaafu punde atakapotimiza umri wa miaka 65.

Na kwa kuwa Jaji Mkuu wetu Profesa Ibrahim Juma ametimiza umri wa miaka 65 tarehe 15/06/2023 hivyo kwa mujibu wa katiba anatakiwa kuwa ameshastaafu. Kuendelea kuwepo ofisini ni kukukiuka katiba.

Kiujumla nchi haipaswi kuwa na ombwe la Uongozi hasa ombwe katika mhimili muhimu kama Mahakama hata katiba yetu imeweka wazi hilo. Hivyo ni hatari nchi kukaa siku 12 bila jaji mkuu, hata wa kukaimu tu kama alivyofanya JPM kipindi fulani.

Au ndiyo tuamini tetesi zilizopo kwamba Rais amemuongezea muda Profesa Ibrahim Juma Kuendelea Kuwa Jaji mkuu kinyume kabisa cha katiba? Rais hana mamlaka ya kumuongezea muda Jaji Mkuu maana umri wake wa kustaafu upo kikatiba


WARAKA WA JAJI MUGASHA KUPINGA JAJI MKUU

Mtendaji Mkuu wa Mahakama​
S.L.P 9004​
DAR-ES-SALAAM​

KUH: KUVUNJWA KWA IBARA YA 118 (2) YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

1. Rejea dokezo kwa Mhe. Jaji Mwarija, Jaji wa Rufaa na Dean pamoja na Mhe. Jaji Kiongozi. Katika dokezo hilo pamoja na mambo mengine umeeleza kama ifuatavyo na ninanukuu:

‘’Mhe, JM amenielekeza kukufikishia salamu, Mhe. JR1 (Dean) na Mhe. JK kwamba Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemuongezea muda aendelee kuhudumu katika nafasi ya Jaji Mkuu baada ya muda wake wa kustaafu ambao ni tarehe 15/06/2023.

Mhe. JM anakushukuru sana wewe Mhe. JR1 na Mhe. JK kwa ushirikiano mkubwa sana mliompatia kwa muda wote ambao amekuwa katika kutumikia Mahakama. Aidha, Mhe. JM anaomba mumfikishie salamu …kwa Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani na wale wa Mahakama Kuu…’’​

[Msisitizo]

2. Dokezo tajwa limenifikia kupitia Dokezo la Mhe. Jaji Mwarija (Dean) aliyebainisha furaha yake kwa jambo hilo. Hata hivyo, Dokezo lako halioneshi muda ulioongezwa kwa Profesa Ibrahim Hamis Juma kuendelea kutumikia nafasi ya Jaji Mkuu. Hata hivyo, hatua ya kumuongezea muda wowote wa kutumikia nafasi ya Jaji Mkuu ni kuvunja Katiba na kutozingatia misingi ya Utawala wa Sheria kama nitakavyobainisha. Barua hiii imeelekezwa kwako kwa vile wewe ndiye uliyefikisha salamu husika.

3. Nibainishe wazi kuwa, sina ugomvi wowote na Profesa Ibrahim Juma na nimefanya naye kazi kwa uaminifu kwa zaidi ya miaka 10. Vilevile, sina maslahi yoyote na nafasi ya Jaji Mkuu kwani nimebakiza muda mfupi wa miaka mitatu kufikia ukomo wa utumishi wangu kama Jaji wa Rufani. Hata hivyo, kwa kiapo changu cha kazi ya Jaji ninawajibika kulinda na kutetea Katiba ya Nchi. Vile vile, kwa mujibu wa Ibara ya 26 (2) ya Katiba, mimi kama raia wa Tanzania kwa kuzaliwa wa Tanzania, nina wajibu na haki ya kutetea na kuhakikisha kuwa Katiba ya Nchi inalindwa ipasavyo.

