Na ingekuwa ni vyema Makamba akajibu a kuhusu hili la Wangwe kutaka kuhamia CCM.Hii ni habari nene..
Nimeambiwa habari hii iko katika Gazeti la Raia mwema la leo,nimemwambia jamaa aliscan na anitumie..
Na Kizitto Noya
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, kumhoji Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, kuhusu kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema jana kuwa, chama chake kina wasiwasi na jinsi CCM ilivyopata waraka wa marehemu kuhusu mgogoro wake na Chadema na kuanza kuusambaza siku moja kabla ya kifo chake.
Alisema, Makamba anapaswa kuhojiwa ili aeleze uhusiano wake na marehemu ambaye alikuwa Mbunge Chadema, hata akapata nyaraka hizo za siri katika kipindi kifupi kabla ya kifo chake na kuzisambaza.
''Hatutaki kuhitimisha kwa sababu sisi ni wanademokrasia, ila tunataka IGP sambamba na maombi yangu ya awali ya kumhoji Mkurugenzi wa TBC1, amhoji Makamba ili tujue uhusiano wake na marehemu na jinsi alivyopata waraka huo na kuusambaza siku moja kabla ya kifo chake,'' alisema Kabwe na kuongeza:
''Waraka huo ulipotolewa kwa mara ya kwanza na TBC1, mimi (Kabwe) nilikuwa na mashaka na Jumamosi iliyopita, niliwasiliana na IGP na Mkuu wa Usalama wa Taifa kuwataka wamhoji Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya umma. Lakini leo (jana) tumefumbuliwa macho kwamba waraka huo ulianzia CCM na ikabidi niwasiliane naye (IGP), tena ili zoezi hilo limguse pia Makamba,'' alisema.
Alisema Makamba anapaswa kueleza alikopata waraka huo na sababu za kutumwa kwake muda mfupi kabla ya kifo cha marehemu ikiwa ni pamoja na msukumo uliomfanya ausambaze kwa viongozi wa CCM.
Kwa mujibu wa Kabwe, sheria ya usalama wa taifa ya mwaka 1996 inatambua ndugu wa marehemu kuwa wamiliki wa mali na taarifa muhimu zinazomhusu marehemu, hivyo ni ajabu CCM kumiliki waraka huo wakati haina uhusiano wa kindugu wala kiitikadi na marehemu Wangwe.
''Hivi CCM ina uhusiano gani na mbunge wa Chadema au ndugu wa marehemu hata ikahalalisha kumiliki waraka huo na kuusambaza bila woga?'' alihoji Kabwe na kusisitiza kuwa Chadema haijauona waraka huo na wala kuambiwa na ndugu wa marehemu.
Akizungumzia suala hilo, Makamba alikanusha kuhusika na waraka huo na kueleza kuwa, CCM haina haja wala sababu ya kuwa nao na kuusambaza.
Alisema CCM haihusiki na waraka huo na kubainisha kuwa wanaofanya hivyo ni watu wanaomwunga mkono marehemu Wangwe katika migogoro yake na chama chake.
''Mimi sijauona waraka wenyewe na sina taarifa nao, lakini kwa nini CCM iusambaze, ina shida gani na Chadema?'' alihoji na kuongeza:
"Chadema sisi hatuiogopi, tuliishinda Jimbo la Kiteto na tutaishinda mwaka 2010, hatuna haja nayo wala haitusumbui."
Kauli za Makamba na Zitto zimefuatia taarifa kwamba, CCM imekuwa ikisambaza waraka wa marehemu Wangwe wenye kurasa sita unaoelezea jaribio la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kutaka kumvua wadhifa wake na uanachama.
Waraka huo unadaiwa kusambazwa kwa viongozi wa CCM kwa lengo la kuwafahamisha mgogoro wa Chadema ambao umekuwa ukihusishwa na chanzo cha kifo cha mbunge huyo.
Ukurasa wa nne wa nakala ya waraka huo unaonyesha kwamba, kwa mara ya kwanza ulitumwa kutoka Dodoma Julai 27 mwaka huu majira ya saa 9:42 alasiri toka namba (026) 2322965 ambayo imeonyesha kusajili kwa jina la KATIBU MKUU CCM DOM tarehe ambayo ni siku moja kabla ya kifo cha Wangwe.
Uchunguzi umebaini kuwa waraka huo ulianza kusambazwa kutoka Dar es Salaam kwa namba za faksi 2667457 iliyotanguliwa na kodi namba ya mkoa (022) ikimaanisha kutumwa kutoka Dar es Salaam Julai 31, mwaka huu saa 5:50 asubuhi na mmiliki wa namba hiyo akitambuliwa kama SIGMA ICT.
Waraka huo, umetumwa kwa baadhi ya viongozi wa CCM mikoani, wakiwemo Makatibu wa Mikoa na Wilaya na wengine ukiwa ni mahususi kwa ajili ya kuwaonyesha kwa kina mgogoro wa Chadema ulivyo.
''Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa 2005, Mbowe alitufahamisha wanachama kuwa alikuwa anakidai chama dola za Kimarekani 181,949.00, sawa na Sh 218,338,546 na mpaka sasa chama kimemlipa Sh175 milioni.
''Baada ya kupata wadhifa wa Makamu Mwenyekiti na kwa kuzingatia takwimu zionekanazo hapo juu katika kulinganisha matumizi ya fedha wilayani na makao makuu, niliamua kumshauri Mbowe asitishe kujilipa deni kutokana na fedha za ruzuku, kwani siamini kuwa kulipa madeni yaliyopita kunaendana na utaratibu wa usimamizi wa pesa za ruzuku kwa vyama vya siasa kutoka serikali.
''Mbowe alichachamaa na ndipo nilipomshauri kuwa kama ni hivyo, basi atuthibitishie pesa hizo anazodai alikopesha chama ziliingia kwenye akaunti gani ya Chadema kupitia hundi ipi na lini?'' ilieleza sehemu ya waraka huo.