JANA Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, alitoa cheti cha usajili wa muda kwa Chama Cha Jamii (CCJ), baada ya kupokea maombi ya chama hicho na kuyafanyia kazi kwa zaidi ya miezi miwili.
Makumi ya mashabiki na wafuasi wa chama hicho walikuwepo kwenye ofisi za msajili kushuhudia tukio hilo muhimu kwa chama chao chenye maskani yake Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Kwa mbwembwe na tambo, wafuasi wa CCJ walibeba mabango huku wakifurahia hatua hiyo. Nawapongeza kufikia hapo.
Hii ilinikumbusha miaka kadhaa nyuma wakati wa kusajiliwa kwa Chama cha Democratic (DP) chini ya uenyekiti wa Mchungaji Christopher Mtikila, ambacho sasa kimebaki kwenye historia na orodha ya vyama vyenye usajili wa kudumu nchini.
Mamia ya wafuasi wa DP, wakazi wa Dar es Salaam na viunga vyake wakisindikizwa na ngoma ya mdundiko walikuwepo nje ya ofisi za msajili hali iliyomlazimu kukabidhi cheti cha usajili nje ya ofisi kutokana na wingi wa watu japo kwa jana, hali haikuwa hivyo.
Baada ya kukabidhi cheti cha usajili wa muda, kwa mara nyingine Tendwa alirudia kauli yake kwamba CCJ haiwezi kushiriki kwenye uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.
Msajili huyo alieleza sababu za chama hicho kutoshiriki kwenye uchaguzi huo kuwa ni muda wa kukamilisha taratibu za kuwasilisha majina ya wanachama 200 kila mkoa kwa mikoa 10 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambao ni miezi sita kwa ajili kupata usajili wa kudumu kabla ofisi ya msajili nayo kutumia muda wake kuhakiki majina hayo.
Miezi sita kutoka siku waliyopokea cheti cha usajili wa muda ni Septemba 2 mwaka huu kipindi ambacho kampeni za wagombea mbalimbali waliosimamishwa na vyama vyao zitakaposhika kasi.
Si hivyo tu, kwa mujibu wa Tendwa mchakato wa kuwapata wagombea watakaowakilisha vyama vyao kwenye uchaguzi kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani zinaanza Mei mwaka huu.
Katika akili ya kawaida, naona wazi kwamba hata CCJ wakipeleka majina ya wanachama wao mwezi mmoja baadaye, sina hakika kama ofisi ya msajili itaacha kila kitu na kushughulikia chama hicho.
Inaingia akilini mwangu kwamba sheria inamtaka msajili kupata majina ya wanachama 200 kila mkoa kwa mikoa 10 nchini kisha kuyahakiki na kujiridhisha kabla ya kuwapa usajili wa kudumu utakaowaruhusu kushiriki kwenye uchaguzi ujao. Sasa muda wa kukamilisha haya utatosha kabla ya Septemba?
Japo si kazi ndogo kuwapata wanachama hao, ila muda waliopewa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 ikifuatwa ipasavyo, ni wazi kwamba chama hicho hakitashiriki kwenye uchaguzi.
Katibu wa CCJ, anajitapa kuwa chama chake kipo tayari kumaliza kazi ya kuzunguka mikoa 10 katika kipindi cha mwezi mmoja kutoka sasa. Hili linawezekana ingawa litaacha maswali mengi ikiwemo ya wao kuvunja sheria za usajili wa vyama vya siasa inayowazuia kufanya shughuli zozote za chama kabla ya kupata usajili wa muda.
Msingi wa mtazamo wangu ni mkanganyiko na mlolongo wa matukio uliokuwepo kabla na baada ya CCJ kupata usajili wa muda hali inayoniacha na swali pengine ujio wa chama hiki ni mkakati wa CCM ama usalama wa taifa kutaka kuchafua hali ya hewa kwenye kambi ya upinzani.
Chama hiki kilianza kusikika mwishoni mwa mwaka jana ingawa hakikupewa nafasi masikioni mwa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania. Januari mwaka huu kikaja kwa kasi na kubeba uzito wa juu kwenye vyombo mbalimbali vya habari.
Kilipoanza, baadhi ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walihusishwa nacho ingawa wapo waliokanusha na wengine kuendelea kuwa kimya hali inayonipa majibu ya kwamba ni kweli wanahusika.
Vigogo wanaohusishwa na CCJ ni Spika wa Bunge Samuel Sitta, makundi ya wanachama watiifu wa CCM walio mstari wa mbele kupambana na ufisadi, ambao wote leo hii wamekula matapishi yao kwa kukubali kufungwa midomo kwa vitisho na hofu ya kutopitishwa kwenye kura za maoni wakielekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Wakongwe wengine wanaotajwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, John Malecela na wengine.
Ujio wa chama hiki kwa kiasi kikubwa ninaamini una mkono wa vijana kutoka usalama wa taifa na kwenye kambi ya siri ya watawala wetu wakubwa ambao wapo tayari kutumia gharama zozote kujisafisha machoni pa wapiga kura ili waendelee kututawala.
Japo wananchi waliaminishwa kupitia taarifa mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya habari kwamba kuna hofu ya kumeguka na kuyumba kwa CCM ambacho ni chama kikongwe nchini baada ya CCJ kujitokeza, baada ya kutafiti dhamira yangu inakataa kulikubali hili.
Zipo pia taarifa za kuaminika kwamba vijana wanaoongoza CCJ kwa muda wapo kwenye kile tunachokiita ‘system'. Kwa akili yangu, ninaamini kabisa kuwa wapo kwa ajili ya kazi maalum ya kuusambaratisha upinzani na kuwavuruga Watanzania walio mashabiki wa siasa.
Hawa wameamua kuchezea kivuli cha CCM ili kupima nguvu ya wapinzani wanaoonyesha kukubalika zaidi Tanzania Bara, huku viongozi wa chama tawala wakitumia nguvu kidogo kuipaka matope CCJ kana kwamba hawajui kinachoendelea. Binafsi siipendi siasa kutokana na wengi wa waliomo ndani yake kuwa ‘wasanii', ingawa napenda kuwaona wanasiasa wanavyoshindwa kueleza ukweli umma wanaouongoza, badala yake wanauma maneno hasa kipindi cha uchaguzi.