Taazia: Balozi Abdulkarim Omar Mtiro (Cisco) 1950 – 2017 kutoka gerezani na Temeke hadi duniani

Mohamed Said

Verified Member
Nov 2, 2008
13,711
2,000
Mohamed Said
Historia, Siasa na Maendeleo Tanzania


Mohamed Said June 07, 2017 0
Amenipigia simu mhariri wa gazeti moja maarufu akiniomba niandike taazia ya Cisco kwa gazeti lake litokalo kila juma. Nikamjibu kuwa hakika namfahamu Balozi Cisco Mtiro kwa miaka nenda miaka rudi lakini sijui niseme nini kuhusu yeye. Nikamshauri amjaribu Balozi Mohamed Maharage Juma maarufu kwa sisi tuliokuwa karibu na yeye kwa jina la ‘’Sancho.’’ Hakika kama kuna mtu anaweza kumweleza Cisco basi ni yeye Balozi Maharage. Wakati tunanyanyukia mjini Dar es Salaam kila mtu alikuwa na jina lake la kupanga, yaani, ‘’nickname,’’ na majina haya wakati mwingine yalimganda na kumwenea mtu kiasi ya kuua jina lake halisi alilopewa na wazazi wake. Hili ndilo lililomfika Abdulkarim Omar Mtiro. Ilikuwa ukimuuliza Cisco kwa jina la Abdulkarim utahangaika sana lakini ukitaja jina la Cisco hata jiwe litakuelekeza nyumbani kwake.


Mufti Sheikh Abubakar Zubeir akiongoza Sala ya Jeneza nyumbani
kwa marehemu


Cisco alizaliwa Mtaa wa Kipata baadae baba yake akahamia Temeke na huko ndiko alikokulia. Mimi binafsi kila Balozi Cisco anapokuja katika fikra zangu basi atafuatia na Balozi Mohamed Maharage Juma. Si kwa sababu ya wao kufanana kwa maumbo watu wa miraba minne au kwa kuwa wote waliingia katika kazi moja Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje la hasha, kinachonigusa mimi ni jinsi wawili hawa walivyoshabiana katika hulka zao ambazo hata kama utakutananao kwa mara moja tu basi wataacha alama katika kichwa chako kama si kuwa rafiki wa maisha. Mohamed Maharage alinipigia simu kuniuliza kama nilikuwa nina taarifa za msiba wa Cisco na akaniambia kuwa yeye tayari yuko nyumbani kwa Cisco pamoja na jamaa wengine na akaniomba nifanye hima niende mara moja. Alifanya hivi akijua ukaribu sote wawili tuliokuwanao na Cisco.

Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Sheikh Alhadi Mussa na
Paul Makonda wakitoka makaburini Kisutu baada ya maziko

Kama jana vile namkumbuka Cisco akija mjini katika, ‘’Boogie,’’ akiwa amepanda baiskeli yake nyeusi akitokea nyumbani kwao Temeke. Boogie ilikuwa ni dansi za mchana maarufu kwa sisi, ‘’teenagers.’’ Hii ilikuwa miaka ya katikati ya 1960 na wastani wa umri wetu ulikuwa miaka 15. Nawakumbuka vijana waliokuwa wakija mjini Arnautoglo Hall palipokuwa panachezwa boogie kutokea Temeke pamoja na Cisco. Kulikuwa na Moses jina halisi Mussa, Micky Jones, huyu jina lake ni Mikidadi, Allan Brown yeye ni Ali Ngotta akitoka katika familia maarufu sana Temeke. Hawa walikuwa vijana watanashati sana. Turudi katika baiskeli ya Cisco. Ukweli ni kuwa baiskeli ilikuwa haiendani na wakati ule na hali ile ya ule ujana tuliokuwanao. Unaweza kupanda baiskeli kuja shule lakini si kujanayo katika boogie. Huwezi kuja na baiskeli kwa kuwa utakuwa, ‘’umeuramba,’’ yaani umevaa vizuri sana sasa katika hali hiyo kuikwea baiskeli na kupiga pedali kutoka Temeke hadi mjini kwa kweli kutavuruga nguo achilia mbali hilo jasho litakalokutoka. Lakini Cisco toka utoto alikuwa mtu wa mikasa na vituko akiyafanya haya kwa makusudi ya dhati yake.

