Zitto, Dk. Mwakyembe watofautiana Dowans
2009-02-27 10:07:44
Na Muhibu Said
Dhamira ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) ya kutaka kununua mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura yenye uwezo wa kutoa megawati 100 inayomilikiwa na Kampuni ya Dowans, imezua mambo.
Hiyo imetokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dk. Harrison Mwakyembe, kutofautiana kuhusu suala hilo.
Tofauti kati ya Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) na Dk. Mwakyembe Mbunge wa Kyela (CCM), imeibuka siku sita baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shellukindo kutamka hadharani kuwa kamati yake haikubaliani na dhamira hiyo ya Tanesco inayoonekana kuungwa mkono na Kamati ya Zitto.
Shellukindo, ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), alitangaza msimamo huo wa kamati yake, siku moja baada ya Tanesco kuripotiwa na vyombo vya habari ikiendeleza dhamira yake mbele ya Kamati ya Zitto ya kutaka kununua mitambo hiyo.
Tofauti kati ya wabunge hao, ambao katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, wametokea kuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania kwa ujasiri wao wa kupambana na ufisadi na mafisadi nchini, imedhihirika baada ya Dk. Mwakyembe, ambaye kueleza hisia zake kwamba, ameshangazwa na hatua ya Kamati ya Zitto kuzungumzia suala la Dowans wakati si kazi yake.
``Kazi ya Kamati ya Zitto ni kuangalia mahesabu na siyo sera. Nadhani Zitto anapaswa kusoma kanuni za Bunge aelewe,`` alisema Dk. Mwakyembe katika mahojiano maalum na Nipashe juzi.
Dk. Mwakyembe alisisitiza kuwa maamuzi yaliyofikiwa na Kamati ya Madini na Nishati kuhusu suala hilo, hayawezi kamwe kupingwa na kamati yoyote hivyo, akamshauri Zitto kusoma kanuni za Bunge.
Naye Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, alisisitiza kuhusu uamuzi wa kamati yake wa kumuomba Spika wa Bunge kibali ili aruhusu kuitisha kikao cha kamati zote mbili (ya Hesabu za Mashirika ya Umma na Nishati na Madini), serikali, Tanesco na Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ili wajadili na kufikia muafaka wa pamoja kuhusu suala la kununua mitambo ya Dowans ili kuepuka kamati kupingana.
Alisema wazo la Dowans lilikuja baada ya kamati yake kukagua matumizi ya Tanesco na kugundua kuwa katika kila Sh. 100 inazopata shirika hilo, Sh. 84 zinakwenda kwa makampuni yanayoiuzia umeme.
``Hivyo, ndio tukaamua kuomba kukutana na Kamati ya Nishati na Madini tujadili hiyo hali kwa pamoja ili nchi isije kukumbwa na giza,`` alisema Zitto.
Alisema kazi ya Bunge si kuingilia utendaji wa serikali bali kusimamia.
``Hata hivyo, inaonekana Bunge linataka kuingilia utendaji wa serikali, linatakiwa lisimamie tu,`` alisema Zitto na kuongeza: ``Kamati ya kina Mwekyembe haikusikiliza Tanesco, hivyo tunaiomba ifanye hivyo``.
Zitto alisema suala lolote lenye maslahi ya umma yuko tayari kukosolewa, hawezi kamwe kuingiza siasa.
``Hivi kweli Watanzania wako tayari kukaa katika giza? Kamati yangu ina nia njema kwamba kamati zote mbili ziwasikilize ndio tutoe uamuzi ambao utakuwa na maslahi kwa taifa kuliko kulumbana,`` alisema
Alisema kwa hali ilivyo sasa taifa linakabiliwa na upungufu wa megawati za umeme zaidi ya 100, hivyo haoni sababu gani nchi iingie katika gharama kubwa za kuweza kuangiza mitambo wakati tayari ipo ya Dowans.
``Kwanza tukianza kuagiza mitambo kutakuwa na gharama kubwa ambazo tutalipa, mawazo yangu ni kwamba tuangalie uwezekano wa kununua mitambo ya Dowans ili nchi isije kuingia katika giza kama Tanesco walivyotuambia. Tukiingia katika giza uzalishaji utakupungua na uchumi utatetereka,`` alisema Zitto
Mimi Jumatatu wiki hii, Nipashe ilimkariri Shellukindo akisisitiza msimamo wa kamati yake wa kupinga dhamira hiyo ya Tanesco kwa vile inakiuka taratibu na haina maamuzi ya kununua mitambo hiyo.
Shellukindo, alisema mwenye maamuzi ya kununua mitambo hiyo ni serikali kama imeona kuna dharura ya kufanya hivyo.
Hata hivyo, alisema taratibu zilizopo zinataka suala hilo lifikishwe kwanza bungeni ili likajadiliwe na kupata baraka za Bunge.
Alisema ipo pia, sheria ya manunuzi inayozuia kununua mitambo chakavu kwa vile hatua hiyo ni ya hatari.
Kutokana na hali hiyo, alisema haoni kuwa ni busara kung'ang'ania kutaka kununua mitambo ya Dowans kabla taratibu zinazohusika hazijafuatwa na kwa kuzingatia pia, kwamba, mitambo ya kampuni hiyo haijulikani ilitumika kwa muda gani.
``Tanesco wanadai kuwa Dowans wanalo jenereta jipya. Lakini mitambo yao (Dowans) iliingizwa nchini mwaka 2006 na utekelezaji ulianza Desemba 2007. Sasa hilo jenereta linaweza kuwa jipya? Na hata yale (majenereta) mengine hatujui kama ni mapya,`` alisema Shellukindo.
Alisema inashangaza kuona Tanesco iking`ang`ania kutaka kununua, huku mkononi mwake ikiwa na amri ya mahakama iliyoomba kuzuia kuuzwa kwa mitambo ya Dowans kwa vile inaidai kampuni hiyo.
``Hatuna uhakika Tanesco wanaidai nini Dowans, hilo haliko wazi, tunataka tujue kwanza hilo. Hata hivyo, kama hilo lipo basi si wangekubaliana wabadilishane badala ya kununua,`` alisema Shellukindo.
Tanesco iliifikisha dhamira yake hiyo kwenye Kamati ya Zitto miezi miwili baada ya Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na Shellukindo, kupinga suala hilo mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja Desemba, mwaka jana.
Awali, Zitto alikaririwa na Nipashe Jumatatu wiki hii akisema kuwa katika kikao kati ya kamati yake na Tanesco kilichofanyika jijini Dar es Salaam Jumamosi wiki iliyopita, uongozi wa shirika hilo walitoa hoja za msingi kuhusu dhamira ya shirika ya kutaka kununua mitambo ya Dowans.
Zitto alitaja sababu nyingine ya kamati yake ya kuomba kibali hicho kwa Spika, ni kwa vile Kamati ya Nishati na Madini, haikutoa nafasi ya kukutana na Tanesco ili waeleze kwanini wanataka kununua mitambo hiyo ya Dowans.
``Walikutana tu na Waziri Ngeleja wakapinga Tanesco kununua mtambo huo wa Dowans,`` alisema Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Alisema pia, watatumia fursa ya ruhusa hiyo Spika kujadili kuhusu hatma ya umeme wenye megawati 300 wa Mtwara baada kampuni ya Barick kujitoa na umeme wa upepo wa Singida.
SOURCE: Nipashe