Nimefanya utafiti wa historia ya hali ya Katiba ya Nchi kwa miaka 28 iliyopita kuhusu ukomo wa umri wa kutumikia nafasi ya Jaji Mkuu kama ifuatavyo:

a. Katiba ya nchi kama ilivyokuwa kati mwaka wa 1995, mwaka 2000 hadi tarehe 5 Aprili 2005, Ibara ya 118 likuwa na ibara ndogo 8 na kwa minajili ya waraka huu ibara (1), (2), (3) na (4) zilisomeka kama ifuatavyo:​

’(1) Kutakuwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani (ambaye katika ibara zifuatazo kwenye Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Jaji Mkuu") na Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani wasiopungua wawili, isipokuwa kwamba kikao maalum cha Mahakama nzima kitakuwa kamili kukiwa na Majaji Rufani wasiopungua watano.​

(2) Jaji Mkuu atateuliwa na Rais na atakuwa ndiye Kiongozi wa Mahakama ya Rufani na pia Mkuu wa Idara ya Mahakama kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 116 ya Katiba hii.

(3) Majaji wengineo wa Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa watu ambao wanaweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyoelezwa katika ibara ya 109 ya Katiba hii au kutoka miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa Sheria zinazotumika Zanzibar.​

(4) Iwapo itatokea kwamba–​
(a) kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi; au​
(b) Jaji Mkuu hayupo Tanzania; au​
(c) Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu yoyote, na Rais akiona kuwa kwa muda wa tukio lolote kati ya hayo matatu inafaa kumteua Kaimu Jaji Mkuu, basi Rais aweza kumteua Kaimu Jaji Mkuu kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kustahili kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, na huyo Kaimu Jaji Mkuu atatekeleza kazi za Jaji Mkuu au mpaka atakapoteuliwa Jaji Mkuu au mpaka Jaji Mkuu 3 mwingine ambaye alikuwa hayupo Tanzania au alikuwa hamudu kazi zake atakaporejea kazini.​

[Msisitizo]
Kama inavyoonekana katika msisitizo, mwaka 1995 na mwaka 2000, ibara ya II8 haikuwa na kipengele kinachoweka umri wa miaka 65 kuwa ni ukomo wa Jaji Mkuu kuhudumu katika nafasi hiyo.
b. Mnamo mwaka 2005 kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Nne Katika Katiba, Sheria Na. 1 ya mwaka 2005, Ibara yote ya 118 ilifutwa na kutungwa upya. Mabadiliko hayo yaliridhiwa (assent) na Mhe Rais tarehe 6 Aprili, 2005. Kwa minajili ya waraka huu nitanukuu ibara ya 118 (1), (2) na (3) zinazosomeka kama ifuatavyo:

“ (1) Kutakuwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani (ambaye katika Ibara zifuatazo kwenye Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Jaji Mkuu") na Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani wasiopungua wanne, isipokuwa kwamba kikao maalum cha Mahakama nzima kitakuwa kamili kukiwa na Majaji Rufani wasiopungua watano.

(2) Jaji Mkuu atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuwa Jaji wa Rufani na atakuwa ndiye Kiongozi wa Mahakama ya Rufani na pia Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 116 ya Katiba na atashika madaraka mpaka atakapotimiza umri wa kustaafu kama Jaji wa Rufani, isipokuwa kama:

(a) atajiuzulu; au
(b) kiti chake kitakuwa wazi kutokana na maradhi au kifo, au
(c) atavuliwa wadhifa wa Jaji Mkuu na Rais.
(3) Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano zilivyoanishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba au kutoka miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria zinazotumika Zanzibar na wamekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua kumi miaka na tano.”

[Msisitizo]

5. Kama msisitizo unavyodhihirisha, tofauti na ilivyokuwa kabla ya mwaka 2005, Ibara ya 118 (2) ya Katiba ya nchi imeweka ukomo kuwa Jaji Mkuu atastaafu atakapotimiza umri wa miaka 65 ambao ni umri wa kustaafu Jaji wa Rufani na hilo ndio kusudi la Bunge kufanya mabadiliko na si vinginevyo.

6. Ikumbukwe kuwa ibara ya 118 (2) ya Katiba inajitegemea na kusimama yenyewe au kwa maneno mengine it is a stand alone provision katika ukomo uliotajwa. Kwa hiyo, cross reference ya umri wa kustaafu kwa Jaji wa Rufani uliotajwa katika ibara ya 120 (1) ya Katiba ndicho kitu pekee kinachotakiwa kuangaliwa ili kufahamu umri wa kustaafu Jaji Mkuu ambao ni miaka 65 tu. na kwa sababu hiyo, nyongeza ya muda kwa Jaji wa Rufani haimhusu Jaji Mkuu asilani.