Cisco alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuzungumza suala lolote kwa umakini wa hali ya juu iwe ni siasa, muziki, mpira nk. Lakini kubwa ambacho Allah alimjaalia Cisco ni kipaji chake cha kuchekesha huku uso wake ukiwa unakupa wewe taswira ya kuwa lile analokueleza ni kweli kabisa kwani uso wake haukutoa taswira kuwa anafanya maskhara. Nadhani kipaji hiki alikitumia vyema katika kazi yake ya diplomasia. Miaka michache iliyopita wakati Cisco amestaafu kazi nilimtembelea Balozi Maharage nyumbani kwake Makongo. Balozi Maharage alikuwa likizo akitokea Abu Dhabi alikokuwa balozi wa Tanzania akiwa pia akiwakilisha na Iran. Balozi Maharage akanambia kuwa Cisco alipostaafu kampigia simu akiwa ofisini kwake Abu Dhabi kumpandisha midadi, akimwambia kuwa yeye anapiga simu ile akiwa Butiama Hoteli na tayari ameshatoa oda ya biriani anaisubiri iletwe mezani pake aishughulikie.

Hii Butiama Hoteli ina nafasi ya pekee katika nyoyo zetu sisi vijana wa zamani. Hii ilikuwa moja ya hoteli maarufu Magomeni Mapipa na ikiwa imemtokea mtu kuwa yuko mitaa ya Magomeni ilikuwa hakosi kuingia hapo kupata biriani yake iliyokuwa inapikwa kwa umahiri mkubwa. Hii kama utakuwa Magomeni wakati wa chakula cha mchana. Lakini ikitokea kuwa uko mjini basi hoteli itakuwa Royal Restaurant, Zahir au Khalid migahawa hii yote ilikuwa ikipika chakula kizuri sana na umaarufu wao mkubwa sana ilikuwa ni upishi wa biriani. Miaka ikapita na sisi tukakua tukatoka katika utoto na ujana tukawa watu wazima si kwa umri tu bali hata kwa nafasi kiasi ambacho ikawa tumepita kuingia baadhi ya migahawa ambayo katika ujana wetu tulikuwa hatupungui. Kama nilivyotangulia kusema, Cisco alikuwa mtu wa mikasa na kupenda kukufanya ucheke na ufurahi. Usingetegemea balozi mzima leo aingie Butiama Hoteli kwenda kula biriani kisha akabishana Simba na Yanga na wahudumu wake. Balozi Cisco hakuwa limbukeni.


Kulia: Balozi Cisco Mtiro, Mwalimu Julius Nyerere na Nelson Mandela

Wapi ambako mguu wake haukutua katika dunia hii akifuatana na maraisi wote waliotawala Tanzania, achilia mbali kusuguana mabega na wakubwa wa dunia kama Bill Clinton na Nelson Mandela, kuwataja wachache. Hapa wala sitaki kugusa alipokuwa na Mwalimu Nyerere akizungukanae kote duniani wakati wa South to South Commision ya Mwalimu Nyerere. Mafanikio haya yote na ukubwa na ukuu wake wote huu haukumvuruga kichwa chake. Barza zake na marafiki zake ni wale wale akina Mohamed Said, Ali Ngota na Ali Mzuzuri waliokuwa pamoja toka utotoni. Mimi nilikuwa ni yule yule ‘’Sidney,’’ rafiki yake wa udogoni na alipokuwa akijisikia atanikumbuka katika, ‘’whatsapp,’’ kwa kuniwekea ‘’clip,’’ ya Earl Klugh mpiga gitaa wa jazz maarufu ambae sote mimi na yeye tukimpenda kwa miaka au. ''clip,'' ya mpiga jazz yeyote yule. Nami kwa kukataa kushindwa na kutaka kuoneshana mizungu nitamrushia, ''clip,'' ya Wes Montgomery, mpiga gitaa nguli lakini wa enzi kabla ya Earl Klugh.


Kulia: Rais Mstaafu Ali hassan Mwinyi, Mohamed Chande Jaji Mkuu Mstaafu, Rashid Othman Mkuu wa Usalama wa Taifa Mstaafu an Benard Membe Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Mstaafu

Butiama bila shaka palimkumbusha mengi na njia ndefu aliyopita hadi kufikia pale alipofika akiwa na ofisi ndani ya Ikulu ya Jamburi ya Tanzania. Wafanyakazi wa Butiama wengi wao ni wale wale na wengi wana Yanga wenzake na bila shaka alipata wasaa wa kukumbushana enzi zilizopita na kucheka pamoja kisha kuwaachia, ‘’tip,’’ nono. Karibu na Butiama Hoteli ilikuwapo hoteli ya marehemu Shomvi Yanga mwenzake na hoteli yake ‘’Michuzi Mikali.’’ Shomvi akapichikwa jina Shomvi Michuzi Mikali. Shomvi yeye alijikita katika kuku wa kukaanga aliotoa kwa ugali au wali. Shomvi alikuwa anatengeneza pilipili ya ajabu chachandu nzuri kabisa iliyokwenda sawia na kuku wake wa kukaanga.

