Ndugu Zangu,
JANA usiku muda mfupi kabla ya taarifa ya habari, TBC1, kulikuwa na mahojiano ya mwandishi wa TBC na Babu wa Loliondo.
Kati ya aliyoyaongea, Babu anasema, kuwa Mungu ndiye aliyepanga bei ya tiba ya kikombe iwe shilingi mia tano. Kuwa alimwonyesha mia tano! Na Mungu akamwambia wageni walipe dola moja!
Tafsiri yangu;
Pamoja na kuwa mwandishi hakumuuliza Babu maswali magumu, bado Babu wa Loliondo hakunisogeza hata hatua moja kutoka kwenye msimamo wangu. Kuwa tiba ya Babu ni Abrakadabra.
Tujiulize swali moja tu; hivi Mungu huyo ni Mungu gani anayebagua waja wake. Kuwa wengine walipe mia tano na wengine dola moja?
Jamani, hivi Mungu huyu wa Babu wa Loliondo naye anafuatilia exchange rate kila siku? Itakuwaje basi, shilingi ikipanda au kushuka thamani dhidi ya dola ya Marekani? Babu itabidi aoteshwe haraka ndoto nyingine ili abadilishe bei ya kikombe!
Na kwenye taarifa ya habari iliyofuatia ikaripotiwa, kuwa Serikali imeshindwa kutoa tamko jana juu ya tiba ya Babu kwa vile Babu amesema kamati iliyoundwa iende kwanza Loliondo!
Mnajua tena mambo haya ya imani! Alitamka mwanakamati mmoja kwenye TBC1. Na leo imeandikwa kwenye gazeti moja, kuwa Serikali itatoa tamko leo juu ya tiba ya ' Babu'.
Naam. Tamko hili liharakishwe kutolewa kabla ' Babu' hajaoteshwa ndoto, kuwa ' Tamko Lisitishwe hadi itakapotamkwa tena!'. Na nani? Fikiri mwenyewe.
Si ilipata kusemwa, kuwa kila kukicha, kuna kioja kinazuka kutoka Afrika!
Maggid
Iringa,
Jumapili, Machi 27, 2011