7. Ni bayana kuwa ukomo wa umri wa miaka 65 uliwekwa kwa makusudi ili kuondoa dhana potofu ya uchifu au usultani katika nafasi hiyo. Hivyo kwa kuwa Bunge lilimaanisha kilichomo katika Ibara ya 118 (2) ya Katiba na si vinginevyo, kitendo cha kumuongezea muda Prof. Ibrahim Hamis Juma baada ya miaka 65 kuendelea kuhudumu kama Jaji Mkuu ni sawa na kuliwekea Bunge mdomoni maneno ambayo halikusema wala kukusudia na ni uvunjaji wa Katiba.

8. Ikumbukwe kuwa, mara baada ya mabadiliko hayo, kulikuwa na mjadala mkubwa ndani ya Mahakama kuhusu uhalali wa Majaji waliotimiza umri wa kustaafu na wakaongezewa muda wa kuhudumu ikiwa ni pamoja na Jaji Mkuu. Wakati huo Mhe. Jaji Mwarija (Dean) alikuwa ni Msajili wa Mahakama ya Rufaa na Mtendaji wa Mahakama kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mnamo November, 2006.

9. Mjadala huo pamoja na marekebisho ya Katiba yaliyozaa Ibara ya 118 (2), vilimuibua aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika ambaye katika barua yenye Kumb. Na. JC/J.10/24/41 ya tarehe 6 Agosti, 2007 iliyoandikwa kwa Katibu Mkuu, na kunakiliwa kwa Mhe. Augustino Ramadhani (Hyt) pamoja na Ndugu Philemon Luhanjo, Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo. Katika barua hiyo, pamoja na kubainisha kuwa anayestahili kuongezewa muda wa kutumikia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji wa Mahakama Kuu, ilitamkwa bayana kuwa Jaji Mkuu anatakiwa kustaafu atimizapo umri wa miaka 65 na hastahili kuongezewa muda wowote au mkataba wa kuendelea kufanya kazi kama Jaji Mkuu. Vilevile, Mwanasheria Mkuu alieleza yafuatayo:

‘’Rais ametoa mwongozo wa kushughulikia nyongeza ya muda wa kustaafu kama ifuatavyo:​
Nashauri njia itafutwe kuondoa migongano ya vifungu vya ukomo wa ajira ya mikataba. Ni vema iendelee kuwepo fursa hiyo. Kwa Jaji Mkuu, naafiki pasiwepo na nyongeza ya utumishi na wala sioni haja ya kubaki Jaji wa Rufani wa kawaida, haipendezi.’’​

[Msisitizo]

Barua husika imeambatishwa.

10. Nilibahatika kupata nakala tajwa kupitia kwa Mhe. Jjaji Mkuu Augustino Ramadhani na ilikuwa hivyo kwa Majaji wengine waliokuwepo wakati huo. Vilevile, katika mkutano wa Majaji wote uliofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, Arusha, mnamo Septemba 2007, Mhe. Jaji Mkuu Augustino Ramadhani (Hyt) alibainisha kuwa, yeye mwenyewe atastaafu katika nafasi ya Jaji Mkuu atakapotimiza umri wa miaka 65 na hataongeza hata nusu saa kwa vile Katiba hairuhusu nyongeza na akatuasa tujiandae kuwa na Jaji Mkuu mwingine.

11. Kwa kuzingatia, matakwa ya Ibara ya 118 (2) ya Katiba, ushauri uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mwongozo wa Rais kuhusu umri wa miaka 65 kuwa ni ukomo wa Jaji Mkuu kutumikia katika nafasi hiyo, Majaji Wakuu waliofuatia yaani Mhe. Augustino Ramadhani na Chande Othman Chande ambao kwa uaminifu mkubwa kabisa na kwa kuzingatia viapo vyao, wote wawili, walitii na kuhesimu Katiba na kustaafu kwa heshima walipofikisha umri wa miaka 65.