Hivi vyote vilikuwa viwanja vyetu katika miaka ile ya 1970 tukiwa vijana. Sehemu hizi si tu mtu alikuwa anapata chakula kizuri bali alikuwa anapata pia maongezi mazuri ya ushabiki wa Simba na Yanga na wakati mwingine wachezaji wa timu hizi hujumuika pale kwa chakula cha mchana. Na wapenzi walikuwa hawabagui ikiwa watalipa chakula basi watawalipia wote wachezaji wa Yanga na Simba bila matatizo na kwa utani kidogo kama vile, ‘’Maulid kula nguvu yetu Simba uje utufunge tena,’’ na watu wote watacheka na kufurahi pamoja. Huyu Maulid alikuwa marehemu Maulid Dilunga, mshambuliaji mkali wa Yanga.

Pale alipokuwa ndani ya Butiama Hotel,Cisco aliweza kuona Shibam Hotel vizuri kabisa kwani ukivuka Barabara ya Morogoro ndipo ilipo Shibam hadi leo, ilipokuwa barza ya marehemu Mkanga shabiki mkubwa wa Simba toka enzi za Sunderland. Miaka mingi ya kuwa Balozi Cisco nje ya nchi haikumtenganisha Cisco na ndugu zake. Alikuwakumbuka na kuwasaidia rafiki zake alioukuwanao African Temeke na Good Hope za Temeke. Timu hizi za mchangani huko Temeke kwao Balozi Cisco ndizo zikitoa wachezaji hodari vijana kuja Yanga na Simba katika miaka ile kama akina Lenard Chitete na Shaibu Ngotta kuja Simba na Yanga.

Balozi Cisco kiti chake kilikuwapo Leaders Club lakini halikadhalika hakusahau kijiwe chake cha mtaani kilichomkuza. Meza yake ilikuwapo katika mahoteli makubwa ya sifa duniani lakini haikumpa shida kuja kula Butiama na kuwasalimia nduguze.

Turudi hoteli ya Butiama na biriani.

Cisco alijua hii ya Butiama atakuwa amemkomesha rafiki yake Balozi Maharage. Ndipo aliponyanyua simu yake ya bei kali akampigia kumfahamisha kuwa yeye yuko hapo Butiama anakula biriani. Balozi Cisco akamaliza mazungumzo yake kwa kumtahadharisha balozi mwenzake kuwa achukue tahadhari ya kuacha ofisi mapema apate mafao yake maana shilingi inaweza kuporomoka na yeye akatoka kapungukiwa pakubwa. Balozi Maharage alipomaliza kunihadithia salamu na indhari aliyopewa na Cisco akaanza kucheka na mimi sikuweza kustahamili tukawa sote tunacheka na kupiga gonga. Hakika Cisco hawezekani tulikubaliana sote.

Siku moja niko darasani Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwalimu Mzungu kutoka Uholanzi akitusomesha kozi, ‘’Politics of Industrial States,’’ bila shaka alikuwa kahisi jambo kwetu sisi wanafunzi wake akasema kutuambia kuwa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje inashangazwa na kiwango cha chini cha miaka ya karibuni ya vijana kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam waliokuwa wanajiunga na wizara hiyo. Mwalimu akaendelea kusema kuwa kulikuwa na wakati hakika chuo kilikuwa kikitoa wahitimu hodari katika nyanja zote kuanzia lugha, Kiingereza na Kifaransa hadi ujuzi wa siasa za dunia. Akamaliza kwa kusema kuwa wizara inashangaa kimepitika nini kuwa vijana kama hawa ghafla wamepotea.

Cisco alikuwa ameingia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje akiwa mmoja wa kundi hili la vijana, ‘’smart,’’ wa ‘’Foreign,’’ ambao walikuwa wa kupigiwa mfano na baadhi nikiwafahamu kama Eliud Aickim ‘’Brown,’’ Mwandembwa, Ami Mpungwe, Kassim Mwawado, marehemu Gasper Yusuf Hakili kwa kuwataja wachache. Vijana hawa walikuwa na, ''sophistication,'' ya aina yake kuanzia, ''etiquettes,'' hadi mavazi. Naukumbuka sana utanashati wa Cisco akiniacha mie kwa mbali sana.

