Kuitangaza nchi ni jambo jema zaidi katika biashara ya kimataifa. Hata hivyo namna ya kutangaza tangazo lolote lazima kuzingatia vitu kadhaa muhimu.
1. Gharama za matangazo zisizidi matokeo ya matangazo husika;
2. Wigo wa kufikia wadau (coverage);
3. Kuzingatia muda (timing), je ni muda mwafaka kufanya tangazo hilo?
Aidha, suala la Rais kujitokeza na kuongelea majukumu ya kuitangaza nchi yaweza kuwa na kuingilia majukumu ya wasaidizi wake (mawaziri hasa - michezo, utalii na biashara). Hiyo ni sawa na baba katika familia kuwapa majukumu watoto wake, halafu inatokea sasa anaamua kufanya kazi ya mmoja wa timu ya vijana wake. Hiyo inaonyesha aidha, kijana kashindwa kazi, (i.e. hawezi uendana na kasi inayotakiwa) ama hajua cha kufanya.
Tumekuwa tukiongelea humu jamvini (JF) habari za uimara wa serikali yetu iliyopo madarakani tangu 2005. Tatizo kubwa ni kukosa dira na mwelekeo kitaifa. Masuala yanafanywa tu kama vile ilikuwa ndoto ya usiku huo, mtu akaamua kuwaambia wanakundi kwamba inabidi leo tufanye hivi. Nasema hivyo, kwa sababu masuala haya ya nchi kujitangaza yanatakiwa yawepo kwenye mikakati ya nyaraka za serikali katika sekta husika. Siyo tu inapotokea mazingira ya kuchezwa kwa mechi kama ya juzi ndipo eti tunaona huo ni mwanya wa kufanya hivyo. Hatuna dira kama nchi.
Mimi huwa natazama televisheni za kimataifa, mara nyingi nawaona kwa ukanda wa Afrika ya Mashariki, Kenya tu ndiyo wana matangazo kuhusu nchi yao na rasilimali zao. Wanaonyesha vitu walivyojitahidi kuviendeleza na ni vivutio kwa wengine (mataifa) kwenda kuviona na hata kuvitumia. Mfano mzuri ni shirika la Ndege la Kenya (KQ).
Kama nchi pengine kwa vile hatuna dira na mwelekeo, hata hayo masuala ya kuyatangaza pengine hayajulikani kwa mujibu wa Serikali. Ndiyo maana sasa wanabaki kimya na kuvizia kutumia shilingi bilioni 7 kuunda kamati ya FIFA 2010. Hizo ni fedha nyingi sana kuweza kutumiwa ndani ya muda wa miezi mitano tu eti zikawa zimeisha. Tujiulize na kujisahihisha kabla ya mambo hayajaharibika zaidi.