WAKATI kukiwa na taarifa kwamba chama kipya kilichopata usajili wa muda, Chama Cha Jamii (CCJ), kimeundwa na baadhi ya vigogo wa CCM ambao wanataka kujing'atua kutoka katika chama hicho tawala, viongozi wa muda wa CCJ wamekanusha vikali madai hayo na kusisitiza kwamba chama chao kimeundwa kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Wakizungunza na MWANANCHI viongozi wa muda wa chama hicho Richard Kiyabo ambaye ni mwenyekiti na katibu wake Renatus Muabhi wanasema kuwa wamekuja kurudisha matumaini ya Watanzania yaliyopotea.
Swali: Nini lengo la kuanzisha chama hiki?
Muabhi: Tumechukua hatua wa kuanzisha chama hiki baada ya kuona nchi inaingia katika matatizo mbalimbali na migogoro isiyokwisha ya vyama. Matokeo yake malengo ya vyama hivyo kwa wananchi hayatekelezwi huku wananchi wakibaki kutaabika.
Swali: Je, CCJ, mtawezaje kutimiza malengo hayo kwa wananchiKwasababu hata vyama vya TANU na CCM vilipoanzishwa vilikuwa na malengo hayohayo lakini wameshindwa kuyatimiza?
Muabhi:Tutaweza kwa sababu kila kitu kinapangwa na kwa kupitia mipango hiyo, chama kama Oganaizesheni tutaifanikisha mipango hiyo. Pia tunaamini tutaweza kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.
Swali: Kuna taarifa kuwa chama hiki kimeundwa na baadhi ya vigogo wa CCM wanaotaka kujiengua, mnasemaje au wadhamini wa chama hiki ni akina nani?
Muabhi: Chama hiki kimeundwa kwa maombi ya wananchi wa kada mbalimbali kama vile vijana, wafanyakazi wastaafu na wengineo wasioridhishwa na mwenendo wa serikali.
Mwenyekiti ni Richard Kiyabo na Katibu ni Renatus Muabhi. Kwa kuwa sasa chama hiki kina usajili wa muda, tutashikilia uongozi wa chama hadi hapo uchaguzi rasmi utakapoitishwa.
Hakuna kigogo yoyote wa CCM aliyehusika kuunda chama hiki. Ila kama kuna vigogo wanaotaka kuja kwenye chama chetu tunawakaribisha, lakini wawe wasafi maana hatutavumilia ufisadi wa aina yoyote.
Swali: Watu hao mlikutana wapi, mlikuwa na ofisi kabla ya kusajiliwa?
Muabhi: Hapana, hatukuwa na ofisi wala kibali cha kutafuta wanachama, lakini tulikaa na kufikiri jinsi ya kuanzisha chama, tukatafuta ushauri kutoka kwa watu mbalimbali kwenye mazungumzo rasmi na yasiyo rasmi.
Tumefanya utafiti, unajua kama mtu kama unataka kufanya jambo lazima uulize watu wakupe ushauri. Kwa hiyo tumepata maoni kutoka kwa watu mbalimbali tukaona tuyatumie. Inawezekana kwa kutumia utaratibu huu.
Swali: Lakini hamuoni kuwa jina hilo la CCJ linashabihiana na uhusiano na lile la CCM?
Muabhi: Hapana, nakanusha hilo. Ni jina tu lililobuniwa kwa ajili ya kuhimiza ustawi wa Watanzania. Kwa mfano watu wanaweza kuanzisha chama cha waosha magari, au chama cha wafanyabiashara na sisi tumeanzisha chama chetu na kuita jina hilo kwa sababu tumeilenga jamii, wala halina uhusiano na CCM.
Swali: Umesema kwamba mmeanzisha chama kutokana na migogoro iliyomo kwenye vyama vingine vilivyoshindwa kutimiza malengo ya wananchi, ni migogoro gani hiyo, au unamaainisha mpasuko wa CCM?
Muabhi: Tunasema kuna migogoro ndani vyama kwa sababu hatuoni chama chenye dira ya kuwakomboa wananchi. Vyama vimekalia kulumbana na kusahau majukumu yao.
Tumepata nguvu zaidi baada ya kuona migogoro ndani ya CCM, kwamfano tumesikia hata kamati zikiundwa kuwakemea Wabunge na mambo mengine. Sisi tumekuja na njia mbadala.
Hata vyama vya upinzani vimesahau wajibu wao, vimekalia kuisifu serikali. Ndiyo maana tumeanzisha CCJ ili kuleta changamoto ya kweli kwa CCM.
Swali: Kwanini mmeanzisha chama hiki miezi michache tu kabla ya uchaguzi mkuu, hamuoni kwamba mnaweza kuchelewa uchaguzi?
Muabhi: Siyo kwamba chama kimeanzishwa dakika za mwisho, tulikuwa na mipango ya kuanzisha chama hiki muda mrefu na hivi sasa ndiyo tunakamilisha.
Kitu kikubwa ni oganaizesheni tu, huwezi kutafuta wanachama kwa miezi miwili kama hujajipanga vizuri. Sisi tumeshajizatiti ili kuhakikisha kuwa tunapata wanachama mapema ili tufikie matakwa ya msajili wa vyama vya siasa.