Iko siku mimi na Mohamed Maharage tuko London Underground tunasubiri treni. Pembeni yetu walikuwa wamekaa viajana wa Kifaransa na walikuwa wanazungumza Kifaransa. Katika kusubiri kule hawa vijana ambao walikuwa watalii, maana walikuwa wakipiga picha nyingi mimi na Mohamed tukawa tunaingia katika picha zao. Mmoja kati yao, kijana wa kiume akawa anazangumza na binti aliyekuwanae kisha wanacheka kwa sauti kubwa. Mara nikaona Mohamed kawageukia na anaanza kuzungumza nao Kifaransa kwa kama dakika mbili tatu. Kutokana na jinsi niliyomuona yule kijana wa kiume anazungumza na Mohamed nikahisi pale pamepitika jambo.

Kweli kwa hakika palikuwa pamepitika jambo. Yule kijana alituita mimi na Mohamed ‘’maua meusi,’’ akimwambia mmoja wa wale akina dada kuwa picha zao zitapendeza sana kwa kurembwa na ‘’maua meusi,’’ ya London. Alisema maneno haya kwa Kifaransa. Hapo ndipo Mohamed akawageukia na kuwaambia kwa lugha hiyo hiyo yao kuwa, ‘’Basi ingawa mmeyapenda, ‘’maua meusi,’’ ingependeza kama mngeyaomba ruhusa kabla hamjayapiga picha. Vijana wenzetu Wafaransa wakatutaka radhi. Hawa ndiyo akina Cisco, vijana, ‘’smart’’ wa Foreign Affairs,’’ wa enzi zile. Mambo haya yametokea sasa zaidi ya miaka 30 imepita.

Nimempa pole Balozi Mohamed Maharage kwa kuwa najua yeye msiba wa Cisco ni mkubwa sana juu yake umemuelemea kwa kuwa ameishi na Cisco kwa miaka mingi toka udogo wao hadi kufika kufanyakazi pamoja Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kisha kustaafu na kuwa pamoja. Halikadhalika nimempa pole Ali Mzuzuru rafiki kipenzi wa Cisco toka utoto wao na ambao wazee wao walikuwa kati ya wazee wa Temeke waliojenga Msikiti wa Tumbi, Temeke wakisaidiwa na Aga Khan wakati wa enzi za East African Muslim Welfare Society (EAMWS).


Kushoto: Salum Matimbwa, Shaib Ngotta na nyuma kulia ni Ali Ngotta, Magombe Makongoro na Hamisi Chenja na nyuma wa pili kulia ni Ilyas Abdulwahid Sykes

Nimempa pole Micky Jones ambae kanineletea picha akiwa na Cisco VIP Longe Copenhagen pamoja na Rais Kikwete alipokwenda huko. Nimempa mkono wa pole Ali Ngotta na mdogo wake Shaibu Ngotta. Nikiwapa pole na hawa wote hawa wote wakawa wananirejeshea mimi pole wakinambia na mimi pia nipoe.

Iko siku wakiwa safarini Cisco alimchekesha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hadi machozi yakammwagika.

Lakini kisa hiki In Shaa Allah nakitafutia siku yake.

There was never a dull moment with Cisco.


Ali Mzuzuri

Balozi Cisco na Mwandishi

Hakika Cisco amevuka milima na mabonde kutoka Kipata na Temeke hadi kufika duniani. Tunamuomba Allah amweke ndugu yetu Abdulkarim Omar Mtiro mahali pema peponi.

Amin
 

Nnangale

JF-Expert Member
Jul 20, 2013
1,822
2,000
pole kaka Mohd Said kwa kuondokewa na nduguyo na rafiki wa tangu utotoni,lakini kisa cha uchaguzi temeke ni cha muhimu mbona hakipo kabisa au nacho utakisimulia siku nyingine?
 

Mohamed Said

Verified Member
Nov 2, 2008
13,711
2,000
pole kaka Mohd Said kwa kuondokewa na nduguyo na rafiki wa tangu utotoni,lakini kisa cha uchaguzi temeke ni cha muhimu mbona hakipo kabisa au nacho utakisimulia siku nyingine?
Nnangale,
Kisa kile ni muhimu sana si kwake tu bali hata kwangu.
Naamini kilimfunza Cisco ukweli wa mambo.

Sikutaka kuingiza machungu katika taazia yake.
 