12. Ikumbukwe kwamba, opinion ya Mwanasheria Mkuu kuhusu ushauri wake hususan jambo tajwa, ndiyo msimamo wa Serikali kama inavyoelezwa na kifungu cha cha 23 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kinachosema:

“23 (1) The opinion of the Attorney General given pursuant to the provisions of subsection (2)of this section shall remain the legal position of the Government on the matter unless it is otherwise revised by a court of competent jurisdiction, the Cabinet or otherwise recalled by the Attorney General at the instance of the Attorney General.
(2) The Attorney General or the Deputy Attorney General may at the instance of the Attorney General recall any opinion given by a law officer, State Attorney or any officer in the publicwhich is made in the name of the Attorney General.”

13. Ni wazi kwamba ushauri na ufafanuzi wa mwaka 2007 kuhusu Ibara ya 118 (2) ya Katiba ulitolewa na Mwanasheria Mkuu mwenyewe na hauguswi na masharti ya kifungu kidogo cha (2). Vile vile, kwa kuwa Mahakama haijawahi kutengua ushauri huo, na kwa vile Katiba na hususan Ibara ya 118 (2) haijawahi kufanyiwa marekebisho tena kuhusu ukomo wa umri wa kustaafu Jaji Mkuu, ushauri wa Mwanasheria Mkuu ndio msimamo wa serikali ambao umetiliwa mkazo na mwongozo wa Mhe. Rais kuwa Jaji Mkuu hastahili kuongezewa muda wa kutumikia nafasi hiyo baada ya kutimiza miaka 65 na haipendezi kubaki kama Jaji wa Rufaa. Msimamo huo kuhusu ukomo ni thabiti kwa mujibu wa kanuni rahisi ya kutafsiri sheria inayotakiwa kuzingatiwa kwa kuangalia plain language ya kifungu kwani:

“A legislature says in a statute what it says there and means in a statute what in means there.”
Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba, Bunge katika Sheria, husema inachomaanisha na si vinginevyo.

14. Kanuni hiyo imezingatiwa na Mahakama ya Rufaa ili kuhakikisha kuwa maamuzi ya Mahakama zote yanazingatia Sheria na Katiba kama inavyoelekezwa na Ibara ya 107B ya Katiba ili kuepusha upotoshaji wa tafsiri ya sheria ikiwa ni pamoja na kukiuka Katiba ya nchi. Baadhi ya maamuzi hayo ni: THE REPUBLIC VS MWESIGE GEOFREY AND ANOTHER, Criminal Appeal No.355 of 2014, PAN AFRICAN ENERGY TANZANIA LIMITED VS COMMISSIONER GENERAL TRA, Civil Appeal No. 81 of 2019 na THE COMMISSIONER GENERAL, TANZANIA REVENUE AUTHORITY AND THE ATTORNEY GENERAL VS MILAMBO LIMITED, Civil Appeal No.62 of 2022.

15. Katika shauri la THE COMMISSIONER GENERAL, TANZANIA REVENUE AUTHORITY AND THE ATTORNEY GENERAL VS MILAMBO LIMITED Mahakama ya Rufaa ililazimika kutengua na kufuta uamuzi wa Mhe. Feleshi aliyekuwa JK, ambaye hivi sasa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu alisikiliza na kuamua mgogoro wa Kodi pasipo kuzingatia kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza migogoro ya Kodi.

16.Pamoja na rejea tajwa, maswali ni mengi kuliko majibu kwani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye bado ni Jaji wa Mahakama Kuu, baada ya kupata salamu za Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuhusu Profesa Ibrahim Juma kuongezewa muda wa kutumikia nafasi ya Jaji Mkuu, alichukua hatua gani ili kumshauri Profesa Ibrahim Juma na Mhe. Rais kwa usahihi ikizingatiwa kuwa tokea Agosti 2007, ofisi Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilishatoa ushauri sahihi wa tafsiri ya Ibara ya 118 (2).

17. Vilevile, ni jambo linalotafakarisha na kushangaza iwapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni custodian wa Sheria zote na marekebisho yake hakutambua matakwa ya Ibara ya 118 (2) ili kumshauri Mhe. Rais ipasavyo kumuepusha kuingia kwenye adha ya kuvunja Katiba aliyoapa kuilinda.

18. Kwa upande wako Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania, kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili ulichohudumu Mahakamani, kama mtawala ninaamini unao uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kiutumishi ya Majaji ikiwa ni pamoja na ukomo wa kazi ya Jaji wa Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu na Jaji Mkuu. Hilo ni kwa sababu katika ofisi yako unaye Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi aliyebobea kuhusu masuala ya kiutumishi ya Majaji wote. Nashindwa kuamini kwamba hukufahamu kuwa ibara ya 118 (2) ya Katiba imeweka ukomo wa Jaji Mkuu kustaafu anapotimiza miaka 65.

19. Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania, salamu zilizomo katika Dokezo lako zinatia simanzi na kutishia Utawala wa Sheria pamoja na Uhai na Ustawi wa Katiba ya nchi. Ninasisitiza hilo kwani, ni masikitiko makubwa kwamba itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Jaji Mkuu kuvunja Katiba kama ambavyo imeridhiwa na Profesa Hamis Juma kuendelea kutumikia nafasi ya Jaji Mkuu kinyume na kiapo chake kuwa atailinda na kuitetea Katiba ya nchi.

Jambo hilo ni hatari kubwa inayoweza kuleta constitutional crisis kwani kwa mujibu wa Ibara ya 46A (2) ya Katiba, Mhe Rais anaweza kushtakiwa katika Bunge kwa kuvunja Katiba aliyoapa kuilinda. Wewe binafsi, ulikuwa na nafasi kubwa ya kumtahadharisha Profesa Ibrahim Hamis Juma mwenye uelewa wa kutosha kuhusu Ibara ya 118 (2) ya Katiba, ili amshauri Mhe Rais ipasavyo kuhusu ukomo wa kazi ya Jaji Mkuu mara atakapotimiza umri wa miaka 65.

20. Naweka bayana kuwa mimi kama raia wa Tanzania niliyepata Elimu yangu hapa nchini kwa fedha za walipa kodi, pamoja na kiapo cha kazi ya Jaji, niliahidi kuwa mtii na mzalendo kwa nchi yangu, kusema ukweli daima kwani fitina kwangu ni mwiko. Kwa hiyo dhamiri yangu ni safi na ninawiwa kuitetea na kuilinda Katiba ya Nchi. Kutosema ukweli kuwa Katiba imevunjwa, kwangu mimi ni sawa na kuisaliti nchi yangu. Siwezi kufanya usaliti kama huo na nitaendelea kuitumikia nchi yangu kwa kadri nitakavyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Aidha, ifahamike kwamba, kunyamazia uvunjaji wa Katiba na kulalamika pembeni itakuwa ni unafiki chukizo na dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu.

21.Kutokana na yote niliyoeleza ikiwa ni pamoja na historia iliyofanya kuwepo kwa ukomo wa Jaji Mkuu kutumikia na kutostahili kuongezewa muda au mkataba wa kutumikia nafasi hiyo atimizapo unri wa miaka 65, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mwongozo ambao Rais alishautoa kuhusu Jaji Mkuu kutostahili kuongezewa muda, inawezekana kuwa huenda, Mhe. Rais hakupata fursa ya kupata facts kamili kuhusu yaliyojiri kwa wakati huo yaani, kati ya mwaka 1995, 2000, 2005 hadi 2007.

22.Nihitimishe kwa kusema kwamba: Wahenga walisema, kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi kwani tunayo nafasi ya kufanya marekebisho. Hivyo, kwa kuwa nafasi ya Jaji Mkuu ni zao la Katiba (creature of the Constitution) inayoelekeza namna anavyopatikana na ukomo wa kutumikia nafasi hiyo; bila kujali matamanio ya yeyote kati yetu, busara, uadilifu, na misingi bora ya Utawala wa Sheria vyahitaji matakwa ya Katiba kuheshimiwa na kuzingatiwa ili kulinda heshima ya Rais, Mahakama Tanzania na Nchi yetu. Kwa kufanya hivyo, kutaepusha kujitia madoa madoa kwani, katika Jumuia zote za Kikanda na Kimataifa ambazo nchi yetu ni mwanachama, Tanzania imeahidi na ipo mstari wa mbele kuheshimu Utawala wa Sheria ambao msingi wake imara ni kuheshimu, kutii na kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 

Attachments

  • Mtendaji Mkuu wa Mahakama.pdf
    381.6 KB · Views: 6
Wacha hisia za ovyo ktk uongozi wa nchi. Dini inahusikaje ktk uongozi wa nchi ya Tanzania ambayo haiongozwi kwa Amri kumi za Mungu wala Sharia? Yaani mtu kala keki ya birthday June 15, leo June 27 ndiyo mlete hisia za kidini? Acheni hizi primitive nonsense. 🙏🙏🙏
Tafadhali tusilishane maneno. Binafsi nimesema nchi ina kaharufu kaudini, hilo la kusema nchi inaongozwa kwa sharia au amri kumi umelileta wewe. Hivi kama nawazungumzia watanzania wa huku mitandoni, au namzungumzia mtoa mada wewe utasemaje ? Acha umbeya.
 
kuna barua inasambaa mitandaoni, najua wengi watasema imegushiwa. inaonekana kuna upinzani kwanini Jaji Juma ambaye alitakiwa kustaafu June 15 mwaka huu (muda umeshapita anatakiwa kuwa nyumbani by now), ameongezewa muda wa kuendelea kuwa jaji mkuu. Rais kamwongezea muda kinyume na ibara ya 118 ya Katiba. tofauti na tulivyozoea, Jaji wa Mahakama ya rufani, Jaji Mugasha, ameandika waraka kupinga hilo na ameongea kwa uchungu sana as if kuna siasa nyingi sana zilikuwa zinaendelea.

amekuwa na mashaka makubwa sana na AG kwamba amelinyamazia hilo aidha kwa makusudi au bila kufanya utafiti, na ametuhumu watendaji wa Mahakama pia kuhusu hilo. hivi kwa waraka huu, mlioko ndani ndnai huko, kulikuwa na bifu gani kati ya Juma na huyu mama?

au ndio hivyo tena, wanaleta moshi mwingine ili kuzima issue ya DP WORLD kwasababu najua wateuliwa woote wa Ujaji huwa aidha wamependekezwa na kuchujwa na TISS au wao wenyewe huwa ni maTISS. hivyo atakuwa ametumwa tu kutimua vumbi tusahau issue za muhimu. nimeambatanisha waraka wenyewe hapa chini.
 

Attachments

  • WARAKA WA MUGASHA JA kupinga CJ.pdf
    381.6 KB · Views: 4
kwani Jaji mkuu yeye hakujua hilo? na swali ni je? Jaji Mkuu ambaye pia ni jaji wa rufaa anahusika na kifungu cha 120(3)? na Je, Mugasha hakukiona hicho kifungu kweli? ninavyomjua Mugasha ana uwezo mkubwa sana na anajua anachoongea.
 
Nihitimishe kwa kusema kwamba: Wahenga walisema, kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi kwani tunayo nafasi ya kufanya marekebisho. Hivyo, kwa kuwa nafasi ya Jaji Mkuu ni zao la Katiba (creature of the Constitution) inayoelekeza namna anavyopatikana na ukomo wa kutumikia nafasi hiyo; bila kujali matamanio ya yeyote kati yetu, busara, uadilifu, na misingi bora ya Utawala wa Sheria vyahitaji matakwa ya Katiba kuheshimiwa na kuzingatiwa ili kulinda heshima ya Rais, Mahakama Tanzania na Nchi yetu. Kwa kufanya hivyo, kutaepusha kujitia madoa madoa kwani, katika jumuia zote za kikanda na kimataifa ambazo nchi yetu ni mwanachama, Tanzania imeahidi na ipo mstari wa mbele kuheshimu Utawala wa Sheria ambao msingi wake imara ni kuheshimu, kutii, na kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Mimi namshauri Mama, ateue Jaji yeyote ambaye hakuwa hakimu kabla. Majaji waliotoka judiciary wana kasumba na umwinyi sana na wala wasingekuwa wamefanya hayo yote ambayo Prof Juma amefanya. hao wanatakiwa kuongozwa tu ni miungu mtu sana. mshaurini Mama vizuri.
 
Back
Top Bottom