Emirates shirika bora la ndege Tanzania

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,148
Emirates shirika bora la ndege Tanzania
Mwandishi Wetu
Daily News; Wednesday,May 31, 2008 @07:39


EMIRATES imechaguliwa kuwa Shirika Bora la Ndege la Mwaka nchini wakati wa sherehe za utoaji tuzo za Chama cha Wakala wa Usafiri Tanzania (Tasota) zilizofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.

Sherehe hizo za Tasota za utoaji tuzo kwa mashirika ya ndege na watu waliofanya vizuri katika sekta za usafiri wa anga na utalii zilifunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta za usafiri wa anga na utalii.

Emirates ilitawala katika sherehe hizo kwa kushinda tuzo sita zikiwamo shirika bora la ndege la mwaka, shirika la ndege linalotoa programu maalum kwa wasafiri wanaosafiri mara kwa mara, shirika la ndege lenye kutoa huduma bora ndani ya ndege, na shirika la ndege lenye huduma zenye ongezeko la thamani.

Katika sherehe hizo wafanyakazi wawili wa Emirates walipata tuzo binafsi ambapo Meneja wa Emirates Uwanja wa Ndege, Juma Abubakar, alitunukiwa tuzo ya Meneja Bora wa Mwaka wa Kituo, wakati Zubeda Kassim alitunukiwa tuzo ya Mfanyakazi Bora wa Mwaka katika mashirika ya ndege.

Akielezea mafanikio hayo, Meneja wa Emirates nchini, Bader Hassan alisema, “Nimefarijika sana kushinda tuzo zote hizi za TASOTA, hii inaonyesha kwamba wateja wetu nchini Tanzania wametambua juhudi zetu katika kutoa huduma bora. Emirates inajitahidi kutoa bidhaa na huduma bora kwa wateja wake duniani kote na ndio maana tumeshinda tuzo nyingi za kimataifa”.

Emirates yenye Makao yake Makuu Dubai ni moja ya mashirika ya ndege yenye kupata faida na yenye mafanikio zaidi duniani. Emirates ambayo inasafiri kwenye majiji 99 katika nchi 62, imejizolea sifa kwa uvumbuzi na kuongoza kutoa huduma bora katika sekta ya usafiri wa anga na pia imeshinda zaidi ya tuzo 400 za kimataifa kwa kutoa huduma za kiwango cha juu.

Kila mwaka Tasota hutoa tuzo kwa wadau wake ambao ni mashirika ya ndege, hoteli pamoja na wafanyakazi ambao hufanya vema na kutoa mchango mkubwa katika sekta husika.
 
Back
Top Bottom