MAWAZO UJENZI

JF-Expert Member
Apr 22, 2012
2,424
2,000
Samahani mwandishi was habari, katika kumbukumbu zangu wakati wa utawala na Jakaya Kikwete,paliwahi kutokea mtafaruku kuhusu ziara ya Kikwete!

Taarifa zilitolewa kwamba mkuu wa Itifaki alipanga safari hewa ya Mzee Kikwete na waliomba 2B! Lakini watu wa foreign affairs wakasema mbona hii safari haipo? Mkuu wa itifaki akatolewa kwenye cheo chake! Naomba kujua ndo huyu marehemu Cisco??
 

124 Ali

JF-Expert Member
Apr 25, 2010
7,520
2,000
Kuna watu wakiandika hawakuchoshi bali wanakufanya uhamaki kwa kutoendelea na simulizi Mohammed Said ni mmoja wa watu hao!
Akhsante mkuu!
 

ISIS

JF-Expert Member
Apr 20, 2016
91,521
2,000
Samahani mwandishi was habari, katika kumbukumbu zangu wakati wa utawala na Jakaya Kikwete,paliwahi kutokea mtafaruku kuhusu ziara ya Kikwete!

Taarifa zilitolewa kwamba mkuu wa Itifaki alipanga safari hewa ya Mzee Kikwete na waliomba 2B! Lakini watu wa foreign affairs wakasema mbona hii safari haipo? Mkuu wa itifaki akatolewa kwenye cheo chake! Naomba kujua ndo huyu marehemu Cisco??
Duh!
 

jogi

JF-Expert Member
Sep 25, 2010
25,394
2,000
Samahani mwandishi was habari, katika kumbukumbu zangu wakati wa utawala na Jakaya Kikwete,paliwahi kutokea mtafaruku kuhusu ziara ya Kikwete!

Taarifa zilitolewa kwamba mkuu wa Itifaki alipanga safari hewa ya Mzee Kikwete na waliomba 2B! Lakini watu wa foreign affairs wakasema mbona hii safari haipo? Mkuu wa itifaki akatolewa kwenye cheo chake! Naomba kujua ndo huyu marehemu Cisco??
Umempiga rungu la kichwa!!!!
Analeta mambo ya kusifiasifia mtu kibwegebwege!!!!!
 

Dingswayo

JF-Expert Member
May 26, 2009
4,022
2,000
Cisco alikuwa mcheshi na aliyekuwa anapenda watu. Nakumbuka pia alikuwa anapenda muziki. Enzi hizo tukiwa Chuo Kikuu DSM tulikuwa tunakwenda kumtembelea pale Chuo cha Diplomasia mimi na Mwandembwa na kusikiliza muziki kwenye 'music system' yake.
 

sodoliki

JF-Expert Member
Apr 2, 2012
2,591
2,000
pole kaka Mohd Said kwa kuondokewa na nduguyo na rafiki wa tangu utotoni,lakini kisa cha uchaguzi temeke ni cha muhimu mbona hakipo kabisa au nacho utakisimulia siku nyingine?
Brother mohammed, kuna wakati Sisco kabla ya kuingia Wizara ya Mambo ya nje alikuwa anafanya kazi National Housing Corporation, na wakati huo alikuwa anaishi Magomeni, nahisi walikuwa na nyumba hapo sikumbuki mwaka lakini kama sikosei ni kama 74 - 76 hivi , hii hukuitaja
 

sodoliki

JF-Expert Member
Apr 2, 2012
2,591
2,000
Cisco alikuwa mcheshi na aliyekuwa anapenda watu. Nakumbuka pia alikuwa anapenda muziki. Enzi hizo tukiwa Chuo Kikuu DSM tulikuwa tunakwenda kumtembelea pale Chuo cha Diplomasia mimi na Mwandembwa na kusikiliza muziki kwenye 'music system' yake.
umenikumbusha tulikuwa tunaiita changer , kama sikosei ilikuwa ya sanyo
 

sodoliki

JF-Expert Member
Apr 2, 2012
2,591
2,000
Samahani mwandishi was habari, katika kumbukumbu zangu wakati wa utawala na Jakaya Kikwete,paliwahi kutokea mtafaruku kuhusu ziara ya Kikwete!

Taarifa zilitolewa kwamba mkuu wa Itifaki alipanga safari hewa ya Mzee Kikwete na waliomba 2B! Lakini watu wa foreign affairs wakasema mbona hii safari haipo? Mkuu wa itifaki akatolewa kwenye cheo chake! Naomba kujua ndo huyu marehemu Cisco??
Sisco hakuusika na hii alikuwa Itatiro
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom