Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,808
- 11,973
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amewaapisha Mahakimu Wakazi wapya 20 na kuwapa angalizo kuhusu matumizi ya mitandao na marafiki wanaowazunguka
Prof. Juma ametoa wito huo leo Jumamosi, tarehe 16 Julai 2022, akiwaapisha mahakimu wakazi wapya 20 Jijini Dar es Salaam.
Amesema: “Ni wakati wa kuanza kuchambua marafiki ambao mtabaki nao. Makundi ya WhatsApp ni maeneo yanayoweza kuwavunjia maadili mkaanza kujadili mambo hayatakiwi.”
Amewataka Mahakimu wasijihusishe na masuala ya siasa kwa kusema: “Usifanye mambo au kutoa kauli ambayo mwananchi anaweza kukuhusisha na chama chochote, sababu sio lazima uwe mwanachama inaweza kuwa vitendo vyako, maneno unayosema, nguo unazovaa.”
Amewataka mahakimu wasijihusishe na masuala ya siasa, kwani yamepigwa marufuku na Ibara ya 113 A ya Katiba ya nchi.
“Naomba msome Ibara ya 113 A, ya katiba ambayo inasema itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama ngazi yoyote, hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa utabaki na haki ya kupiga kura. Hivyo lazima tuelewane,” amesema Prof. Juma.
Katika hatua nyingine, Prof. Juma amewataka Mahakimu kutoahirisha kiholela tarehe za utoaji hukumu au uamuzi.
“Jambo lingine ambalo Mahakimu wamekuwa wakilifanya ambalo wananchi wamekuwa wakilalamika, ni kupanga tarehe ya kusoma hukumu halafu inafika husomi. Unapanga tarehe nyingine, inafika husomi. Wananchi wanakuwa na haki ya kukushuku,” amesema Prof. Ibrahim Juma.