Sijui wengine mmepokeaje taarifa hii, tutaona mtakavyochangia.
Mimi nilipoipokea tu moja kwa moja nikatafuta sentensi ambapo Hamadi ataeleza ni kanuni gani ya bunge ambayo CHADEMA wameivunja. Hakuna hata sentensi moja. Ni tatizo, kubwa tu la CUF.
Kuna ugonjwa mbaya unaoanzia hata kwenye jamii na kuendelea hadi kwenye makundi makubwa ya kitaifa kama vyama. Ugonjwa huo uko hivi: tunajua kwamba fulani anaweza kufanya jambo fulani tulipendalo kwa hiari yake na utashi wake tu.
Lakini badala ya kumuomba na kumuacha hiari yake na utashi wake vimsukume kufanya tupendalo kale ka-ugonjwa kanatusukuma tumshinikize hadi ile hiari yake igeuke kuwa kama lazima.
Ukweli unabaki palepale kwamba kelele hata kama ni za dunia nzima haziwezi kugeuza jambo la hiari kuwa la lazima. Tukifanikiwa kulilazimisha na hivi vishinikizo vyetu basi huo nao ni ufisadi mwingine wa kupora hiari ya mtu\chama na kuifanya lazima.
Ndicho wanachokifanya wenzetu hawa bahati nzuri Hamad haelezi kuwa kama CHADEMA waliwahi kushinikiza hiari kama wao sasa hivi.
Tumejadili kanuni za bunge kuhusu hili na hapa tuzisome tena vifungu vyake:
14(2):
Wabunge wote wa Upinzani wanaweza kuunda Kambi Rasmi ya Upinzani iwapo idadi yao itakuwa si chini ya asilimia 12.5 ya Wabunge wote.
14(3):
Chama cha Upinzani hakitakuwa na haki ya kuchagua Kiongozi wa Upinzani Bungeni, isipokuwa tu kama kina idadi ya Wabunge wasiopungua 12.5% ya Wabunge wote.
14(4):
Endapo kutakuwa na Vyama vya Upinzani zaidi ya kimoja ambavyo kila kimoja kina Wabunge 12.5% au zaidi, basi Chama chenye idadi kubwa zaidi ya Wabunge kuliko vingine ndicho kitakuwa na haki ya kuchagua Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, lakini, ikiwa kutakuwa na vyama viwili au zaidi vyenye idadi sawa ya Wabunge ambao ni zaidi ya 12.5%, Wabunge wa vyama vinavyohusika watachagua Kiongozi wa Upinzani Bungeni chini ya utaratibu watakaokubaliana wenyewe.
15(1):
Chama chenye haki ya kumchagua Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kinaweza pia kuchagua Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
15(2):
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni atateua Wabunge wa Chama chake au Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao watakuwa wasemaji wakuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara zilizopo za Serikali.