Swali: Uwezo huu hasa wa kifedha, wa kukamilisha masharti ya msajili wa vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na gharama za kuzunguka mikoani, kwa muda mfupi mnaupata wapi?
Muabhi: Chama kinapotaka kujizatiti huwa na mipango.
Kwa kuwa sasa tunaendelea kusajili wanachama, hao ndiyo watakaotoa michango. Siyo kwamba tunatarajia kupata ufadhili kutoka kwa watu fulani.
Swali: Kwani chama hiki kina tofauti gani na vyama vingine vya upinzani?
Kiyabo: Tofauti yetu kubwa ni sera. Pamoja na kwamba kila chama kina sera za kimapinduzi, sisi tumekwenda mbali zaidi. Tunataka wananchi wamiliki njia kuu za uchumi ili wafurahie matunda ya rasilimali zao. Wawe na uhuru wa kupata maendeleo na kujiendeleza.
Tumefanya feasibility study (upembuzi yakinifu) wa sera za vyama vingine, kwa kweli CCJ ni chama mbadala wa CCM.
Swali: Je, Mna matarajio ya kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu? Kama ndiyo mtasimamisha mgombea urais?
Kiyabo: Ndiyo, hilo ndiyo lengo letu kubwa. Lazima tusimamishe mgombea urais na wagombea wengine nchi nzima bara na visiwani. Hivi sasa tayari tumeshapata wanachama 2000 hapa Dar es Salaam tu na wengine kutoka mikoani wameshaanza kutuulizia, hivyo tuna uhakika wa kukamilisha masharti ya usajili wa kudumu hivi karibuni. Tunataka hadi ifikapo mwisho wa mwezi Februari tuwe tumekamilisha masharti ya msajili wa vyama vya siasa. Tunajua msajili hatatuangusha.
Swali: Kabla ya kuanzisha chama hiki ninyi mlianzia siasa wapi?
Kiyabo: Mimi (Richard Kiyabo) ni mjasiriamali, sitasema nafanya nini hasa lakini ijulikane tu hivyo.
Nilizaliwa mwaka 1965. Nina taaluma ya sosholojia niliyoipata nje ya nchi na sasa ninachukua shahada ya uzamili katika chuo kimoja huko Marekani. Isitoshe nilikuwa mwanachama wa CCM kabla ya kuunda chama hiki.
Muabhi: Kwa upande wangu (Renatus Muabhi), nina miaka 41 na ni mwenyeji wa Musoma mkoa wa Mara, kwa sasa ninafanya kazi zangu binafsi.
Kabla ya kuingia kwenye siasa nilikuwa mwanajeshi. Nimestaafu baada ya kulitumikia jeshi kwa zaidi ya miaka 20. Kuna taratibu za jeshi ambazo zinaruhusu askari kustaafu kwa hiari anapofikisha miaka hiyo ya utumishi. Mimi pia nilikuwa mwanachama wa CCM.
Swali: Kwanini umestaafu jeshi mapema na kujiunga na siasa, au uliona maisha ya jeshini ni magumu sasa umeona uingine kwenye siasa ili kuganga njaa?
Muabhi: Hapana, sikuingia kwenye siasa kuganga njaa. Nimestaafu jeshini kwa taratibu zote, na nilikuwa nalipwa vizuri na sasa nimekamilishiwa mafao yangu mazuri tu. Kwa hiyo nilijiandaa na maisha vizuri na jeshi pia liliniandaa vizuri. Nimeingia kwenye siasa kutokana na kuwa na uchungu wa nchi yangu.
Maisha ya Watanzania yanatia uchungu, angalia jinsi ufisadi unavyoifilisi nchi. Wakati vigogo serikali wanajichotea fedha wananchi wanateseka. Angalia kwa mfano ubinafsishaji wa shirika la reli, watu wanataabika na mizigo yao wakisubiri usafiri kwa sababu tu ya mfumo mbovu wa ubinafsishaji.
Angalia jinsi wananchi walivyopigwa mabomu kule Mbagala na wengine wanabomolewa nyumba kule Kipawa. Angalia hali ya hospitali zetu kama vile Muhimbili, wagonjwa wanakosa hata vitanda.
Sisi tumekuja kurudisha matumaini ya Watanzania yaliyofifia.
Swali: Katika maisha yako ya ujanani uliwahi kufikiria kuingia kwenye siasa?
Muabhi: Hapana, unajua mambo ya siasa hayapangwi, ila kuna wakati tu ukifika mtu unavutiwa na siasa basi unaingia. Na mimi nimeingia kwa jinsi hiyo.
Swali: Ni mwanasiasa gani anayekuvutia katika maisha yako?
Muabhi: Mwanasiasa anayenivutia hayupo kwa sasa. Nilikuwa namhusudu Mwalimu Nyerere hasa kwa uzalendo wake, aliweza kutetea maslahi ya Watanzania kuliko Watanzania wengine.
Swali: Inasemekana kuwa mnatumiwa na vigogo fulani?
Kiyabo: Watu wanasema hivyo kwa sababu, ya matatizo yaliyomo kwenye vyama vyao. CCJ haikuanzishwa kwa migongo ya watu fulani. Tunaendelea kusisitiza kwamba tumeianzisha kwa malengo ya ustawi wa Watanzania