Huduma kwa Wateja TANESCO yaelemewa, Simu zinazopigwa ni 40,000 zinazopokelewa ni 12,000 tu kwa siku

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
1701113406754.png
Imebainika kuwa kati ya Wateja 10 wanaopiga Simu Huduma kwa Watje TANESCO, ni Wateja Watatu pekee wanaoweza kusikilizwa kwa siku katika kituo cha huduma kwa wateja cha Shirika la hilo la Umeme. Hali hiyo imefanya Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kutaka mikakati ya muda mfupi kuboresha huduma hiyo.

Kauli hiyo imekuja baada ya kufanya ziara kituoni hapo jijini Dar es Salaam huku akielezwa takribani simu 40,000 zinapokelewa lakini ni 12,000 pekee ndiyo zinasikilizwa.

Tanesco iliingia makubaliano na kampuni binafsi ya EROLINK kwa ajili kuboresha huduma kwa wateja huku ikiahidiwa uwepo wao utafanya wateja kuhudumiwa kwa wakati.

Akizungumza baada ya ziara hiyo jana Jumatatu, Novemba 27, 2023, Kapinga amesema Tanesco imejitahidi kuweka mikakati ili kuboresha huduma inayokwenda kwa mteja ikiwemo kuingia ubia na kampuni binafsi ili kuboresha huduma hiyo.

“Ni kweli tuliboresha lakini kuna upungufu kadhaa, simu zinazopigwa hapa huduma kwa wateja ni 40,000 na zinazoweza kupokelewa ni simu 12,000 kwa siku, hii inatufikirisha sisi kwa ajili ya namna bora ya kuboresha huduma na kuhakikisha Watanzania wote wanaopiga simu wanapata huduma,” amesema Kapinga

Amekitaka kitengo cha huduma kwa wateja kuja na mikakakati ya muda mfupi ili kuhakikisha wateja wote wanasikilizwa na changamoto zao kupokelezwa.

“Kupokelewa changamoto ni suala la kwanza na kutatuliwa ni suala lingine lakini hazitaweza kutatuliwa kama uwezo wa kupokea changamoto ni mdogo kuliko yale ambayo tulitakiwa tuyafanye,” amesema Kapinga

Amesema ni jambo lisilovumilika kwa shirika lililo na zaidi ya miaka 50 kuzungumzia changamoto ya huduma kwa mteja huku akieleza wanafahamu kuna changamoto sugu ndani ya Tanesco huku akitaka ifike sehemu zitafutiwe ufumbuzi.

“Kama hadi leo hatujatafuta suluhu huenda tumeshindwa au wale tuliowaamini wafanye majukumu hayo wameshindwa, kama wameshindwa inabidi tufikirie namna ya kuboresha kwa kuhakikisha tuna watu sahihi kwa sababu haiwezekani changamoto ya huduma kwa mteja kwa karne hii mwananchi apige simu isipokelewe kwa sababu kituo hakina uwezo huo,” amesema

Amesema mtu anapopata changamoto ni lazima ahudumiwe ndani ya saa tatu lakini kwa sasa asilimia 32 ya wanaopiga simu ndiyo wanahudumiwa ndani ya saa tatu hadi nne huku asilimia 52 wakisubiri hadi saa nane.

“Tulipofikia umeme si anasa bali ni suala la msingi kwa Mtanzania, huwezi kumuacha mteja akae saa 12 kwa sababu umeshindwa kwenda kumtatulia tatizo lake, mgao ni kitu kingine na kumtatulia mtu changamoto kwa wakati sahihi ni jambo lingine,” amesema Kapinga.

Naibu Waziri huyo ameitaka Tanesco kuacha kusingizia mvua kuwa sababu ya kukosekana kwa huduma kwa wakati kwa kile alichokieleza walikuwa wakifahamu mvua inakuja hivyo ilikuwa lazima wajipange kama ni miundombinu ibadilishwe ili kukabiliana na hali hiyo.

Akijibu maagizo hayo, Kaimu Mkurugenzi huduma kwa wateja, Martin Mwambene amesema moja ya yatakayofanyiwa kazi kwa haraka ni kuwa na njia mbadala ya kuripoti matatizo yao.

Awali, ilielezwa kuwa, baadhi ya watu wamekuwa wakishindwa kuhudumiwa kutokana na kukosa mtu wa kuzungumza nao kwa wakati huo watumishi wanapokuwa wakizungumza na wateja wengine.

“Lakini moja ya njia tutakayokuja nayo ni WhatsApp bott na huko mbele tutakwenda kuiweka katika, Messenger ya facebook, Instagram na wengine Twitter na tutaimarisha tanesco Mobile App kwa kuiunganisha na mfumo wa sasa ili wateja wawe na njia mbadala,” amesema Mwambene.

Pia, katika maboresho hayo yatawafikia wale wasiokuwa na simu janja ili waweze kutoa taarifa za matatizo yao.

“Tutaendelea pia kuimarisha miundombinu ya umeme kwasababu changamoto zote zinaanzia huko, changamoto zinapokuwa nyingi hapa ndiyo mahali pekee watu wanaweza kutoa taarifa,” amesema Mwambene

Kutokana na kadhia hiyo, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora amesema ili kupata huduma tarajiwa ni lazima zichukue muda kidogo ili kuweza kuweza kupata kile kilichotarajiwa.

“Miundombinu na teknlojia zilizopo si zinazoweza kufanya kazi kwa haraka kiasi cha kufananisha na nchi zilizoendelea, tukiendelea kuongeza nguvu zaidi na mikakati kufanyika tunaweza kupata huduma ya papo kwa papo inayohitajika kama ilivyokuwa malengo kusudiwa,” amesema Kamuzora
 
Back
Top Bottom